Habari za Punde

HOTUBA YA EIDUL FITR YA RAIS KARUME LEO

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,

MHE. AL-HAJJ DK. AMANI ABEID KARUME,

KATIKA BARAZA LA EIDUL EL FITR

SEPTEMBA 2010, MFUNGO MOSI 1431 A.H.



BISMILLAHI RAHMANI RAHIM


Awali ya yote, ni wajibu wetu kumshukuru Mwenyezi Mungu aliekamilika kwa sifa zake, ambae ndie Muumba wa Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo ndani yake; kwa Uwezo wake tumebahatika kukutana hapa kwa siku ya leo na tumshukuru kwa hili (Al-hamdulillah).



Mheshimiwa Naibu Mufti Mkuu,

Mheshimiwa Naibu Kadhi Mkuu,

Mheshimiwa Waziri Kiongozi,

Mheshimiwa Naibu Waziri Kiongozi,

Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi,

Mheshimiwa Jaji Mkuu,

Waheshimiwa Mawaziri,

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,

Waheshimiwa Mabalozi,

Ndugu Wananchi,

Mabibi na Mabwana




ASSALAM ALEYKUM WA RAHMATULLAH WABARAKATUH


Nimetanguliza kumshukuru na kumsifu Mola aliyetuumba na kutupa uhai, Yeye Ndiye Mwenye kustahiki sifa na unyenyekevu kutoka kwetu sote. Salamu na Rehma zimfikie Mtume wetu Sayidina Muhammad (S.A.W) aliyeletwa kuwa ni Rehma kwa walimwengu. Aidha, nawaombea maghfira na Rehma za Mwenyezi Mungu wazazi, ndugu, sahiba, marafiki na wenzetu wote waliotutangulia mbele ya Haki. Mwenyezi Mungu awasamehe makosa yao na awaweke pahala pema peponi – Amin.


Ndugu Wananchi,

Tumemaliza ibada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa salama na amani. Baada ya kutekeleza ibada hiyo adhimu ya kufunga, Mwenyezi Mungu kwa ukarimu na rehma zake kwetu ametujaalia sikukuu ya Idd el Fitri, ikiwa ni moja katika sikukuu mbili adhimu (Idd el Fitr na Idd el Hajj). Leo tunasherehekea sikukuu ya Idd el Fitr.


Ndugu Wananchi,

Naomba nichukue nafasi hii kutoa pongezi kwa waumini wote ambao wametekeleza ibada ya kufunga Ramadhani na suna mbali mbali zilizoambatana pamoja na ibada hiyo, kama sala za Tarawehe, Tahajudi na Witri; kuzidisha kusoma Quran na kutoa zaka na sadaka kwa wingi. Ni jambo la kujivunia kwamba utekelezaji wa ibada hiyo kwa mwaka huu, umepambika kwa utulivu wa aina yake. Nyoyo za imani, upendo, heshima na mshikamano zilidhihirika katika kila sehemu ya nchi yetu. Hali hiyo imechangia kukuza amani na usalama. Mwenyezi Mungu kwa utukufu na uwezo wake alitujaalia hali ya hewa nzuri ya kuburudisha mwezi wote wa Ramadhani hata kuwavutia wageni kutoka nje kuja kufunga na sisi. Pia, tulijaaliwa neema ya vyakula vya aina mbali mbali. Natoa shukurani za dhati kwa wakulima wote kwa jitihada zao za kuzidisha ukulima wa kitaalamu na kupata mavuno mazuri, hali iliyopelekea kupatikana vyakula vya futari tulivovizowea kwa wingi, kwa mfano ndizi, viazi, maboga, mihogo na majimbi pamoja na matunda ya aina zote.


Ndugu Wananchi,

Hatuna budi kuzidi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake, kwani Yeye Mwenyewe, kwa mapenzi yake ametuelimisha waja wake katika Aya ya Saba ya Suratul Ibrahim: kwa kusema:-


Kama Mkinishukuru Nitakuzidishieni (yaani yaliyo mazuri zaidi).


Ndugu Wananchi,

Wazee wamesema nyota njema huonekana alfajiri. Msemo huo umedhihirika nchini kwetu kwa vitendo tokea kumalizika mizozo na ushabiki wa kisiasa uliopelekea malumbano yasiyo na msingi hasa kwa wakati wa sasa. Baada ya kupatikana maridhiano baina yetu, wananchi wameitikia wito wa umoja na mshikamano. Umoja umejidhihirisha zaidi kwa kura ya maoni ambayo wananchi walio wengi zaidi wameridhia mfumo mpya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar utakaokua na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa faida ya wananchi wake na maendeleo ya nchi yao ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla.


Leo tumekamilisha mwezi mtukufu wa Ramadhani na tumo katika furaha ya sikukuu ya Idd el Fitr ambapo imetangulia kuwepo mikusanyiko mikubwa mikubwa katika sala za pamoja kama ilivyokua asubuhi katika sala ya Idd el Fitr. Hakika mshikamano na ushirikiano wenye nia safi ni katika miongozo ya Mola wetu.


Mwenyezi Mungu katika kusisitiza hayo amesema katika Suratul Maida Aya ya pili:

“Na saidianeni (shikamaneni) katika wema na uchamungu, na wala msisaidiane (msishikamane) katika dhambi na uadui”.


Kwa uzito wa Aya hii mimi binafsi nimepata nguvu ya kuuona umuhimu wa kuendeleza umoja na mshikamano wetu wa Wazanzibari.


Ndugu Wananchi,

Idd ni siku adhimu yenye furaha na tuna wajibu wa kusherehekea kwa pamoja na kukuza furaha hiyo. Katika kufanya hivyo tuwe watu wenye kuwajali wenzetu ambao wana upungufu wa mahitaji na watoto yatima na kuwafanya na wao kufurahika. Kwa hekima yake, Mola wetu ametupa agizo la kutoa Zakatul-Fitr ambayo tunatakiwa tuwe tumeshamaliza kuitoa kabla ya sala ya Idd, natumai wengi wetu tumewahi kutoa Zakatul-Fitr kwa wakati. Lakini kwa wale ambao hawajatoa basi mlango wa kutoa sadaka upo wazi. Wakati huu wa sikukuu ndio unaofaa hasa kwa waislam wote wenye uwezo kutoa kwa moyo mkunjufu zaka kwa wakati na sadaka zetu kuwapa wale wasiokua na uwezo. Aidha, tuwakumbuke wagonjwa waliopo hospitalini au majumbani kwa kuwatembelea na kuwapa sikukuu yao ili na wao wapate faraja.


Kwa wafanyabiashara nawaomba wazidi kuwa na huruma kwa wanunuzi wao kwa kuweka bei nafuu kwa bidhaa mbali mbali hasa nguo, vyakula nakadhalika. Huruma yao hiyo ni miongoni mwa sadaka yao hususan wakati huu wa sikukuu.


Ndugu Wananchi,

Nchi yetu, katika kipindi hiki, imo katika harakati za siasa ikiwa tunaelekea Uchaguzi Mkuu, tarehe 31 Oktoba mwaka huu. Hiki ni kipindi cha kampeni za vyama vya siasa kama uchaguzi unavyohitaji. Wito wangu kwa wananchi wote ni kuzidisha hali ya utulivu kwa kuzingatia hali ya maridhiano yaliyotuletea umoja na mshikamano.


Tukiwa katika mchakato na harakati za uchaguzi tukumbuke kuwa hayo ni mambo ya mpito. Baada ya siku chache tutabaki na hali ya kawaida, kwa hivyo, ni muhimu tuendeshe kampeni na mchakato wote wa uchaguzi kwa njia ya kuheshimiana, umoja, amani na utulivu nchini kote. Siasa si ugomvi bali ni sehemu tu ya kutekeleza mahitaji ya watu katika jamii. Baada ya hapo tutaendelea na shughuli zetu za maendeleo kama kawaida. Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa mshikamano wetu hautetereki.


Ndugu Wananchi,

Mshikamano wetu, bidii yetu na umoja wetu umeleta mafanikio nchini mwetu kisiasa, kiuchumi na ustawi wa jamii katika kipindi cha Awamu ya Sita ya Serikali ya Mapinduzi. Maendeleo yaliyo wazi yanaonekana katika nyanja za kilimo, miundombinu, elimu, afya na maeneo mengine ya utoaji huduma zikiwemo huduma za benki na utalii. Hata hivyo, juhudi za pamoja bado zinahitajika katika kuendeleza nyanja hizo za maendeleo kwa kasi zaidi na kwa faida ya kila mmoja wetu. Ni vyema kwa kila mwenye nafasi na uwezo ajitume kwa bidii zaidi na kufanikisha malengo yetu tuliojiwekea katika mipango mbali mbali kama vile Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondosha Umasikini (MKUZA) pamoja na Malengo ya Milenia. Kwa kufanya hivyo pato letu la taifa na la mtu binafsi litaongezeka.


Tuzidishe nguvu za ujasiriamali, ujima na mashirikiano katika shughuli za maendeleo zinazopangwa na serikali; kamati za shehia na wilaya; pia tuzitumie vyema fursa zinazotolewa na mifuko ya maendeleo ya jamii kama TASAF na mengineyo kwa kuimarisha huduma za jamii ndani ya majimbo yetu. Kwa hakika ushirikiano na umoja wetu utatufikisha pahala pazuri zaidi. Kwa mfano hivi karibu nilitembelea miradi ya ujenzi wa barabara za ndani Pemba na kushuhudia wananchi wenyewe, wake kwa waume, wakishiriki katika ujenzi wa barabara hizo kwa bidii. Wananchi hao ambao wamepatiwa ajira katika miradi hio, hupatiwa mafunzo maalum ya ujenzi na ukarabati wa barabara hizo kwa lengo la kuajiriwa tena hapo baadae kwa kazi za ukarabati. Utaratibu huo utahakikisha uimara wa barabara zetu wakati wote pamoja na ajira ya kudumu kwa baadhi ya wananchi wetu vijijini. Kwa siku zijazo tutapeleka baadhi ya wanavijiji kutoka Unguja huko Pemba wakajifunze utaalamu huo ili utumike kwa ujenzi wa barabara za vijijini hapa Unguja.


Ndugu Wananchi,

Hatuna budi kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukamilisha nyingi ya shughuli zetu muhimu za maendeleo. Miongoni mwa shughuli hizo ni ukarabati wa barabara za mijini ambazo nyingi zao zimefanyiwa matengenezo makubwa; mji umepambika na unang’ara. Ninalousia sana ni kudumisha maadili ya usafi wa mji, pamoja na kuepuka utupaji taka taka ovyo barabarani. Mwenyezi Mungu anatuhimiza sana suala la utunzaji wa mazingira, hivyo ni vyema turejeshe akhlaki zetu za kuzitunza bustani zetu ili mji upendeze zaidi. Mfano mzuri ni utunzaji wa bustani yetu ya Forodhani.


Kwa upande wa Pemba, pia, tumebarikiwa kupata umeme wa uhakika tokea mwezi wa Juni mwaka huu. Hatua imeanza kwa kasi nzuri yenye kushajiisha harakati za maendeleo na ajira kwa vijana wetu. Kufuatia hatua hiyo kisiwa cha Pemba kimezidi kupendeza pamoja na kuongezeka kwa kasi ya harakati za kiuchumi na hivyo kupelekea kuwa na mchango mkubwa wa maendeleo ya nchi yetu. Majumba ya fakhari yanayojengwa pembezoni mwa barabara za miji ya Pemba ni miongoni mwa dalili za maendeleo ya wananchi. Inafaa tushukuru.


Kwa upande wa Zanzibar kama kila mmoja wetu anavyoelewa, tumefanikiwa kufunga majenereta mapya ya umeme wa dharura ambayo yanauwezo wa kutoa umeme wa Megawati 25.


Halikadhalika, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukamilisha ujenzi wa barabara mpya ya kurukia na kutulia ndege (runway) katika uwanja wetu wa kimataifa ambao kwa sasa unajulikana kwa jina la “Abeid Karume International Airport”. Kiwanja hicho hivi sasa kina uwezo wa kuhudumia ndege za aina zote duniani bila ya matatizo. Kukamilika kwa mradi huu kutatuwezesha kupokea wageni wengi zaidi na kuimarisha shughuli za utalii ambao ndio muhimili mkuu wa uchumi wetu. Nachukua nafasi hii kueleza kuwa maendeleo haya yaliyofikiwa yamefungua fursa zaidi za ajira, ukuaji uchumi na kukua kwa pato binafsi la kila mwananchi.


Natoa wito kwa vijana na wananchi wote kwa jumla kuzitumia vyema fursa hizo kwa kujipatia ajira binafsi kwa misingi ya kujitegemea na kujiongezea pato lao. Vijana wetu wachukue juhudi za makusudi za kujiendeleza katika nyanja mbali mbali za elimu, zikiwemo nyanja za teknolojia, ili kuweza kukabiliana na utandawazi na ushindani katika soko huru la ajira hasa kufuatia makubaliano ya kuanzishwa kwa soko la pamoja la Afrika Mashariki.


Ndugu Wananchi,

Sio nia yangu siku ya leo kuzungumzia siasa, maendeleo ya kiuchumi au ustawi wa jamii, ila nimekusudia kuhusisha wito wa ushirikiano na maneno ya Mwenyezi Mungu ya kutuamrisha tushirikiane katika mema na kuepuka kuhasimiana. Idd ni siku adhimu ya furaha na tuna wajibu wa kusherehekea kwa pamoja na kuikuza furaha hiyo.


Mwisho:

Ndugu Wananchi,

Sina budi kuitumia fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa ndugu zangu waislamu na wananchi wote kwa jumla kwa utulivu, wema, umoja na heshima mlionipa kwa kunipokea rasmi katika sherehe zetu za Idd zote mbili kila mwaka na kuzisikiliza hotuba zangu zenye munasaba na sherehe zenyewe. Tegemeo langu kubwa ni kuwa hotuba hizo zimeleta faraja kwenu na kuuona muelekeo thabiti wa uislamu wetu ndani ya nchi yetu na sera zake za maendeleo.


Tabia zenu za uvumilivu na subira ni miongoni mwa sifa zetu Wazanzibari na ndio hasa (sifa zenu hizo) zilizonipa moyo kuendelea kuutafuta umoja na mshikamano miongoni mwetu wa kujenga nchi yetu na kushirikiana na wenzangu katika kuandika historia mpya nchini mwetu.


Tegemeo langu katika sikukuu zetu za Idd zinazofuatia tutaweza kuuganisha nasaha zetu zilizotangulia na zijazo kwa manufaa ya dini yetu na nchi yetu.


Kama kawaida napenda kutoa wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto wawe waangalifu barabarani pamoja na abiria wao kwa kuendesha vyombo vyao kwa mwendo wa usalama na bila shaka jeshi letu la Polisi kwa kutumia kitengo chake cha usalama barabarani watalisimamia jukumu hili vilivyo.


Pia, natoa shukrani zangu kwa Masheikh kwa kuiongoza ibada katika mfungo wote wa Ramadhan pamoja na kufanikisha sala na baraza letu la Idd Kitaifa.


Ndugu Wananchi,

Kwa kumalizia, nachukua nafasi hii kutoa salamu zangu za Idd na za aila yangu kwa wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania yote. Pia, tunatuma salamu kwa jamaa na marafiki waliopo nje ya nchi. Aidha, kwa niaba yangu na wananchi wa Zanzibar natoa salamu za Idd kwa ndugu waislamu duniani kote kupitia mabalozi wao waliopo hapa na Tanzania Bara. Idd ni wakati wa kukumbushana umoja wa waumini kama tulivyoambiwa kuwa waislamu sote ni ndugu. Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe baraka, sisi na aila zetu zote, atupe jaza njema na kutukubalia dua zetu tunazoziomba kila wakati.


Baada ya maelezo hayo, nakutakieni nyote mliohudhuria Baraza la Idd na wanaofuatilia sherehe hii kupitia vyombo vya habari, Idd ya kheri na baraka.


Wabillahi Ttawfiq


IDD MUBARAK

WA KULLU AAM WA ANTUM BIKHEIR

WASSALMU ALEYKUM WARAHMATULLAHI WABARAKATU


Ahsanteni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.