Habari za Punde

SMZ KUWAFIDIA NYUMBA BORA WANANCHI WATAKAOPISHA MIRADI YA MAENDELEO: DK MWINYI

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa Mauzo ya Nyumba za Chumbuni za Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) hafla hiyo ya uzinduzi iliyofanyika katika Ukumbi wa Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar.

RAIS  wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa  Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  amesema kuanzia sasa Serikali  itawafidia nyumba bora wananchi wanaotoa maeneo yao kupisha miradi ya maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi amefahamisha  kuwa Serikali imedhamiria  na jukumu la msingi la kuhakikisha  wananchi wanapata makaazi bora ya kuishi.

Ameeleza kuwa  kumekuwa na baadhi ya wananchi wanazoendelea kujenga nyumba zisizo na ubora (Vibanda) licha ya kufidiwa fedha za kutosha na Serikali.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo, alipozindua Mradi wa mauzo wa Nyumba za Chumbuni zinazojengwa na  Shirika la Nyumba, Zanzibar  Ukumbi wa Mikutano Hoteil ya Amani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Rais Dk. Mwinyi  amefahamisha kuwa jitihada hizo zimekuwa endelevu kwa awamu tofauti  zilizoanza  baada ya Mapinduzi ya Januari 1964  Chini ya Uongozi wa Hayati Abeid Aman Karume.

Dk. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea  kutafuta fedha zaidi za kuuendeleza Miradi mikubwa ya Ujenzi wa Nyumba za Maakazi maeneo mbalimbali.

Aidha Rais Dk. Mwinyi amezisitiza taasisi za kifedha ziliopo  kufanya kazi kwa ukaribu na Shirika la  nyumba la Zanzibar ili kufanikisha azma hiyo.

 Amefahamisha kuwa  Ujenzi wa Nyumba Bora za Makaazi  unaenda Sambamba na  Uimarishaji  wa Miji Bora  na  Barabara zitakazotoa taswira  nzuri ya Nchi.

Halikadhalika, Rais Dk. Mwinyi ametoa rai kwa Wananchi kuhamasika kununua nyumba hizo ili kuwa na Makaazi bora na ya kisasa.

Hata hivyo, Dk. Mwinyi amelisisitiza Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC)kuendelea kutafuta Soko la Nyumba zinazojengwa kwani ni wajibu  pamoja na kuwa na Nyumba nyengine za kuwakodisha wananchi.

Rais Dk ,Mwinyi amefahamisha kuwa ni vyema kwa wananchi kununua nyumba hizo hivi sasa kwa  maeneo yanayojengwa  yatakuwa na biashara nyingi baadae Pamoja na shughuli za kijamii na  barabara za uhakika. 

Ameishauri taasisi kutoka  Sekta Binafsi kushirikiana na Shirika la Nyumba ili lipate mafanikio zaidi.

Rais Dk. Mwinyi pia ameipongeza taasisi ya Infinity Group of Companies  kwa wazo la kuwekeza Zanzibar  na  mpango wao wa kuwajengea uwezo Vijana wa Zanzibar kwenda kujifunza nchini Dubai  ili kuleta uzoefu huo Zanzibar. 

Rais Dk Mwinyi ameeleza kufarijika  na kasi ya Utendaji wa Shirika la Nyumba hivi sasa kwani limekuwa likitekeleza Miradi yenye tija badala ya  kushughulikia Migogoro ya Nyumba kwa Muda mrefu.

Pia, ametumia fursa hiyo kuwahimiza Watendaji wa Sekta ya Umma wanaokabidhiwa Majukumu kuhakikisha Wanaacha Alama   katika maeneo yao ya kazi yatakayowajengea heshima wakati wote.

Akitoa Taarifa ya Kitaalamu ya Mradi huo  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzbar, Sultan Said ameeleza kuwa Mradi huo ni Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025 ya kuimarisha nyumba za Makaazi .

Ameeleza Mradi wa Chumbuni Utakuwa na Nyumba 3000 na Shirika linakusudia kuuendeleza Miradi mikubwa ya Kimkakati ya Ujenzi wa Nyuma maeneo ya Kikwajuni, Kwa Mchina Unguja, Kisakasaka na Mabaoni Mfikiwa Pemba.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Rahma Kassim Ali  ameleza kuwa kuanzishwa Idara ya Maendeleo ya Makaazi  kutaleta chachu ya utekelezaji wa  Sera ya Makaazi itakayoleta Mafanikio makubwa  hapo baadae.

Amebainisha kuwa Wizara bado ina maeneo mengi  yaliotengwa kwa ajili ya Maendeleo ya Makaazi  ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuwa na Miji Bora.

IDARA YA MAWASILIANO IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.