Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis
Hamza Khamis amesema Serikali imesajili miradi 63 ya biashara ya kaboni kupitia
sekta mbalimbali.
Mhe. Khamis ameliarifu Bunge jijini Dodoma leo Novemba 06, 2024 wakati
akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Amani Mhe. Abdul Yussuf Maalim aliyetaka
kujua Serikali ina mpango gani wa kuongeza wigo wa biashara ya kaboni ili
kupunguza uharibifu wa ukataji wa misitu nchini.
Akiendelea kujibu swali hilo Naibu Waziri Khamis ametaja sekta zilizo
katika miradi iliyosajiliwa ni pamoja na Kilimo (asilimia 8), Nishati (asilimia
33), Misitu (asilimia51), Mifugo (asilimia 5) na Usimamizi wa taka (asilimia 3).
Amesema kati ya miradi iliyosajiliwa kupitia Sekta ya Misitu ni minne
inahusisha shughuli za upandaji miti, miradi 20 ni kwa ajili ya kupunguza
uharibifu na upotevu wa misitu na miradi mitano ni kwa ajili ya kurejesha uoto
wa asili.
Aidha, Mhe. Khamis ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa
Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024 – 2034) ambao unahamasisha matumizi ya nishati
safi za kupikia ikiwemo gesi asilia, nishati jadidifu, mkaa mbadala na umeme
ambazo zinaweza kuchangia katika Biashara ya Kaboni na kupunguza matumizi ya
kuni na ukataji wa misitu.
Halikadhalika, amesema Serikali imeandaa na inatekeleza Sera ya Taifa ya
Uchumi wa Buluu 2024 na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa
Buluu (2024 – 2034).
“Mheshimiwa Mwenyekiti katika Sera hii ya Taifa ya Uchumi wa Buluu tumeweka
mikakati ya kuhamasisha matumizi ya hati fungani za buluu na biashara ya kaboni
katika shughuli za rasilimali za Uchumi wa Buluu kwa lengo la kuongeza wigo wa
biashara ya kaboni nchini ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira,“ amesema.
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali inachukua mipango
madhubuti kuhakikisha misitu inakuwa sehemu ya mapato kupitia biashara ya
kaboni katika vijiji, shehia na wilaya kwa kuwashirikisha wananchi katika kuihifadhi.
Akijibu maswali la nyongeza la Mhe. Maalim kuhusu hatua Serikali inachukua
katika kuitunza misitu na Zanzibar imenufaikaje na biashara ya kaboni, Mhe.
Khamis ameeleza kuwa
Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imeanza kutoa elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo wabunge kuhusu fursa
zinazopatikana katika biashara ya kaboni kwa upande wa Zanzibar pamoja na
kuwaunga mkono katika kuandaa kanuni za biashara ya kaboni.
No comments:
Post a Comment