Habari za Punde

TUENZI MAADHIMISHO YA KIISLAMU KWA VIZAZI VYETU-DKT.MWINYI*


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewahimiza wazazi, walezi, walimu na taasisi zote za elimu kutilia mkazo suala la kuenzi Maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu ili vizazi na jamii iweze kutambua  mila na desturi. 


Alhaj Dkt.Mwinyi ameyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu mwaka 1446 Hijriya katika Msikiti wa Jamiu Zinjibar Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 6 Julai 2024.


Aidha Alhaj Dkt.Mwinyi amesema suala la kutunza na kudumisha amani na utulivu ni kiini cha mafanikio ya nchi yoyote duniani na amewaomba waumini wa dini ya kiislamu kuendelea kuitunza amani kama ilivyoamrishwa na Mola Mtukufu katika kitabu chake kitukufu.

Halikadhalika Alhaj Dkt.Mwinyi amewaomba wafanyakazi wote, wafanyabiashara wakubwa na wadogo kuongeza bidii katika kazi kwa madhumuni ya kuinua uchumi wa nchi na ustawi wa watu.

Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi ameipongeza na kuishukuru Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuandaa maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu na kutekeleza majukumu yake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.