Habari za Punde

Nchi Ilifanya Jitihada Kubwa za Kutenga Maeneo na Kuanzisha Bustani za Kijani -Dkt.Mpango

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la Kuhamasisha Uwekezaji katika Bustani za Kijani Nchini kwa Maendeleo Endelevu linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Gaspar mkoani Dodoma tarehe 15 Aprili 2024.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…

Awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kushiriki Kongamano hili muhimu. Aidha, naishukuru Taasisi ya UONGOZI, Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kuandaa Kongamano hili. Nawashukuru pia waandaaji kwa kunialika tena kuwa mgeni rasmi kwenye mwendelezo wa makongamano ya Jukwaa la maendeleo endelevu, ambapo hili ni kongamano la nane mahsusi kwa ajili ya kuhamasisha uwekezaji katika Bustani za Kijani. Asanteni sana!

 Ndugu Washiriki;

Kama mnavyofahamu, Bustani za Kijani (Green Parks) ni muhimu kwa ajili ya upatikanaji wa hewa safi, utunzaji wa vyanzo vya maji na utunzaji wa maliasili za nchi. Aidha, Bustani za Kijani zinasaidia kukabiliana na baadhi ya athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na ongezeko la joto hasa maeneo ya mijini, kupunguza vifo vinavyotokana magonjwa yanayosababishwa na ongezeko la joto na kusaidia kupunguza ongezeko la hewa ya Kaboni. Vilevile, Bustani za Kijani zinawezesha kuwepo maeneo ya kupumzika, kufanya mazoezi na michezo mbalimbali na hivyo kusaidia  kuboresha afya. Bustani za Kijani zikitunzwa vizuri zinaweza kuwa vivutio vya utalii na hivyo kuchangia pato la Taifa. Hata hivyo, pamoja na umuhimu mkubwa wa Bustani za Kijani, bado kuna mwamko mdogo wa uanzishaji, utunzaji na uendelezaji wa Bustani za Kijani. Maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya Bustani za Kijani hapa nchini hayatunzwi vizuri na baadhi yamebadilishwa matumizi, tofauti na ilivyokusudiwa awali.

Ndugu Washiriki;

Miaka iliyopita miji mingi hapa nchini ilifanya jitihada kubwa za kutenga maeneo na kuanzisha Bustani za Kijani.  Baadhi ya bustani hizo za kijani ni pamoja na iliyo mkabala na ukumbi wa Karimjee (Dar es Salaam); iliyo mkabala na Ofisi ya CCM Mkoa (Mwanza); Nyerere Square, Chinangali Park na Medeli zilizopo Dodoma pamoja na ile ya mjini Iringa iliyo nyuma ya hospitali ya Rufaa. Pamoja na msisitizo wa kuhakikisha miji na majiji yetu nchini yanatenga maeneo kwa ajili ya Bustani za Kijani, kama nilivyosema hapo awali, uwekezaji na utunzaji wa maeneo hayo bado siyo wa kuridhisha. Nchi yetu, hususan katika miji mikubwa, bado kuna uhaba wa Bustani za Kijani. Nafahamu kwamba kumekuwepo na mipango na jitihada za hapa na pale za kuanzisha na kuendeleza bustani hizi, lakini utekelezaji wake umekuwa siyo endelevu.

 Ndugu Washiriki;

Ni wazi kuwa jitihada kubwa zaidi zinahitajika ili kuhakikisha kunakuwa na mwamko wa kutosha katika kuanzisha, kuendeleza na kutunza maeneo ya Bustani za Kijani hapa nchini. Hivyo, napongeza uchaguzi wa kaulimbiu ya kongamano la mwaka huu isemayo  “Kuhamasisha Uwekezaji katika Bustani za Kijani kwa Maendeleo Endelevu Tanzania (Promoting Investments in Green Parks for Sustainable Development in Tanzania).

Changamoto kubwa inayokabili uanzishaji na uendelezaji wa Bustani za Kijani nchini ni pamoja na usimamizi dhaifu wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Bustani za Kijani, kubadili matumizi ya maeneo yaliyotengwa mahsusi kwa ajili Bustani za Kijani, mwamko hafifu wa viongozi na wananchi kulinda, kutunza na kuendeleza maeneo hayo na kutopewa kipaumbele katika bajeti za halmashauri za Miji na Majiji. Sekta binafsi nayo kwa kiasi kikubwa haijachangamkia fursa ya kuwekeza katika uendelezaji wa Bustani za Kijani. Hata hivyo, napenda kuwapongeza kwa dhati vijana na akina mama wajasiriamali wanaojihusisha na utunzaji wa vitalu vya miti na maua katika Miji na Majiji hapa nchini.  Kwa hapa Dodoma, wajasiriamali hao ni pamoja na wale waliojiajiri katika bustani ya miti ya CDA (maili mbili), Kikundi cha Chapa Kazi kilicho pembeni ya kipita shoto (round about) cha barabara ya Iringa – Kikuyu magorofani, na Chinangali Park.  Vilevile, napenda kuzipongeza taasisi za dini ambazo zimeendelea kutunza bustani ndogondogo za kijani katika maeneo yao, likiwemo eneo hili tulipo la St. Gasper na Martin Luther lililo upande wa pili wa barabara kuu ya kwenda Dar es Salaam.

Ndugu Washiriki;

Zipo nchi nyingi zilizopiga hatua kubwa katika uwekezaji kwenye Bustani za Kijani na kunufaika sana na uwekezaji huo. Baadhi ya maeneo ambayo uwekezaji mkubwa umefanywa ni kama vile Singapore, Bustani katika Mji wa Sejong (Korea Kusini), Central Park (New York), Summer Palace (Beijing), Boboli (Florence), Hampstead Heath (London), Al Azhar Park (Cairo) na bustani zilizopo Abu Dhabi na Dubai (Umoja wa Falme za Kiarabu). Umaarufu wa bustani hizi za kijani unatokana na uwekezaji, usimamizi na utunzaji mzuri wa maeneo hayo. Hivi sasa,  maeneo hayo yamekuwa kivutio kikubwa cha utalii kwa wageni mbalimbali wanaotembelea nchi hizo. Vilevile, katika baadhi ya nchi, maeneo ya Bustani za Kijani yamekuwa yakitumika kutunza mitidawa (natural herbs) au viumbe vilivyo hatarini kutoweka. Ni wajibu wetu kuiga mifano ya nchi zilizofanikiwa katika uwekezaji wa Bustani za Kijani, ili kuwezesha uwekezaji kama huo hapa nchini kwa maendeleo endelevu. Lakini, haitoshi kusifia tu bustani nzuri za kijani katika nchi nyingine. Wakati sasa umefika tutengeneze Bustani za Kijani za hapa kwetu. Tena ziwe za kiwango bora zaidi. Mimi na wenzangu tunaamini kwa dhati kabisa kwamba vijana wa kitanzania wanao uwezo mkubwa na ubunifu wa kufanya miujiza katika maeneo mengi, ikiwemo hili la Bustani za Kijani kama fursa ya ajira na chanzo cha kipato kizuri na cha uhakika.  Ninafahamu tunao vijana wazuri sana katika tasnia ya kutumia na kuboresha sura ya nchi iliyopo (landscaping). Aidha, tunao vijana wenye vipaji vya hali ya juu vya kubuni na kutengeneza aina mbalimbali za mapambo yanayoweza kutumika kwenye Bustani za Kijani na kuvutia watu wengi wakiwemo watalii kuja kuona au kununua maua, mitungi/vyombo vya kufinyanga, miti na wanyama wa kubumba n.k. yatayowekwa katika sehemu za kuingilia na ndani ya bustani hizo za kijani.

Ndugu Washiriki;

Uanzishwaji na uendelezaji wa Bustani za Kijani ni suala linalohitaji ushirikishwaji wa taasisi na wadau mbalimbali wenye utaalam au uzoefu stahiki ili kuhakikisha uendelevu wa bustani hizi na thamani ya fedha itakayowekezwa. Baadhi ya mambo yanayopaswa kuangaliwa kabla ya kuwekeza ni utambuzi na uchambuzi wa mazingira ya bustani; usanifu wa ardhi na bustani yenyewe; aina ya miti na maua yanayofaa katika eneo hilo; kubainisha vifaa vitakavyotumika; sehemu za huduma mbalimbali kama vile kupumzika, michezo na mazoezi; ukusanyaji wa rasilimali pamoja na mpango kazi wa utekelezaji. Katika muktadha huu, natoa tena pongezi za dhati kwa Taasisi ya UONGOZI, kwa kuandaa Kongamano hili ili kujadili namna ya kuvutia uwekezaji katika Bustani za Kijani, kwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali. Ni matumani yangu kuwa kupitia Kongamano hili, masuala mbalimbali muhimu yahusuyo uwekezaji na uendelezaji wa Bustani za Kijani nchini Tanzania yatajadiliwa na kuja na mkakati wa utekelezaji ili tupige hatua katika suala hili.

Ndugu Washiriki;

Ningependa kuona mijadala katika Kongamano hili ikiangazia mbinu mbalimbali za kuwekeza na kuendesha Bustani za Kijani na jinsi tunavyoweza kujifunza kutokana na uzoefu na ubunifu wa vijana wa kitanzania na ikibidi kuasili maarifa kutoka nchi nyingine; fursa na changamoto za uanzishaji, uendelezaji na uendeshaji wa Bustani za Kijani, na namna ya kukabiliana nazo; na  ushirikiano na wadau muhimu. Hivyo, matarajio yangu ni  kuwa haya yote na mengine muhimu kuhusu uwekezaji katika Bustani za Kijani yatajadiliwa kwa kina. Aidha, nitapenda kupata taarifa ya Kongamano hili na mapendekezo ya hatua za kuchukua za muda mfupi na muda wa kati katika kuendekeleza Bustani za Kijani kote nchini.

Ndugu Washiriki;

Hapo awali nilieleza kuhusu changamoto mbalimbali katika uanzishaji, utunzaji na uendelezaji wa Bustani za Kijani hapa nchini. Hivyo, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu napenda kutoa msisitizo na maelekezo kama ifuatavyo :

(i)   Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Mamlaka za Miji, Halmashauri na Majiji wachukue hatua za makusudi kulinda maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya Bustani za Kijani na kuhakikisha hayavamiwi au kubadilishwa matumizi. Maeneo hayo yapimwe na kuwekewa alama za kudumu kuonesha mipaka yake. Aidha, naagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa zitunge sheria ndogo (by-laws) na kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha maeneo ya Bustani za Kijani yanalindwa na kutumika kama ilivyokusudiwa;

 

(ii)  Mamlaka zote za Miji, Halmashauri za Wilaya na Majiji, washindanishe vijana wa kitanzania kubuni bustani bora ya kijani katika Makao Makuu ya Wilaya, Mkoa, Mji au Jiji iweje;

 (iii)    Waziri wa Nchi – OR TAMISEMI na Waziri wa Nchi – OMR washirikiane kuanzisha mashindano na Tuzo ya Kimkoa na Kitaifa ya bustani bora za kijani katika Miji na Majiji. Hili linaweza kufanyika kwa makundi ya bustani bora za kijani za watu binafsi, makampuni na Halmashauri; na,

 (iv)    Natoa wito kwa sekta binafsi (makampuni, watu binafsi, vikundi) pamoja na mashirika na taasisi za umma na AZISE bila kusahau taasisi za dini kuwekeza katika uanzishaji na uendelezaji wa Bustani za Kijani nchini kwa maendeleo endelevu.  Hii iwe ni pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi katika utekelezaji wa agenda hii muhimu. Aidha, makampuni binafsi na mashirika ya umma wajumuishe uanzishaji, utunzaji na uendelezaji wa Bustani za Kijani kuwa sehemu ya wajibu wao wa kurejesha kwa jamii (CSR).

 Ndugu Washiriki;

Mwisho, napenda  kueleza shauku niliyonayo ya kuona walau Bustani tatu mpya za Kijani zinaanzishwa hapa Dodoma kabla ya mwisho wa mwaka 2025 na mojawapo iwe Botanical Garden. Ninafahamu kuwa Mamlaka ya Jiji la Dodoma, imetenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha bustani hizo. Ninapenda kulishawishi Jiji la Dodoma lichukue hatua ya kutangaza sasa fursa ya kuwekeza katika Bustani hizi tangulizi (pioneer green parks). Hivyo, natoa wito kwa sekta binafsi kujitokeza kuwekeza katika kuanzisha bustani hizo hapa Dodoma ili pamoja na kutunza mazingira tulifanye Jiji letu kupendeza zaidi. Uzoefu kutoka nchi mbalimbali zilizopiga hatua katika eneo hili, unathibitisha kuwa uwekezaji katika kuanzisha na  kutunza bustani nzuri za kijani unalipa (profitable investment). Mkuu

Baada ya kusema hayo, ninayo heshima kutamka kuwa Kongamano la Kuhamasisha Uwekezaji katika Uendelezaji wa Bustani za Kijani nchini kwa Maendeleo Endelevu limefunguliwa rasmi. Nawatakia majadiliano mema.

 

 

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.