Habari za Punde

Diaspora Ubelgiji Wampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa Miradi ya Maendeleo na Kudumisha Amani

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na Watanzania waishio Ubelgiji uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji.

Watanzania wanaoishi nchini Ubelgiji wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti unaoendelea kuleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.

Pongezi hizo zilitolewa wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, na Watanzania waishio Ubelgiji na Luxembourg, uliofanyika katika makazi ya Balozi wa Tanzania jijini Brussels, Ubelgiji.

Akizungumza kwa niaba ya diaspora hao, Bw. Riziki Thomas – Mwenyekiti wa Watanzania waishio Ubelgiji, na Bw. Mrisha Sarazya – Mwenyekiti wa Watanzania waishio Luxembourg, walieleza kuwa diaspora inaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa inayosimamiwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia.

“Mhe. Waziri, leo tumejitokeza kwa wingi sio tu kukuona, bali kuwasilisha shukrani zetu kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya. Tukiwa nje ya nchi bado tunaona jitihada zake – kama vile kukamilika kwa reli ya kisasa, mradi mkubwa wa kufua umeme kupitia Bwawa la Julius Nyerere – yote haya yanatupa heshima kubwa kama Watanzania na faraja kuona taifa linapiga hatua,” alisema Bw. Thomas.

Kwa upande wake, Bw. Mrisha aliongeza kuwa diaspora inatambua na kuthamini jitihada hizo na itaendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo nchini, ikiwemo kushiriki katika biashara na uwekezaji, kulipa kodi, na kusaidia kuongeza ajira nchini.

Akihutubia diaspora hiyo, Mhe. Balozi Kombo aliwashukuru kwa mwitikio wao mkubwa na kwa kuonesha mshikamano na uzalendo kwa kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla.

Aidha, aliwataka Watanzania hao kujisajili kwenye mfumo wa Digital Diaspora Hub, ili kuwezesha Serikali kukamilisha mchakato wa utoaji wa hadhi maalumu kwa diaspora pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi.

Waziri Kombo yupo nchini Ubelgiji kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Aprili 14, 2025, ambapo pamoja na kukutana na diaspora, atakuwa na mazungumzo ya kikazi na viongozi mbalimbali wa Umoja wa Ulaya na taasisi za kifedha kuhusu masuala ya ushirikiano na maendeleo.

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestus Nyamanga akizungumza na Watanzania waishio Ubelgiji uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji.

Sehemu ya Watanzania waishio Ubelgiji wakifuatilia mkutano.
 Mwenyekiti wa Watanzania waishio mjini Luxembourg Bw. Mrisha Sarazya akizungumza kwenye mkutano wa Watanzania waishio Ubelgiji na Waziri Kombo uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji.
Sehemu ya Watanzania waishio Ubelgiji wakifuatilia mkutano.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania waishio Ubelgiji, baada ya kumaliza mkutano wake uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji. 
 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akiwa katika picha ya pamoja na Watanzania waishio Ubelgiji, baada ya kumaliza mkutano wake uliofanyika jijini Brussels, Ubelgiji. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.