Habari za Punde

MASAUNI APUNGUZA TATIZO LA MAJI KIKWAJUNI

Na Khamis Mohammed

ZAIDI ya shilingi milioni 50 zimetumika kwa uchimbaji wa visima vya maji safi na salama kwa wananchi wa jimbo la Kikwajuni mjini Unguja.

Mradi huo unaendeshwa na Mbunge wa jimbo hilo, Hamad Yussuf Masauni, kwa kushirikiana na wananchi katika kuhakikisha wanaondokana na tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi hao walisema, hivi sasa wameondokana na shida hiyo iliyokuwa ikiwasumbua kwa miaka mingi kwa kiasi kikubwa.

Salma Juma, mkaazi wa Kikwajuni juu, alisema, walikuwa wakilazimika kufuata huduma ya maji kwa masafa makubwa huku wakitumia zaidi ya shilingi elfu tano ili kukidhi mahitaji ya maji, lakini hivi sasa wameondokana na tatizo hilo.

"Tulikuwa tukipandisha maji kwa kifua kutoka chini na kwa kweli hali ilikuwa ngumu", alieleza, Salma ambaye yupo hapo tokea mwaka 1968.

Naye Abeid Hemed, alisema, tatizo la maji safi na salama jimboni humo lilikuwa likiridisha nyuma jitihada za wananchi katika kujitafutia maendeleo ya kila ya siku ya maisha.

Lakini, alisema, tokea mbunge huyo achimbe visima hivyo, tatizo hilo limepungua na kwamba hivi sasa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida bila ya hofu ya kukosa huduma hiyo.

Naye Sheha wa Shehiya ya Kikwajuni Bondeni, Ibrahim Ali, alisema, tatizo la maji katika shehiya yake limepungua huku wakiendelea na jitihada za kuhakikisha maeneo nayo yanapata huduma hiyo.

Jumla ya visima saba tayari vimeshachimbwa na mbunge huyo huku vyengine viwili vikiendelea kuchimbwa katika shehia tofauti za jimbo la Kikwajuni.

Jimbo la Kikwajuni linaundwa na shehiya sita za Miembeni, Kikwajuni Juu, Kiwajuni Bondeni, Kilimani, Kisiwandui na Kisimajongoo.

Visima ambavyo tayari vilivyokwishachimbwa ni Miembeni Jitini, Miembeni klabu, Kilimani Mashariki na Kisimamajongoo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.