Habari za Punde

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Awatembelea Wananchi Mkoa wa Kaskazini Unguja

Na.Mwandisi OMWR. 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba ziara za kuwatembelea waananchi wenye matatizo mbali mbali katika maeneo wanayoishi ni muhimu kwani ni fursa kubwa kwa viongozi katika ngazi tofauti kujifunza na kujua hali halisi ya maisha  yao waliyonayo.  

Mhe. Othman ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT – Taifa ameyasema hayo  mkoa wa Kaskazini Unguja akiwa katika muendelezo wa ziara ya kuendeleza utamaduni wa kuwatembelea wagonjwa, wenyemisiba na matatizo mbali mbali ya kijamii.

Aidha Mhe. Othman amesema mbali na hali hiyo, pia suala hilo linasaidia na linajenga matumaini ya kuwepo na kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi na wananchi sambamba na kuwepo matumaini makubwa kwa wananchi kutoka kwa viongozi wao.

Amefahamisha kwamba umuhimu wa ziara hizo pia ni viongozi kujifunza kwa uhalisia changamato za wananchi walizonazo sambamba na kutafuta mbinu za pamoja katika kuzikabili na kuweza kuzitatua changamoto hizo.

Hiyvyo  Mhe. Othman amesema kwamba   kufanya hivyo kwa viongozi ni kutekeleza wajibu mkubwa walionao  katika kuwafariji na kuwapa matumini mema wananchi katika kuendeleza umoja miongioni mwa wananchi na viongozi wao kwa ngazi mbali mbali.

Mhe. Othman amewataka wananchi na viongozi  kuendelea kuwa na umoja pamoja subra kutokana na matatizo mbali mbali yanayowafika ikiwemo ugonjwa na misiba na kumuomba mwenyezi mungu kuwarejeshea afya wale wote waliofikwa na mitihani ya maradhi na kuendelea kuwaombea dua waliotangulia.

Amewataka viongozi kuendeleza  mila hizo nzuri za kuwatembelea watu na wagonjwa mbali mbali  hasa katika kipindi kama hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani kwani ziara kama hizo ni alama za kuwakumbusha katika wajibu wa kuwa pamoja wakati wa furaha na changamoto mbali mbali .

Akizungunzia suala la nchi, Mhe. Othman amesema kwamba viongozi wamekabidhiwa dhamana na wananchi na kwamba kwa juhudi kubwa   wamekua wakifanyakazi chini ya serikali ua umoja wa kitaifa kwa kusimamia  vyema na kuwepo kwa matumaini  ya kuondosha shida mbali mbali za wananchi kupitia serikali hiyo  ili na wengine watamani  kuiga mfumo  wa serikali hiyo.

Mapema Mwenyekiti wa Chama hicho mkoa wa Kaskazini A Kichama Mcha Rajab Haji, akitoa shukrani zake kwa Mhe. Othman amesema kwamba viongozi na wananchi wamefarijika sana kwa kuwepo ziara za namna hiyo kwa kuwa zinawaweka wananchi pamoja.

Naye Katibu wa Haki za Binaadamu na Makundi Maalum wa Chama hicho Pavu Abdalla Juma, amesema kwamba ziara hizo zinaleta faraja na matumaini kwa wananchi na kwamba viongozi wamekuwa wakifanya kazi kubwa  na kwamba ameweza kutembelea zaidi nyumba 43 katika mkoa huo pekee.

Mhe. Othman tayari amefanya ziara kama hizo katika Mkoa wa Kusini Unguja, Mjini Magharib na mikoa miwili ya Pemba ambapo kesho anatarajiwa kukamilisha ziara yake hiyo katika wilaya ya Magharib A na B.

Ziara hizo ni mwendelezo wa urithi uliachwa na Mtangulizi wake Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ambazo  katika uhai wake alizifanya kila ifikapo mwenzi mtukufu wa Ramadhani kuwatembelea wagonjwa, wenye misiba na shida nyeingine mbali mbali katika visiwa vya Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.