Habari za Punde

AFYA YAUFIKIA MPANGO WA MKUZA

Na Fatma Kassim Maelezo

WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii Sultan Mohammed Mughery amesema kuwa sekta ya Afya nchini inaimarika kutokana na jitihada za Serikali na washirika wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi.

Alisema kutokana na jitihada hizo huduma mbali mbali zimekuwa zikitolewa kwa ufanisi hasa kuwepo kwa vifaa vya kisasa pamoja na wataalamu wa kukabiliana na maradhi mbali mbali yakiwemo maradhi sugu yanayosumbua jamii.

Waziri Mugheir alieleza hayo katika hoteli ya Zanzibar Ocean View, alipofungua mkutano wa tano wa mwaka wa kutathmini sekta ya afya, kwa washirika wa maendeleo na wadau wa ndani na nje ya nchi wanaoisaidia sekta ya afya.

Alisema mwaka 2010 Wizara ya Afya imekamilisha malengo muhimu iliyojiwekea ya kuufikia mpango mkuu wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini Zanzibar (MKUZA), ikiwemo kuimarisha Chuo cha Taaluma za Sayansi pamoja na utekelezaji wa mpango wa mabadiliko ya sekta ya afya ili kukabiliana na maradhi makubwa yanayowasumbua wananchi wa Visiwa vya Unguja na Pemba.

Aidha Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, inaendelea kuimarisha madarasa ya Madaktari wazalendo kwa Unguja na Pemba ili kukabiliana na upungufu wa wataalamu katika hospitali.

Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa sekta ya Afya kwa mwaka uliopita Mkurugenzi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Malick Abdalla Juma alisema kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo Wizara imefanikiwa kutekeleza mambo muhimu katika sekta ya afya.

Aliyataja miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuwapatia taaluma wafanyakazi wake wa kada mbali mbali ili kukabiliana vyema na mapambano ya maradhi yakiwemo ya akinamama wajawazito na watoto wachanga ambayo ni tatizo kubwa kwa jamii.

Aidha aliyashukuru mashirika mbali mbali ya ndani na nje ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia sekta ya afya katika mambo mbali ikiwemo elimu, upatikanaji dawa , vifaa vya kisasa na elimu ya afya kwa jamii kuanzia ngazi ya taifa hadi Shehia.

Nao washiriki wa mkutano huo wamesema kuwa elimu zaidi itolewe ili jamii ielewe kuwa uimarishaji wa sekta ya afya sio jukumu la Serikali pekee kwani linamgusa kila mtu.

Mkutano huo umewashirikisha wadau mbali mbali yakiwemo mashirika ya kimataifa ya DANIDA, WHO, UNICEF, UNFPA ambapo umebeba ujumbe wa ‘tuliyojifunza kutokana na miaka iliyopita na mikakati kwa miaka ijayo’.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.