VIONGOZI na Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wamemaliza kikao chao cha siku moja mjini Gaborone Botswana ambapo walizungumzia masuala mbali mbali yanayohusu Jumuiya hiyo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal alimuwakilisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika mkutano huo ambao ulitanguliwa na sherehe za uzinduzi wa Makao Makuu ya Jumuiya hiyo.
Katibu Mkuu wa SADC, Dk. Tomaz Augusto Salomao aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Grand Palm kuwa viongozi hao wamewaagiza Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Jumuiya hiyo kukamilisha taarifa juu ya ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya za kikanda (ikiwemo SADC) hususan katika suala la namna maamuzi yanavyopitishwa na kutekelezwa katika vikao vya Umoja huo wa Afrika.
Kwa mujibu wa Dk. Salomao kikao cha viongozi wa SADC kilichofanyika mjini Windhoek Namibia mwezi Agosti mwaka huu kilieleza haja ya kufanyika kikao maalum cha kuzungumzia suala la hilo baada ya kutafakari matukio kadhaa yanayohusiana na maamuzi yanavyofanyika ndani ya vikao vya AU.
“Wameona (viongozi wa SADC ) mambo hayaendi vizuri,maamuzi mengine hayafuati utaratibu na miongozo ya Umoja huo hivyo wamewataka Mawaziri wa Mambo ya Nje wa SADC wakamilishe taarifa yao haraka ili iwasilishwe katika kikao kijacho cha AU kitakachofanyika mjini Adis Ababa,” alibainisha Dk Salomao.
Katibu Mkuu huyo wa SADC pia alisema katika kikao hicho, wakuu hao walipokea taarifa juu ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliofanyika Oktoba 31 ambapo Jumuiya hiyo ilipeleka timu ya waangalizi 97.
Dk. Salomao alifafanua kuwa taarifa ya awali ya Timu ya waangalizi hao ilieleza kuwa uchaguzi huo ulifanyika kwa uhuru,haki na kwa utulivu na kwamba SADC imempongeza Rais Kikwete kwa uchaguliwa tena kuiongoza Tanzania na kuwapongeza wananchi wa Tanzania kwa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu.
Katika mkutano huo masuala ya hali ya kisiasa katika nchi za Zimbabwe na Madagascar yalijadiliwa na viongozi hao wa SADC walimtaka msuluhishi wa mgogoro wa Zimbabwe Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kuendelea na mashauriano na pande zinazohusika katika serikali ya umoja wa kitaifa nchini Zimbabwe ili kukamilisha utekelezaji wa makubaliano yaliyotiwa saini Septemba 15, 2008.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ulijumuisha pia Balozi wa Tanzania nchini Botswana mwenye makaazi yake mjini Pretoria Afrika Kusini, Balozi Radhia Msuya na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajab Gamaha.
Akiwa nchini Botswana Makamu wa Rais alikutana pia na Watanzania wanaoishi nchini humo.
No comments:
Post a Comment