Jamhuri ya Muungano wa Tanzania …
1.
Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha
sisi sote kukutana hapa Tanga leo ili kuzindua uuzaji wa Hatifungani ya kijani
kwa ajili ya kupata fedha za mradi wa kuboresha miundombinu ya maji katika Jiji
la Tanga na Wilaya za Muheza, Pangani na Mkinga. Nawashukuru na kuwapongeza washiriki wa hafla hii muhimu sana. Naipongeza Kamati
ya Maandalizi na wote waliofanikisha
tukio hili.
Wahe. Viongozi na Ndugu Washiriki;
2.
Mnamo tarehe 25 Oktoba 2021, Mheshimiwa Dkt.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokutana na
ujumbe wa Shirika
la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Mitaji (UN Capital Development Fund-UNCDF), Ikulu ya Dar es Salaam, aliridhia na
kuelekeza kutumika kwa Hatifungani katika ngazi ya Serikali za Mitaa na Taasisi
nchini kama njia mbadala ya kibunifu ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha
za miradi ya maendeleo. Kufuatia hatua hiyo, Kamati ya Kitaifa ya wadau kuhusu
uuzaji wa hatifungani kwa Taasisi za Serikali (National Municipal and Sub National Bond Stakeholders Taskforce)
iliundwa. Wizara ya Fedha nayo iliunda na kuzindua Timu ya Kitaifa ya
Uwezeshaji (National Facilitation Team (NFT)) mnamo tarehe 24 Februari
2022
Wahe. Viongozi na
Ndugu Washiriki;
3.
Uamuzi huu wa Serikali unatokana na ukweli
kwamba Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
(2021/22-2025/26)– 2025/26 una mahitaji makubwa ya rasilimali fedha
ikilinganishwa na ukomo wa vyanzo vilivyozoeleka vya kupata fedha za maendeleo.
Vilevile, uwekezaji katika kuendeleza miundombinu ya huduma ya Maji unahitaji
rasilimali fedha nyingi ili kumaliza kero ya upatikanaji wa maji safi na
salama.
Wahe. Viongozi na
Ndugu Washiriki;
4.
Natambua kwamba, Tanga UWASA imekidhi vigezo na kupata idhini ya kuuza
Hatifungani hii kutoka kwenye mamlaka
mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana na Wizara ya
Fedha. Nawapongeza kwa dhati Mawaziri na
Makatibu Wakuu wa Wizara ya Maji, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais Mipango na
Uwekezaji, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana
(CMSA) kwa kufanikisha mpango huu. Vilevile, nalishukuru Shirika la Umoja wa
Mataifa la Maendeleo na Mitaji (UNCDF) kwa kufadhili na kuratibu mchakato mzima
wa jambo hili.
Wahe. Viongozi na
Ndugu Washiriki;
5.
Kama mlivyoeleza kwenye taarifa yenu, Hatifungani hii
itasaidia kuongeza kiasi cha maji yanayozalishwa kutoka lita milioni 42 hadi
milioni 60, kuongeza upatikanaji wa maji katika jiji la Tanga kutoka asilimia
96 hadi takriban asilimia 100 ifikapo Juni 2025. Kuongeza mtandao wa maji
katika miji ya Muheza na Pangani kutoka asilimia 70 hadi zaidi ya asilimia 95
ifikapo Juni 2025. Mradi huu utanufaisha zaidi ya wananchi 458,365 waliopo
katika jiji la Tanga na miji ya Pangani na Muheza. Pia kupata maji ya kutosha
kwa ajili ya wananchi wapatao 74,124 wa wilaya ya Mkinga.
6.
Nimefurahi kuona utekelezaji umeanza, maana
kabla ya kufika ukumbini nilipata fursa ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa
Mradi huu kwenye eneo la Mtambo wa Kusafisha na Kutibu Maji wa Mowe, Kata ya
Kiyomoni. Nawapongeza sana Tanga UWASA kwa kuweza kuanza utekelezaji wa sehemu
ya mradi huu kwa fedha za mkopo wa
Shilingi bilioni 7.6 kutoka Benki ya TIB kupitia Mpango wa Investment
Facility Financing - Output Based Aid (IFF-OBA) ambao ulibuniwa kwa kushirikiana
na Shirika la KfW la Serikali ya Ujerumani.
Wahe. Viongozi na Ndugu Washiriki;
7.
Njia hii ya matumizi ya Hatifungani ni
nzuri kwa kuwa inaruhusu ukopaji wa muda
mrefu na uwezekano wa kupata fedha nyingi zaidi kwa wakati mmoja, hivyo
kuzisaidia Taasisi zetu kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati na kuboresha
huduma kwa wananchi. Napenda kutumia fursa hii tena kuwapongeza sana Bodi ya Wakurugenzi,
Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Tanga UWASA kwa kuwa na uthubutu na
kutufungulia njia hii mbadala ya kupata fedha za kugharamia miradi ya
maendeleo. Ni imani yangu kuwa hamtashawishika kuwekeza fedha za hatifungani
hii yenye riba ndogo katika fursa nyingine (arbitrage profit). Mkifanya hivyo,
kuna hatari ya kupoteza imani ya wadau kutumia njia hii kama malengo yake
hayatafikiwa (reputational risk).
8.
Napenda kuhitimisha kwa kutoa maelekezo juu
ya mambo ya kuzingatia, kama ifuatavyo:
Kwanza, Hatifungani
tunayozindua leo iwe ni chachu na motisha kwa Halmashauri na taasisi nyingine zikiwemo
Halmashauri kutumia njia hii ya kupata fedha za miradi ya maendeleo. Hivyo
naielekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kama msimamizi wa Taasisi na Mashirika ya
Umma nchini na Waziri wa OR-TAMISEMI kama msimamizi wa Halmashauri, kuona namna
Taasisi, Mashirika na baadhi ya Halmashauri
zinavyoweza kutumia dirisha hili la Hatifungani kuharakisha utekelezaji
wa miradi na kutoa nafasi kwa Serikali kujikita kwenye maeneo mengine ya kipaumbele
ambako hakuna uwezeshaji wa aina hii.
Pili, naitaka Bodi
ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Tanga UWASA, kusimamia
vizuri matumizi ya fedha zitakazopatikana kupitia Hatifungani tunayoizidua leo
na mapato mengine mtakayokusanya baada ya kukamilisha mradi huu. Nidhamu ya
fedha na usimamizi thabiti ndiyo utakaowawezesha kurejesha kwa wakati fedha za
wawekezaji wa Hatifungani hii. Serikali haitavumilia uzembe wa aina yoyote
utakaoonekana kukwamisha jitihada hizi za Mheshimiwa Rais.
Tatu, natambua kwamba
Mamlaka zetu za Maji kwa kiwango kikubwa zinafanya vizuri. Napenda kuwakumbusha
Tanga UWASA kuongeza ufanisi katika uendeshaji wenu ili urejeshaji wa
Hatifungani hii usiwe sababu ya kuzorota kwa huduma au ongezeko la bei za maji.
Nne, Mamlaka ya
Masoko ya Mitaji na Dhamana kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Mipango na
Uwekezaji na Wizara ya Maji, iweke utaratitu na mfumo wa tahadhari (early warning system) ili kufuatilia na
kubaini mapema vihatarishi vinavyoweza kujitokeza.
Tano, kwa kuwa urejeshaji wa fedha hizo ni kwa mkupuo baada ya kuiva kwa
Hatifungani, inaweza kuleta changamoto wakati wa malipo. Hivyo, ni vyema
kujipanga mapema, ikiwezekana
kufungua mfuko maalum wa kukusanya kidogokidogo fedha za marejesho (sinking
fund). Lakini napenda nikiri kuwa nimefurahishwa na wazo la kibunifu la matumizi
ya dira za malipo ya awali (pre-paid meters), naamini litasaidia kuongeza
ufanisi wa ukusanyaji mapato na hivyo kuwajengea uwezo wa kulipa.
Wahe. Viongozi na
Ndugu Washiriki;
9.
Ninapofikia tamati ya hotuba yangu napenda
kutumia jukwaa hili kuwaalika na kuwahamasisha wawekezaji wote wa ndani na nje
ya nchi, mifuko ya hifadhi za jamii, mifuko ya bima, taasisi mbalimbali, sekta
binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi kwa ujumla kushiriki katika ununuzi wa
hatifungani hii ili kupata faida na wakati huo huo kuwekeza katika maendeleo ya
jamii nzima.
10. Baada ya
kusema hayo, sasa ninayo heshima kutangaza kuwa uuzaji wa hatifungani ya
kijani kwa ajili ya kupata fedha za mradi wa kuboresha miundombinu ya maji Tanga,
umezinduliwa rasmi.
Asanteni
sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment