Habari za Punde

UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI SKULI YA MSINGI KIJIDICHI

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma akiweka jiwe la msingi skuli ya msingi kidichi ikiwa ni maadhimsho ya miaka 60 ya mapiduzi

PICHA NA MAELEZO

NA SABIHA KHAMIS, MAELEZO. 05/01/2024.

 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amesema umoja na mshikamano ndio msingi wa maendeleo katika Nchi.

 

Ameyasema hayo huko Kidichi Wilaya ya Magharib "A" katika uwekaji wa jiwe la msingi Skuli ya Msingi Kidichi, ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Amesema ili nchi iwe na maendeleo lazima kuwepo na umoja na mshikamano kwa wananchi wenyewe jambo ambalo litapelekea kuimarisha uchumi wa nchi na kupiga hatua katika maendeleo.

 

Alieleza kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964 yamewakomboa na kuwaweka huru Wananchi wa Zanzibar na kuweza kujitegemea katika masuala mbalimbali ikiwemo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

 

Amefahamisha kuwa mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar Serikali ilitangaza elimu bure ili kuwawezesha wananchi kupata elimu bora na stahiki kwa Wazanzibar wote.

 

"Kabla ya Mapinduzi elimu na huduma nyengine zilikuwa ni haki za wachache na ilikuwa haiwafikii walio wengi hasa wanyonge" alisema Waziri.

 

Aidha amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka Mazingira rafiki ya elimu Wananchi wa Mjini na Vijijini bila kuwepo ubaguzi wa aina yoyote.

 

"Niipongeze Serikali ya awamu ya nane kutoa kipao mbele katika sekta ya elimu kwa kutengeneza Mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia" alisema Waziri.

 

Hata hivyo amewataka wananchi kuitunza miundombinu ya elimu inayowekwa na Serikali ili kuweza kupata Wataalamu wazalendo wa kuijenga Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

 

Sambamba na hayo amesema kuwepo Ujenzi wa Miradi ya maendeleo itasaidia kupunguza wimbi la mrundikano wa Wanafunzi Madarasani na kuwawezesha Wanafunzi kuingia Skuli kwa awamu moja tu (asubuhi).

 

Mbali na hayo amewataka Wazazi kufuatilia mahudhurio ya watoto wao ili waweze kufanya vizuri sambamba na Walimu kuwasimamia Wanafunzi wao ili waweze kupata elimu bora inayoendana na wakati uliopo wa Sayansi na teknolojia.

 

 Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa Skuli hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Mwanahamis Ameir Mohamed amesema kuwa mradi huo utasaidia kuimarisha Mazingira bora ya upatikanaji wa elimu na kupunguza Idadi kubwa ya Wanafunzi hadi kufikia Wanafunzi 45 kwa kila darasa.

 

Amesema skuli hio ya kisasa itakuwa ya ghorofa mbili yenye madarasa 29, vyoo 25, ofisi 4 za walimu, ukumbi mmoja wa mitihani pamoja na chumba kimoja cha tehama na maktaba moja.

 

Jumla ya shilingi Bilioni 4.5 zitatumika katika ujenzi wa mradi huo ambapo Skuli hiyo ya kisasa, itakuwa ya ghorofa mbili, Madarasa 29, Vyoo 25,Ofisi 4 za Waalimu Ukumbi wa Mitihani,Chumba cha Maktaba na Tehama na unatarajiwa kukamilika mwaka huu 2024.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.