Na Mwanajuma Abdi
JUMLA ya wanafunzi 25,133 wanatarajiwa kufanya mitihani ya Taifa ya kumaliza darasa la saba itayoanza leo hadi Novemba 25.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdulla Shaaban, alitoa taarifa hizo jana, kwa vyombo vya habari huko Mazizini nje kidogo wa Mji wa Zanzibar, mara baada ya kukabidhiwa Ofisi hiyo na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Haroun Ali Suleiman.
Kati ya watahiniwa hao wavulana ni 11,558 na wasichana ni 13,575.
Mitihani hiyo itafuatiwa na mithani mengine ya kidato cha pili ambayo itaanza Novemba 29 hadi Disemba 4 na kuwashirikisha watahiniwa 21,465, ambapo kati yao wasichana ni 11,616.
Waziri Shaaban amewataka wazazi na walezi wa watahiniwa kuwahimiza watoto wao kufuata kanuni na taratibu zote za mitihani zilizowekwa.
Aidha aliwataka watahiniwa hao waache kuchukua vifaa visivyohitajika katika mitihani ikiwemo simu za mikononi, sambamba na kutokatoka nje ya chumba cha mitihani kabla ya kutimia nusu saa tokea kuanza kwa zoezi hilo na kutowasiliana na mtu yoyote ndani au nje ya chumba cha mtihani isipokuwa msimamizi.
Aidha alionya juu ya vitendo vya udanganyifu wa mitihani akisema kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yoyote ataebainika kufanya vitendo hivyo au atayemsaidia mwenzake.
Alieleza kwamba udanganyifu katika mitihani hauwasaidii wanafunzi na mara zote huathirika kutokana na vitendo hivyo, ambapo wanaobainika hufutiwa matokeo ya masomo yote hata kama undanganyifu umeonekana katika swali moja au katika somo moja.
Katika mitihani ya mwaka uliopita kesi za uadanganyifu zilikuwa 22, ambapo wahusika walifutiwa matokeo yao.
No comments:
Post a Comment