Habari za Punde

Kampeni ya "Soma na Mti" Yazinduliwa Zanzibar

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Gallos Nyimbo akipanda mti kuashiria uzinduzi wa kampeni ya “soma na mti” huko Skuli ya Mtule wilaya ya kusini, ikiwa ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mwazilishi wa Taasisi ya pamoja kwa Samia (together for Samia) Slim Salim Mohammed akimkabidhi mti mwanafunzi wa skuli ya Mtule wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “soma na mti” huko skuli ya Sekondari Mtule Wilaya ya Kusini.

Picha na Mpiga Wetu. 

Na Fauzia. Mussa. Maelezo. 18.05.2024.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Gallos Nyimbo ameitaka jamii kuacha kukata miti na kuendeleza kuipanda ili kukabiliana na mabadidilko ya tabia nchi na kutunza mazingira.

 

Akizingumza katika uzinduzi wa kampeni ya soma na mti, iliowashirikisha wanafunzi wa skuli ya Sekondari Mtule amesema kampeni hiyo ni chachu ya kuendeleza jitihada na harakati za uhamasishaji wa utunzaji wa mazingira katika wilaya hiyo.

 

Amesema Serikali kupitia wadau wa mazingira wanachukuwa juhudi mbalimbali ikiwemo kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala katika jamii pamoja na kuzuia ukataji wa miti hasa katika maeneo ya hifadhi.

 

"Tunaona skuli hii ilikuwa uwanda mtupu lakini saa hizi imepandwa miti, inapendeza sana, Kampeni hii ni nzuri Sana itaisaidia Wilaya yetu kuhakikisha ipo salama na misitu yetu haihujumiwi.” Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

 

Aidha amewataka wanafunzi hao,kuitunza miti hiyo ili iendelee kubaki kuwa hai na kuleta haiba nzuri ya skuli hiyo.

 

Mwazilishi wa Taasisi ya pamoja kwa Samia (TOGATHER FOR SAMIA) Slim Salim Mohammed amesema katika hatua ya awali wanatarajia kupanda zaidi ya miti elfu 20 kwa Unguja na Pemba.

 

Amesema hatua hiyo ni kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali zote mbili katika kupambana na mabadiliko ya Tabia Nchi.

 

Kwa uapnde wake Balozi wa mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano bibi Dorin Gibson amesema programu ya soma na mti, imeelekezwa kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanafunzi hao wanakuwa mabalozi wazuri kwa kulinda mazingira ndani ya skuli na jamii zao.

 

Amesema katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi, takribani miti 300 ya matunda na kivuli itapandwa katika Skuli ya Sekondari Mtule.

 

Amefahamisha kuwa mwamko wa Vijana katika kushiriki kampeni hiyo ni mkubwa sambamba na Serikali kwani Taasisi hiyo imekua ikipata usaidizi mkubwa  kutoka kwa viongozi wa Serikali wakiwemo wakuu wa Mikoa,Wilaya na walimu wa Skuli husika.

 

Nao Baadhi ya Wanafunzi walioshiriki kampeni hiyo akiwemo Sabrina abdulrahman na Murshidu Mshemba Seif wameahidi kuiendeleza  na kuitunza miti hiyo kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

 

Hata hivyo wameahidi kuwa Mabalozi wazuri wa kuelezea faida za kupanda miti kwani inasaidia kwa kupata kivuli matunda na hewa safi.

 

Zaidi ya miti elfu 20 ya kivuli na matunda itapandwa katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba, ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya soma na mti inayotekelezwa na Taasisi ya pamoja kwa Samia (together for Samia) yenye  Kauli mbiu "Zanzibar yangu, mazingira yangu, nayapenda daima"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.