Katika kukabiliana na matukio ya uhalifu yanayotokea katika
jamii tunayoishi Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi imefanya Kikao Maalumu na Viongozi wa Dini lengo
ikiwa kuhusisha kundi hilo maalumu katika kudhibiti matukio
ya uhalifu ikiwemo mauaji,mmomonyoko wa
maadili,matumizi ya dawa za kulevya na matukio mengine
yanayoweza kuvuruga amani ya nchi.
Akizungumza katika Kikao hicho kilichofanyika Makao
Makuu ya wizara Mtumba jijini Dodoma,Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni amewaomba
viongozi hao wa dini kuendelea kuisaidia serikali katika
kudumisha amani na usalama,akiwaomba kutochoka kutoa
ushauri kwa serikali katika kudhibiti matukio ya uhalifu
yanayoweza kuvuruga amani ya nchi huku akikiri kuwepo kwa
upungufu wa uhalifu nchini akiwaomba viongozi hao kuiunga
mkono serikali katika adhma yake ya kumaliza kabisa uhalifu.
‘Wajibu wa Jeshi la Polisi ni kuhakikisha ulinzi wa raia na
mali zao unaimarika na amani inatawala nchini ili kuwezesha
wananchi kufanya kazi zao za kiuchumi na kijamii na katika
kutekeleza wajibu huo Jeshi la Polisi ushirikiana na jamii na
wadau wengine na katika kipindi cha Julai,2023 hadi
April,2024 makosa makubwa ya jinai yaliyoripotiwa katika
Vituo vya Polisi yamepungua kutoka 45,485 hadi 43,146 sawa
na asilimia tano ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka
2022/2023,kwahiyo nawaomba viongozi wa dini mkaiunge
serikali mkono katika sehemu zenu mnakotoka kukemea na
kudhibiti uhalifu’ Alisema Waziri Masauni
Akizungumza wakati wa kikao hicho,Mufti Mkuu wa
Tanzania,Sheikh Abubakari Zubeir aliipongeza serikali kwa
uamuzi wa kuhusisha viongozi wa dini katika mapambano
dhidi ya uhalifu huku wakiitaka serikali kutochoka kuwaita
yanapotokea matatizo mbalimbali ili kuendelea kuimarisha
uhusiano huo.
‘Sina kumbukumbu kama tuliwahi kukaa hivi kujadili masuala
ya uhalifu tangu wakati wa viongozi wetu wa zamani ila kwa
hatua hii ya kuamua kutuita viongozi wa juu wa dini
umefanya jambo la maana sana mheshimiwa Waziri na
nikupongeze wewe na wenzako kwa wazo hili ambalo sasa
linaenda kufungua milango ya mahusiano kati ya serikali na
taasisi hizi za dini katika mapambano dhidi ya uhalifu.’
alisema Sheikh Zubeir
Akizungumzia usajili wa taasisi za kidini, Askofu wa Jimbo
Kuu Katoliki Mbeya na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania, Gervais Nyaisonga amesema serikali ipitie upya
katiba za vikundi mbalimbali vya kidini kwani kupitia katiba
zao ndio serikali itajua msingi wa shughuli za taasisi hizo za
kidini ili kuepusha baadhi ya uhalifu ambao pia unatokea
katika baadhi ya taasisi au vikundi vya kidini.
Naye Mkuu wa Kanisa Kuu la Kiinjili na
Kilutheri(KKKT),Askofu Dkt. Alex Malasusa alisema
wanaishukuru serikali kwani sasa wamepata mahali kama
viongozi wa dini ambapo wanaweza kuzungumza na kuweka
mikakati ya pamoja katika mapambano dhidi ya uhalifu na
kukubaliana juu ya maazimio yaliyofikiwa ili kuona nchi
inakua na amani na usalama.
No comments:
Post a Comment