Habari za Punde

Tanzania Yashinda: World’s Leading Safari Destination/ Sisi Sasa Ndio Eneo Maridhawa Zaidi Kwa Utalii wa Safari Duniani.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi (wa pili kulia) na Rais wa World Travel Awards Bw. Graham E. Cooke (wa pili kushoto) mara baada ya kukabidhiwa Tuzo ya Kivutio Bora Zaidi Duniani kwa Utalii wa Safari 2024 katika hafla hiyo iliyofanyika usiku wa Novemba 24, 2024 katika Kisiwa cha Madeira, Ureno.

Na Mwandishi Wetu- Madeira, Ureno.

Hatimaye baada ya mchuano mkali Tanzania imeibuka kuwa eneo linaloongoza zaidi duniani kwa utalii wa safari (hasa za kuona wanyama wa porini) ikiyashinda mataifa mbalimbali duniani ikiwemo nchi za Afrika, hii ni kwa mujibu wa Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards) zilizotolewa usiku wa kuamkia leo yaani jana Novemba 24, 2024 kisiwani Madeira, Ureno.

Zikitambulika kuwa sawa na “Tuzo za Oscars”  katika tasnia ya utalii, World Travel Awards (WTA), ndio tuzo za juu zaidi duniani na tangu mwaka 1993, zimekuwa zikitambua mafanikio na umahiri katika ngazi ya mabara na kidunia katika kategoria anuai za utalii.

Tunawashukuru wote waliotupigia kura kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwemo wadau wa utalii na uhifadhi wenye hadhi ya kupiga kura lakini na mtu mmoja mmoja walioichagua Tanzania.

Tuzo hii ni ushahidi wa matokeo ya uhifadhi wetu mkubwa uliofanywa na viongozi wa awamu zote na unaoendelezwa katika Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini pia na uwekezaji mkubwa tunaoendelea nao katika kutangaza utalii kwani wengi walioipigia kura Tanzania maana yake ni wazi walitembelea na kuridhika na umaridhawa na uasili wa hifadhi zetu,” alisema Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, aliyeongoza msafara kupokea Tuzo hiyo hapa Madeira.

Awali mwezi Oktoba mwaka huu, Tanzania ilishinda Tuzo nne za WTA katika ngazi ya Bara la Afrika ikiwemo ile ya “Africa’s Leading Destination.”

Awali katika Tuzo hizo kampuni binafsi inayofanya kazi Tanzania katika Hifadhi za Serengeti na Ruaha ya Serengeti Balloon Safaris nayo imeshinda Tuzo ya kuwa Kampuni Bora ya Baluni Duniani.

Baadhi ya nchi nyingine zilizoshinda ni Visiwa vya Saint Lucia (Honeymoon Destination), ugiriki (Athens, Leading City Destination), Ureno (World Leading Beach Destination), Ufaransa (Leading Events Destination), Peru (Cultural and Culinary Destination), Ureno (Praga, Emerging Tourism Destination),     Hispania (Madrid, World Leading Meeting Destination) na Maldives (World Leading Destination).

Kwa mafanikio hayo Rais wa WTA Bw. Graham  Cooke pia 

ameitangaza Tanzania kuwa mwenyeji wa Tuzo za Utalii   
Duniani Kanda ya Afrika 

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi (wa pili kushoto) akimkabidhi zawadi kutoka Tanzania Rais wa Kisiwa cha Madeira, Mhe. Miguel Albuquerque (Katikati) mara baada ya Hafla ya Utoaji Tuzo ya World Travel Awards ambapo Tanzania imeshinda kuwa Kivutio Bora Zaidi Duniani Cha Utalii wa Safari 2024 katika hafla iliyofanyika usiku wa Novemba 24, 2024 katika Kisiwa cha Madeira, Ureno. Wengine pichani ni Watendaji kutoka Bodi ya Utalii Tanzania na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi akiwa kwenye picha ya pamoja na washindi waliopata Tuzo kwenye Hafla ya Utoaji Tuzo ya World Travel Awards iliyofanyika katika Kisiwa cha Madeira, Ureno usiku wa  Novemba 24, 2024.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi (katikati) na ujumbe kutoka Tanzania wakipokea Tuzo kutoka World Travel Awards baada ya Tanzania kushinda kuwa Kivutio Bora Zaidi Duniani Kwa Utalii wa Safari 2024 katika hafla iliyofanyika usiku wa Novemba 24, 2024 katika Kisiwa cha Madeira, Ureno.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.