Habari za Punde

WAZIRI JIHADI AWAPIGIA UPATU WADAU KUISAIDIA ZANZIBAR HEROES.


Apongeza uzalendo wa Zanzibar Ocean View, Jazeera


Na Donisya Thomas, Dar-es Salaam

WITO umetolewa kwa wadau wa soka, mashirika na kampuni binafsi kujitokeza kuisaidia timu ya Taifa ya Zanzibar Heroes ili iweze kufanya vizuri katika mashindano ya Chalenji yanayoendelea jijini hapa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Abdilah Jihad Hassan, wakati akiikabidhi timu hiyo fedha zilizotolewa na uongozi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View kufuatia ushindi wa mabao 2-0 ilioupata dhidi ya Sudan juzi.

Alisema timu hiyo ni ya Wazanzibari wote, hivyo hawana budi kuiunga mkono pamoja na kuipatia misaada ya aina mbali mbali ili iweze kupeperusha vyema bendera ya nchi yao katika mashindano hayo.

Waziri Jihad, aliwataka wadau wengine kuiga mfano wa hoteli hiyo kuipatia misaada timu yao ambayo inaiwakilisha Zanzibar katika mbio hizo zinazosimamiwa na CECAFA.

Jihad aliikabidhi Zanzibar Heroes shilingi 4,000,000 zilizotolewa na hoteli hiyo pamoja na laki tano ambazo zimechangiwa na Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo Nassor Salum Ali 'Jazeera' mara baada ya kumalizika kwa pambano lao na Sudan katika kundi B la ngarambe hizo.

Nae Nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub 'Cannavaro', aliwataka Wazanzibari kuungana na kuipa kila aina ya msaada wa hali na mali kwani hiyo ni timu yao hivyo wanatakiwa kuiunga mkono na kuhakikisha inatwaa ubingwa.

"Tunawaomba Wazanzibari wajue kwamba hii timu ni yao na wanatakiwa kutuunga mkono ili tuweze kufika mbali zaidi kwani uwezo tunao ila kinachotakiwa ni ushirikiano wa pamoja kwa Wazanzibari wote" alisema Cannavaro.

Aidha aliushukuru uongozi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View kwa uzalendo wake na moyo wa kuthamini michezo na kuona umuhimu wa kuipa sapoti timu hiyo, na kuahidi msaada huo utakuwa chachu ya kuuleta ubingwa visiwani humu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.