Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Awasili Nchini Malawi Kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Katika Uapisho wa Rais Mteule wa Malawi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea heshima kutoka Jeshi la Malawi  alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chileka  nchini Malawi  ambako alimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwenye uapisho wa Rais Mteule wa Malawi  Profesa Arthur Peter Mutharika kwenye uwanja wa Kamuzu Blantyre, Malawi Oktoba 4, 2025. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi, Balozi Dkt. Mwayiwawo Polepole alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chileka  nchini Malawi  ambako alimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye uapisho wa  wa Rais Mteule wa Malawi Profesa Arthur Peter Mutharika kwenye uwanja wa Kamuzu Blantyre, Malawi Oktoba 4, 2025.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mheshimiwa Agnes Kayola  alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa  Kimataifa wa Chileka nchini Malawi  ambako alimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye uapisho wa Rais Mteule wa Malawi  Profesa Arthur Peter Mutharika kwenye uwanja wa Kamuzu Blantyre, Malawi Oktoba 4, 2025.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Oktoba 04, 2025 amemwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye uapisho wa Rais Mteule wa Malawi, Peter Mutharika uliofanyika katika uwanja wa Kamuzu, Blantyre nchini humo.

Mheshimiwa Rais Mutharika wa Chama cha Democratic Progressive (DPP) alimshinda mpinzani wake Rais Mstaafu Lazarus Chakwera wa The Malawi Congress Party (MCP) kwa asilimia 56.8.

Mutharika aliwahi kuwa Rais wa nchi hiyo kati ya mwaka 2014 hadi 2020 alipoangushwa na Mheshimiwa Chakwera, hivyo Mheshimiwa Rais Mutharika anarudi tena katika kiti hicho cha Urais baada ya miaka mitano.

Akizungumza baada ya kuapishwa Mheshimiwa Rais Mutharika amesema nchi ya Malawi ni kwa ajili ya Wamalawi wote, hivyo amewataka viongozi wajitokeze na washirikiane katika kuwatumikia watu na si matumbo yao, watoto wao au marafiki zao.

“Sote tunahitaji mabadiliko na ninawaahidi mabadiliko na kama nchi hii tunataka kuibadilisha ni lazima yatoke kwetu sisi Wamalawi. Ameongeza kuwa Serikali yake itahakikisha wananchi wanahudumiwa katika nyanja zote za kimaendeleo na kwa pamoja tutaijenga Malawi.”

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,                    

JUMAMOSI, OKTOBA 4, 2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.