Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Asisitiza Kuwatumia Wachezaji Wenye Asili ya Tanzania Walio Nje ya Nchi. Aagiza Wizara Husika Zikutane

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace  Karia  hundi ya Shilingi milioni 500 ikiwa ni ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu, Taifa Stars baada ya kufuzu michuano ya AFCON ya mwaka 2024. Makabidhiano hayo yalifanyia katika uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salam, Oktoba 4, 2023. Wa pili kushoto ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila

Na Shamimu Nyaki

Waziri  Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ifanye kikao na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuona namna ya kuwatumia  wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza nje, ili wapate nafasi ya kuitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania.

Mhe. Majaliwa ametoa agizo hilo Oktoba 4, 2023 Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kuwapongeza na kukabidhi Hundi ya Shilingi Milioni 500 kwa  Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars), ikiwa ni zawadi ya Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan baada ya timu hiyo kufuzu kucheza michuano ya AFCON mwaka 2023 itakayofanyika mapema mwakani nchini Ivory Coast.

"Nawaelekeza Wizara ya fedha kuhakikisha fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa zinafika kwa wakati ili ukarabati ukamilike kabla ya mashindano ya AFCON mwaka 2027 kwa kuwa nchi yetu ndio muandaji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda. Pia asilimia 5 inayotengwa kutokana na mchezo wa kubashiri kwa ajili ya Mfuko wa michezo ifike kwa wakati" amesisitiza Mhe. Majaliwa.

Ameilekeza pia Wizara ya Utamaduni, ishirikiane na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo Tanzania kuandaa mpango thabiti wa kuhakikisha unawezesha Taifa Stars kuwa na maandilizi mazuri na kuelekea mashindano ya AFCON mwaka 2023 na mwaka 2027 ili Timu hiyo ifanye vizuri.

Ameipongeza Wizara na Shirikisho hilo ihakikishe Tanzania inafanikiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON mwaka 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda huku akiviasa vilabu vinavyoshirirki mashindano ya Kimataifa vifanye vizuri kwa kuwa Goli la Mama bado linaendelea.

Awali Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema Sekta ya Michezo inaendelea kufanya vizuri kwa kuwa hivi karibuni timu za Mpira wa Miguu za Wanawake Serengeti Girls na timu ya JKT Queens zilitwaa Ubingwa wa CECAFA na JKT Queens itashiriki Klabu Bingwa Afrika.

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema mwezi Novema hadi Disemba wataendesha mashindano ya Mpira wa Miguu kwa wanaume na Wanawake chini ya miaka 17 Jijini Mwanza lengo likiwa ni kupata wachezaji wengi watakaotumikia Timu za Taifa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka wa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro (wa tatu kushoto) kuhusu ukarabati wa Uwanja wa Taifa wakati alipokagua ukarabati huo jijini Dar es salaam, Oktoba 4, 2023. Kushoto kwake  Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka wa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro (wa tatu kushoto) kuhusu ukarabati wa Uwanja wa Taifa wakati alipokagua ukarabati huo jijini Dar es salaam, Oktoba 4, 2023. Kushoto kwake  Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia.Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya kukabidhi  hundi ya Shilingi milioni 500 ikiwa ni ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu, Taifa Stars baada ya timu hiyo kufuzu michuano ya AFCON ya mwaka 2024. Hafla hiyo ilifanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Oktoba 4, 2023No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.