Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali zote mbili zinaendela na juhudi mbali mbali za kuimarisha huduma za Afya kwa wananchi wote wa Mijini na Vijini.
Ameyasema hayo kwa Niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la Kumi na Moja(11) la Tanzania Health Summitt (T.H.S) lililofanyika katika Ukumbi wa Zanzibar International Trade Fair Fumba Wilaya ya Magharibi “ B ” Unguja.
Amesema Serikali zinaendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya utoaji wa taarifa ili iweze kusomana kutoka kituo kimoja cha Afya kwenda chengine katika ngazi zote za utowaji wa huduma kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa za wagonjwa ikiwemo vipimo na matibabu sambamba na kutoa fursa ya kupata matibabu zaidi katika maeneo yote ya nchi.
Mhe. Hemed amesema Serikali zote(SMT na SMZ) zinaendelea kuchukua hatua za kuimarisha huduma za kinga, kuwekeza katika miundombinu ya Afya kwa kujenga na kukarabati hospital zote na vituo vya Afya ili ziweze kutoa huduma bora na za kisasa kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Mhe. Hemed amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya na mpango wa Mama Samia wa ufadhili wa ubingwa na ubingwa bobezi imeboresha elimu kwa wataalamu wa afya kwa kutoa kipaombele na kuongeza ufadhili kwa mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi katika taaluma za kimkakati ili kupata wataakamu ambao watasaidia kutoa huduma za kibingwa kwa wanachi.
Makamu wa pili wa Rais amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya hivi karibuni inatarajia kufungua Mtambo mkubwa wa Oxygen katika Hospitali ya Mkoa ya Lumumba utakaotumika kwa Zanzibar nzima ambao utapunguza changamoto mbali mbali ikiwemo ya gharama za ununuzi na usafirishaji wa Oxygen pamoja na kupunguza madhara yaliyokuwa yakijitokeza kwa wagonjwa kwa kukosekana ama kuchelewa kwa huduma hio.
Sambmaba na hayo Makamu wa Pili wa Rais ametoa wito kwa Taasisi za Serikali na Taasisi binafsi pamoja na Mikutano mengine ya Afya nchini kushirikiana na Tanzania Health Summitt ili kuongeza nguvu ya majadiliano katika Sekta ya Afya na kuboresha utowaji wa huduma za Afya kwa wananchi wote wa Tanzania waliopo mijini na vijijini.
Kwa upande wao mawaziri wa Afya kutoka serikali ya SMT na SMZ wamewashukuru viongozi wakuu wanchi kwa kupiga hatua katika kuwekeza kwenye sekta ya Afya kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi ya taifa kwa kuboresha miundombinu ya afya ikiwemo vifaa kinga na tiba, upatikanaji wa dawa usio na mashaka katika bohari kuu na kuekeza katika kuwasomesha madaktari wa nagazi mbali mbali ili kuweza kulisaidia taifa katika utoaji wa huduma bora za Afya.
Aidha wametoa wito kwa sekata binafsi kushirikiana na serikali katika kuimarisha huduma za Afya katika eneo la ubingwa na ubingwa ubobezi ili kuifanya Tanzania kuwa kituo cha utalii wa tiba.
Mapema akitoa Taarifa ya Kitaalamu kwa niaba ya Bodi ya Tanzania Health Summitt Dkt. GRACE MAGEMBE amesema T.H.S imekuwa ni chachu ya kuleta mabadiliko endelevu katika Sekta ya Afya hasa katika kuhamasisha utowaji wa huduma kwa mifumo ya Kidijitali ili kuendana na wakati.
Dkt. Grace amesema Tanzania Health Summitt imewawezesha vijana kupitia program ya Youth Capacity Building kwa kuwapatia mafunzo, kuwaendeleza kitaaluma pamoja na kuwaunganisha watumishi wa Afya na fursa mbali mbali zilizopo nje ya nchi, hivyo amesema kuwa T.H.S ina jukumu kubwa la kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya katika kuboresha na kuimarisha Sekta ya Afya hasa katika eneo la kutoa elimu ya Afya kwa jamii.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametembelea mabanda mbali mbali ya Maonesho ya Watoa huduma za Afya walioshiriki katika Kongamano la Kumi na Moja(11) la Tanzania Health Summitt kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan lililofanyika katika Viwanja vya Ukumbi wa International Trade Fair Fumba Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.
Imetolewa na Kitengo Cha Habari ( OMPR)
No comments:
Post a Comment