RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Mamlaka ya Mji Mkongwe kuifunika mitaro yote iliyowazi kwenye
mji huo ili kuepusha maradhi na ajali kwa wananchi na wageni wanaoutembelea mji
huo.
Dk. Mwinyi amesema hayo kwenye
kilele cha maadhimisho ya siku ya Mji Mkongwe wa Zanzibar yaliyofanyika katika
viwanja vya bustani ya Forodhani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amefahamisha kuwa kuwepo wazi
kwa mitaro hiyo hakutoi haiba na taaswira njema ya Mji Mkongwe na kushusha
hadhi ya kuwa mji wa urithi wa dunia unaotambulika na Shirika la Kimataifa la
Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Ameeleza Serikali imetenga jumla ya shilingi Bilioni 9 kwa ajili
ya kufanya ukarabati mkubwa wa majengo yaliyo katika hali mbaya zaidi ndani ya Mji Mkongwe ambayo wananchi
hawamudu gharama za kukarabati.
Pia Rais Dk. Mwinyi amesema, Serikali ipo katika hatua za
kukamilisha upembuzi yakinifu wa Mradi wa kupitisha chini ya ardhi miundombinu
yote ya umeme, mawasilano na maji katika Mji Mkongwe ili kurejesha haiba ya
taswira ya majengo hayo kupitia mradi wa BIG Z wa Benki ya Dunia na kukamilisha matayarisho ya mageuzi makubwa ya miundombinu ya barabara na
maeneo ya wazi kwa lengo la kuboresha hadhi ya Mji huo muhimu kwa maendeleo ya
Zanzibar hasa kwa sekta ya utalii.
Amesema Mji Mkonge hautoweza kubakia hai endapo
hautofanyiwa matenegenezo makubwa yanayohitaji nguvu ya kila mmoja ikiwemo
wakaazi wa mji huo, taasisi za umma na binafsi kwa kuhakikisha kila mmoja
anatoa mchango wake katika kuutunza, kuuhifadhi na kuuendeleza mji huo.
Amewahakikishia wakaazi wa Mji Mkongwe kuwa Serikali
itaendelea kushirikiana na wadau, taasisi za ndani na kimataifa ili kuhakikisha
Mji Mkongwe unaimarika na kubaki kuwa kioo cha maendeleo na utalii wa Zanzibar
kwa maslahi vizazi vya sasa na baadae.
Rais Dk. Mwinyi ametumia maadhimisho hayo kuishukuru
Serikali ya Oman kwa kuungamkono kwa hali na mali juhudi za Zanzibar za
kuuhifadhi Mji Mkongwe na maeneo mengine ya kihistoria yaliopo Zanzibar kwani
msaada huo umechangia kuyaweka maeneo hayo kuwa endelevu wakati wote.
Ameiomba Serikali ya Oman kuendelea kuwajengea uwezo
watendaji na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe kwa kuwapatia mafunzo
mbalimbali ikiwemo ujuzi ambao umewaongzea weledi wanaoutumia katika
kuuendeleza Mji huo.
Aidha, Dk. Mwinyi amezipongeza Kampuni za INFINIX, Maxbit
na Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango
mkubwa wanaoutoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Mamlaka ya Mji
Mkongwe.
Rais Dk. Mwinyi amesifu hatua ya Mamlaka ya Mji Mkongwe
kwa kuanzisha Mfumo wa kiditali aliouzindua katika kilele cha siku hiyo kwa
uendeshaji wa mamkala hiyo na usimamizi wa uingiaji wa watalii hatua
itakayochangia kuongoza mapato ya Serikali na utoasi wa taarifa sahihi za Mji
Mkongwe.
Ameeleza kufarajika kwake kwa kushirikishwa wajasiriamali
wadogo katika maadhimisho ya mwaka huu na kutoa agizo kwa Mamlaka ya Mji
Mkongwe kuwaongezea muda wa kufanya biashara zao na kuwapangia utaratibu
maaluumu wa kufanya biashara hizo kama walivyoomba wajasiriamali hao ili
kuwaongezea tija.
Awali maadhimisho hayo yaliambatana na shughuli
mbalimbali zikiwemo uzinduzi wa upakaji wa rangi bure kwa majengo yote ya Mji Mkongwe kwa
zaidi ya nyumba 2,700 ziliomo katika mji huo uliofanywa na Rais Dk. Mwinyi,
mradi unaoendeshwa na Kampuni ya INFINIX pia kutembelea makumbusho ya Makaburi
ya wafalme walioitawala Zanzibar yaliopo pembezoni mwa nyumba ya wananchi, (People’s
Palace) iliyopo Forodhani na kusimuliwa historia ya makaburi hayo, kutembelea mabanda
ya wajasiriamali wa kazi za Utalii na kushuhudia mashindano maalumu ya makachu
yaliyofanywa na vijana wa Mji Mkongwe yaliyoshuhudiwa na mamia ya wananchi wa
Zanzibar na wagemi wa mataifa mbalimbali.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudriki
Ramadhan Suraga, amesema mabadiliko chanya uongozi wa Serikali ya awamu
ya nane yameleta mabadiliko makubwa kwa Mji Mkongwe na kuuongezea umaarufu
zaidi kimataifa.
Naye, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Mji Mkongwe, Mhandisi
Ali Said Bakari, ameishukuru Serikali ya Oman kwa msaada wa Dola za Kimarekani
milioni 25 kwa ukarabati wa jengo la Beit el Ajaab ambalo lina uhumimu kwa
historia na Utalii wa Zanzibar.
Wakiwasilisha salamu za wadau na wananchi wa
Mji huo, wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwaondoshea tozo za
Maegesho, katika mji huo waliozilalamikia kama ni mzigo kwao.
Akitoa salamu za UNESCO, Mwakilishi wa Shirika
hilo kwa Tanzania, Michel Toto ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea
kuulinda, kutunza na kuuendeleza Mji Mkongwe na kubaki kuwa ni Urithi na hifadhi
ya dunia na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao na Serikali.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa
Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Hamisi Masanja Malebo, amesema Mji Mkongwe wa
Zanzibar unatofautiana na mengine duniani kutokana na sifa ya kuwa Mji wa
zamani uliohai kwa kuwa na watu wanaoishi na kufanya shughuli zao za uchumi
jamii na Utalii ambapo hakuna mji kama huo duniani hasa kwa ukanda wa pwani ya Afrika
Mashariki.
Maadhimisho hayo ya siku ya Mji
mkongwe yamebeba kauli mbiu inayosema “Dk. Mwinyi ni nuru ya Mji Mkongwe” yaliasisiwa rasmi tarehe 28 Disemba mwaka
2020 na yamekua yakiadhimishwa kila mwaka.
IDARA YA
MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment