Habari za Punde

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUMTUA MWANAMKE KUNI KICHWANI-KINANA

Na Mwandishi Wetu, Ngerengere

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulurhaman Kinana amesema kampeni ya nishati safi iliyoanzishwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inalenga kumtua mwanamke mzigo wa kuni kichwani na kumpa muda mwingi wa kujikita katika shughuli za maendeleo.
Akizungumza mbele ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Ngerengere, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, jana, Kinana alisema uamuzi huo wa Rais Samia unakusudia kusaidia kuwainua wanawake.

Mbunge wa jimbo hilo Hamisi Taletale alitumia mkutano huo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 na kukabidhi mitungi ya gesi ya Kampuni ya Oryx.

“Nimeona mitungi ya gesi ambayo nitaikabidhi na uwepo wa mitungi hii ni matokeo ya sera na ubunifu kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Mwaka jana Rais Samia alianzisha mchakato wa kuwatua akina mama mzigo wa kuni, kaanzisha mradi wa nishati safi na salama.

“Mwaka jana lilifanyika kongamano kubwa, lakini Rais akaona kwamba shughuli hii inahitaji fedha nyingi sana, inahitaji kuungwa mkono na dunia nzima, inahitaji msaada wa watu wenye uwezo, Rais si msemaji sana lakini ni mtendaji wa hali ya juu. Kuna msemo usemao ukitaka jambo lako lisemwe vizuri mpe mwanaume lakini ukitaka jambo lako lifanyike vizuri mpe mwanamke,” alisema.

Aliongeza kuwa uongozi wa Rais Samia umedhihirisha yeye ni mtu wa vitendo, mbunifu, anajituma, anajitolea na anatumia maarifa mbalimbali huku akifafanua hivi karibuni alikuwa Ufaransa katika mkutano wa nishati safi ambao alikuwa Mwenyekiti Mwenza uliolenga kuasidia kumtua mama mzigo wa kuni.

“Kuna maelfu ya akina mama wanafariki dunia kwa sababu ya matumizi ya kuni na mkaa, karibu watu 50,000 wanafariki kila mwaka kwa sababu ya nishati isiyosalama. Rais Dk. Samia ameamua kuanza kampeni ya kuhakikisha kila nyumba inatumia gesi ya kupika.

“Nchi yetu ina umri wa miaka 60 jambo hili halijawahi kufikiriwa wala kubuniwa, lakini Rais Samia ameona umuhimu wake, inawezekana anawajali sana Watanzania lakini ni ukweli usiopingika anawajali sana akina mama, ndio maana amelichulikua jambo hili. Sote ni mashahidi Rais alianza na kampeni kubwa ya kumtua mama ndoo kichwani na ameanza miradi mikubwa ya maji nchi nzima na miradi hii inafanyika kwa ufanisi mkubwa.

“Kuwatua akina mama ndoo na mzigo wa kuni, hii si kazi ndogo na haya ni mafanikio makubwa katika maisha ya Watanzania. Ninyi mnajua kina mama wakirahisishiwa kazi hii nchi itapiga hatua kubwa na nguzo ya familia ni mama, kina mama wachapakazi, mahodari, wanafanya kazi zao vizuri na wanafanya kazi kubwa,“ alieleza.
 

KUHUSU UCHAGUZI
Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, aliwataka wana CCM kutenda haki kwani kila mwanachama anahaki ya kuchagua na kuchaguliwa huku akifafanua wakati wa uchaguzi ukifika nafasi inakuwa wazi hivyo kila mwnye sifa anahaki sawa.

“Unakuta mwana CCM hodari, mchapakazi lakini uchaguzi ukifka atatengenezewa mizengwe ambayo haipo. Ataambiwa alikuwa tapeli, amekula hela wakati hela zenyewe hata hajawahi kuzishika. Tuwaruhusu wana CCM wapige kura wamchague mtu wanayemtaka kugombea nafasi sio mtu ambaye ametengenezwa.

“Epukeni rushwa kwani rusha ni adui wa haki, kila mtu apate nafasi sawa.Lakini na ninyi nawaomba si kila mtu anaweza kuwa kiongozi hivyo tafuteni mtu ambaye jamiiinamkubali , mtu anayejituma , mtu anayejitolea.Uchaguzi wa mwaka huu na uchaguzi wa mwaka ujao utakuwa na ushindani mkubwa kuliko mwaka 2019 na mwaka 2020,”amesema Kinana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.