Habari za Punde

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuleta mabadiliko sekta ya elimu


Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema itaendelea kuzitatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ili kuweza kuleta mabadiliko katika sekta hiyo.
Akizungumza na Walimu Wakuu,Wenyeviti wa Kamati za Skuli pamoja na Viongozi wa Jimbo la Chumbuni ,katika Kikao cha kutathmini maendeleo ya Elimu katika Jimbo hilo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe.Lela Muhamed Mussa,amesema Wizara imo katika maboresho ya Sekta ya Elimu kwa kujenga majengo mapya ya ghorofa ili kupunguza idadi ya wanafunzi madarasani na kuondoa utaratibu wa wanafunzi kuingia mikondo miwili.
Aidha amewataka Walimu Wakuu na Wenyeviti wa Kamati za Skuli kuisimamia programu kwa wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika ili kupunguza wimbi la watoto wasiojua kusoma na kuandika.
Pia amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itaendelea kutoa. kipaumbele cha ajira kwa walimu wa masomo ya Sayansi ili kuongeza kiwango cha ufaulu wa masomo hayo kwa Skuli za Zanzibar.
Nae Muwakilishi wa Jimbo la Chumbuni Ndg. Miraji amesema, lengo la Kikao hicho ni kutathmini na kutafuta njia sahihi ya kutatua changamoto zinazoikabili Sekta ya Elimu kwa upande wa Skuli ya Jimbo hilo.
Wakitoa michango yao Walimu wa Skuli za Jimbo hilo wamesema,kuwa uchakavu wa majengo,uhaba wa viti vya kukalia, vyoo na vifaa vya kufanyika kazi ni miongoni mwa matatizo yanayorejesha nyuma juhudi za maendeleo ya kielimu ndani ya Jimbo hilo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (WEMA )

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.