WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame amesema kuwa kuundwa kwa Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutasaidia kuyapatia ufumbuzi maslahi ya wafanyakazi na wananchi kwa jumla.
Dk. Mwinyihaji aliyasema hayo leo katika hafla ya kumkabidhi majukumu ya Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inayokuwa chini ya uongozi wa Mhe. Waziri Haji Omar Kheir, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Mwinyihaji alisema kuwa ni lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuona maslahi ya wafanyakazi yanapatiwa ufumbuzi ambayo ni hatua moja wapo ya maendeleo nchini.
Alieleza kuwa wafanyakazi wanamatumaini makubwa kuwa changamoto mbali mbali zinazowakabili zitapatiwa ufumbuzi kupitia Wizara hiyo kwa mashirikiano makubwa ya pamoja.
Waziri Mwinyihaji alitoa pongezi kwa Serikali kwa kuunda Wizara hiyo mpya na kusisitiza kuwa ni Wizara muhimu katika Wizara za nchi ambayo umuhimu wake unajulikana Kimataifa.
Dk. Mwinyihaji alimpongeza Waziri Kheri kwa kuteuliwa nafasi hiyo na kumkaribisha katika Afisi ya Rais Ikulu ambapo alimuahidi kumpa mashirikiano ya kutosha.
Aidha, Dk. Mwinyihaji alieleza kuwa mchakato wa kuundwa kwa Wizara hiyo ulienda vizuri kwa kuandaa Sera na Sheria. Na kusisitiza kuwa kutokana na umahiri, uzoefu na uchapakazi wa Waziri Kheri ana matumaini makubwa kuwa ataisimamia vyema Wizara hiyo.
Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Haji Omar Kheri alitoa shukurani kwa makaribisho aliyoyapata na kueleza kuwa jambo kubwa ambalo litaleta mafanikio katika kuendeleza Wizara hiyo ni mashirikiano.
Alieleza kuwa mashirikiano ni jambo muhimu kwani matumaini ya wafanyakazi na wananchi ni lazima yatekelezwe kwa taratibu na sheria zilizopo ambapo hayo yatafikiwa iwapo kutakuwepo kwa mashirikiano mazuri.
Waziri Kheri aliahidi kutoa mashirikiano makubwa kwa wafanyakazi na watendaji wote wa Wizara hiyo na nyenginezo kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya Wizara hiyo sanjari na maendeleo ya nchi na wananchi wake.
Nao viongozi, wajumbe na wafanyakazi kutoka Tume ya Utumishi Serikalini na Idara na Taasisisi nyenginezo zilizokuwa chini ya Utumishi walimuahidi Waziri huyo kumpa mashirikiano ya kutosha ili kufikia lengo lililokusudiwa katika kuletea maendeleo nchini.
Aidha, wafanyakazi hao walieleza kuwa kutokana na wananchi kujengeka imani kubwa kutokana na Serikali yao ya Umoja wa Kitaifa watahakikisha wanatoa kila msaada wa kumsaidia Waziri huyo ili kufanikisha na kuendeleza vizuri Wizara hiyo kwa maendeleo ya Taifa.
Sambamba na hayo, wafanyakazi hao walimpongeza Dk. Mwinyihaji kwa mashirikiano yake mazuri aliyowapa wakati akiwa Waziri katika Wizara hiyo na kueleza kuwa mafanikio makubwa yalipatikana chini ya uongozi wake.
No comments:
Post a Comment