Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji hasa kwa sekta binafsi ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo wakati wa kuakhirisha Mkutano wa Tatu(3) wa kuwajengea maarifa wajasiri amali na wafanya biashara katika kutumia Teknolojia na uvumbuzi kwa ajili ya kuchochea mfumo wa ikolojia Zanzibar uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinatu Al Bahari Mbweni Zanzibari.
Amesema Serikali inaendelea kutambua umuhimu wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi na ushirikiano unaoweza kuharakisha ubunifu na maendeleo endelevu nchini sambamba na kutatua changamoto zote zinazojitokeza kwa maslahi mapana ya wawekezaji na wananchi kwa ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais amesema serikali itaendelea kuunga mkono na kuendeleza miundombinu ya Teknolojia ikiwemo kuwekeza katika upatikanaji wa mtandao wa kasi ya juu, kuboresha mitandao ya mawasiliano na kukuza maarifa ya kidijitali ili kuongeza ustawi na kukuza uchumi na kuleta mabadiliko ya biashara.
Aidha Mhe.Hemed amesema Serikali imewekeza kwa kujenga miundombinu ya kutosha ili kuinua uchumi kutoka kipato cha chini, cha kati hadi cha juu itakapofika mwaka 2050 kama ilivyoainishwa katia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwepo mkutano huo utatoa maarifa kwa vijana ambao wanachipukia katika ujasiriamali na Uvumbuzi wa kiteknolojia katika nyanja za kiuchumi na kijamii utakaowawezesha kusimamia biashara zao kwa kutumia mifumo ya kisasa inayotumika duniani kote.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Uchumi na Uwekezaji Mhe. Sharif Ali Sharif amesema Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji itatoa kila aina ya ushirikiano kwa wale wote wenye nia ya kuekeza Zanzibar kwa lengo la kukuza na kunyanyua uchumi nchini.
Mhe. Sharif amewataka washiriki wa Mkutano huo kuitumia vyema taaluma waliyoipata ili wakawe chachu ya madiliko katika sekta ya biashara kwa kutumia Teknolojia na Uvumbuzi katika kukuza biashara zao ndani na nje ya nchi.
Mapema Mkuu wa mradi wa ( UFUNGUO ) kutoka ( UNDP ) Ndugu. JOSEPH MANIRAKIZA amesema kuwa UNDP itaendelea kushirikiana na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika kuwanyanyua wajasiliamali na wafanyabiashara Kwa kufanya biashara zao kwa ubunifu zaidi ili kuweza kufikia malengo waliojiwekea.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR)
No comments:
Post a Comment