Rais Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Chakula Barani Afrika akiwatambulisha Profesa Mary Abukutsa-Onyango kutoka Kenya (kulia) na Mercy Diebiru-Ojo kutoka Nigeria ambao ni washindi wa Tuzo ya Chakula Barani Afrika kwa mwaka 2025 (Africa Food Prize 2025) kwenye hafla iliyofanyika mjini Dakar, Senegal, pembezoni mwa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AFSF) linaloendelea kuanzia tarehe 1 hadi 5 Septemba 2025.
Rais Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Chakula Barani Afrika kwenye hafla ya kutoa tuzop ya Chakula Barani Afrika kwa mwaka 2025 mjini Dakar, Senegal, pembezoni mwa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AFSF) linaloendelea kuanzia tarehe 1 hadi 5 Septemba 2025.
Wanasayansi
wanawake wawili – Profesa Mary Abukutsa-Onyango kutoka Kenya na Mercy
Diebiru-Ojo kutoka Nigeria – wametangazwa washindi wa Tuzo ya Chakula Barani
Afrika kwa mwaka 2025 (Africa Food Prize 2025).
Tuzo hiyo,
yenye thamani ya Dola za Marekani 100,000, ilikabidhiwa na Rais Mstaafu wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Tuzo ya Chakula Barani Afrika.
Hafla ya
kukabidhi tuzo ilifanyika mjini Dakar, Senegal, pembezoni mwa Jukwaa la Mifumo
ya Chakula Afrika (AFSF) linaloendelea kuanzia tarehe 1 hadi 5 Septemba 2025.
Katika hotuba
yake, Dkt. Kikwete aliwapongeza washindi kwa mchango wao wa kipekee katika
tafiti zinazolenga kuongeza tija ya uzalishaji na kuboresha maisha ya wakulima
wadogo barani Afrika.
“Tuzo hii
inadhihirisha nafasi kubwa ya wanasayansi wa Afrika katika kutafuta suluhu za
changamoto za kilimo. Ingawa mwaka huu imeenda kwa washindi wawili, tunatambua
kazi kubwa inayoendelea kufanywa na watu binafsi na taasisi nyingi ili
kuhakikisha bara letu linakuwa na mifumo imara na endelevu ya chakula,” alisema
Dkt. Kikwete.
Profesa
Abukutsa-Onyango amejikita katika tafiti za mboga mboga za asili za Kiafrika
kama mchicha, sukuma wiki, mgagani, mchunga, figiri na kisamvu, akihamasisha
uzalishaji na ulaji wake kwa madhumuni ya kuimarisha lishe.
Kwa upande
wake, Mercy Diebiru-Ojo anasifika kwa kubuni na kuendeleza teknolojia ya kisasa
ya uzalishaji na upandikizaji wa mbegu za mihogo kwa kutumia mbinu ya semi-autotrophic
hydroponic technology, ambayo imeongeza mavuno na tija katika kilimo hicho
muhimu barani Afrika.
Tuzo ya Chakula
Barani Afrika ilianzishwa mwaka 2005 chini ya mwamvuli wa mpango wa Mageuzi ya
Kijani Afrika (AGRA). Inatolewa kila mwaka kwa watu binafsi au taasisi
zinazotoa mchango wa kipekee katika kuimarisha mifumo ya chakula na maendeleo
ya sekta ya kilimo.
Kwa mwaka huu
2025, jumla ya maombi 601 kutoka ndani na nje ya Afrika yaliwasilishwa kuwania
heshima hii kubwa.
No comments:
Post a Comment