
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka wananchi wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kwa wingi katika kuwapigia kura wagombea wote walioteuliwa na Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 27.11.2024.
Ameyasema hayo katika Mkutano wa Hadhara wa kufunga Kampeni kwa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani katika Uwanja wa Standi ya Zamani ya Mabasi Kibaha meli Moja Wilaya ya Kibaha Mjini.
Amesema kila mwanchi ana haki ya kutekeleza takwa la kikatiba la kuchagua kiongozi anaemfaa na kumuamini ambao ni wagombea kutoka chama cha mapinduzi ndio wenye sifa zote za kuwa viongozi wa serikali za mitaa kutokana na sera nzuri na ahadi zinazotekelezeka.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amewaahidi wananchi wa Mkoa wa pwani kuwapa kila aina ya ushirikiano katika uchaguzi huo ili kuhakikisha CCM inaendelea kushinda na kushikilia Dola kutokana na viongozi wake wazuri, sera zinazotekelezeka na utekelezaji wa ahadi wanazoziahidi kwa wananchi.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa Uchaguzi huu wa serikali za mitaa kwa chama cha mapinduzi ni matayarisho ya uchaguzi Mkuu wa Nchi wa mwaka 2025 ambapo Chama cha mapinduzi kimejipanga kupata ushindi mkubwa wa kishindo.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed ametumia hadhara hio kuwaombea kura wagombea wa Chama cha Mapinduzi na kuwataka wanaCCM kuhakikisha kila mmoja katika mtaa wake wanakwenda kukipigia kura Chama cha Mapinduzi kwa kuwachagua wagombea wote waliopitishwa na chama hicho.
Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kibaha Mjini Ndugu MWAJUMA NYAMKE amesema CCM Wilaya ya Kibaha Mjini imejiandaa vizuri katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kufanya kampeni katika Mitaa yote 73 ambayo wagombea wa CCM wamepitishwa na kuhakikisha kuwa wagombea wote watashinda kwa kishindo kikubwa sana.
NYAMKE amesema kuna kila sababu ya CCM kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutokana na kazi kubwa ya kuekeza katika miradi ya maendeleo iliyogusa Sekta zote za Maendeleo hivyo wanaCCM na wananchi wote wana wajibu wa kukipigia kura za ndio Chama cha Mapinduzi.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Mhe. SILVETUS FRANSIS KOKA amesema kuwa viongozi wa Wilaya hio hawana hofu na ushindi wa CCM katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila Mkoa ndani ya Tanzania unapitiwa na miradi ya maendeleo ambapo Kibaha Mjini ni miongoni mwa wanufaika wakubwa na miradi hio ya maendeleo iliyogusa Sekta zote za Maendeleo.
KOKA amesema Jimbo la Kibaha Mjini limeongeza wanachama wapya wengi waliojiunga na CCM wakiwemo waliotoka vyama vya upinzani jambo linalotoa Taswira ya ushindi wa kishindo kwa chama cha Mapinduzi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika November 27, 2024.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe.. 26 / 11 / 2024.
No comments:
Post a Comment