Habari za Punde

Ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Pemba

 Na..OMWKR.

Mwenyekiti wa Chama cha ACT – Taifa Mhe. Othman Masoud Othman ameseama kwamba kuwepo kwa mamlaka katika nchi ndio kuhuwika kwa uchumi wa taifa lolote duniani bila hayo hayo nchi haiwezi kupata maendeleo.

Mhe. Othman ameyasema hayo huko katika Viwanja vya Laurent Ole wilaya ya Chake chake  Mkoa wa Kusini Pemba alipozungunza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho akiendelea na ziara yake katika kisiwa cha Pemba.

Mhe. Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesisitiza kwamba bila kuwepo  hali kama hiyo taifa litaendelea kudamirika na kukumbwa na umasikini na kushindwa kupata maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Amefahamisha kwamba nchi mbali mbali duniani zikiwemo ndogo kwa ardhi na idadi ya watu kuwa ndogo pamoja na rasilimali zake kuwa chache kuliko ilivyo Zanzibar, lakini uchumi wao umeweza kupiga hatua kubwa kuliko Zanzibar kutokana na kuwa na mamlaka na viongozi wao kuwa na maono na uwajibikaji wa kizalendo kuitumikia nchi yao.

Amewataka wananchi wa Zanzibar kutoendelea kudanganyika na kughilibika na badala yake washirikiane kwa kukiunga mkono chama hicho cha ACT ambacho kimejipambanua katika kuleta mabadiliko na Zanzibar yenye mamlaka kamili.

Aidha amewataka wananchi hasa vijana kuendelea kuwa na tafakuri ya kina  juu ya masuala mbali mbali yanayojitokeza hasa kwenye ajira  kutokana na ahadi zinazowekwa kwamba mara nyingi huwa sio za kweli.

Hata hivyo Mhe. Othman amesema kwamba uchumi uliopo  Zanzibar licha kwamba ni mdogo lakini iwapo utasimamiwa vyema unauwezo wa kuivuusha Zanzibar katika tatizo la umasikini na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Amefahamisha kwamba chama chake cha ACT  kina dhamira ya kweli ya kuisaidia Zanzibar na kuwataka kujenga imani na mashirikiano kwa viongozi wa chama hicho ili kuendelea kuitetea nchi yao hasa kwa vile hawana mahala pengine pakukimbilia na jambo pekee lenye ulazima kwao ni nguvu za pamoja za  kuipambani .

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Ismail Jussa Ladhu, amewataka wazanzibari kuendelea kumuunga Mkono na kumpa mashirikiano Mwenyekiti wa Chama cha ACT Mhe. Othman Masoud  kwa kuwa ni kiongozi aliyenania ya na msimamo wa kweli katika kuwatetea wazanzibari na Zanzibar ili  kutimiza dhamira ya chama hicho ya kuleta mabadiliko  ya kweli kimaendeleo.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho Mansour Yousuf Himid, amewataka wazanzibar kutohadaliwa kwa  kutegemea kupatiwa ajira na mafanikio na kwamba ni muhimu kuwa na mamlaka ili kuudhibiti uchumi wa Zanzibar uweze kuwanufaishi wananchi wenyewe.

Amesema Karume alitangaza mapinduizi ili kuwafanya watu wote kuwa sawa na kwamba dhamira ya mapinduzi ni kuondoa matabaka jambo ambalo hivi sasa limekuwa likiendelezwa kwa wafuasi wa upinzani kubaguliwa.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho Khadija Anuari , amesema kwamba wanachama hasa vijana wasiogope vitisho na kwamba waendelee kuweka  na kusimamia dhamira yao ya kueleta mabadiliko kwa kuwa ipo pale pale .

Amesema kwamba vijana wa kizanzibari wamekosa matumaini licha ya kujitahidi kusoma, lakini hakuna mafanikio wanayopata hivyo amewataka kuendelea kuwa kitu kimoja katika kufikia malengo ya ushindi kwenye uchaguzi ujao .

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Ngome ya wanawake wa Chama hicho Mkunga Hamad Sadala, amesema kwamba wanawake wanathaminiwa sana na chama hicho kwa kuwa ni jeshi kubwa na wameweza kujitoa katika kukiunga mkono chama hicho.

Amewataka wanawake kuwa na mashirikiano hasa viongozi wa ngazi mbali mbali kuanzia matawi, majimbo na wajitahidi kuzitafuta kura kwa ajili ya chama hicho muda utakapowadia.

Akifungua mkutano huo Kaimu Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Chake chake Maalim Saleh Nassor Juma amesema kwamba wananchi wanakila sababu ya kuumga mkono viongozi wa Chama hicho kwa kuwa wanauwezo wa kuipeleka nchi katika maendeleo.

Mwisho

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha Habari leo Jumapili tarehe 28 Julai 2024.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.