Na Suleiman Almas
KAWA limetumika kama stara ya uhifadhi wa chakula kwa wakaazi wa Visiwa vya Unguja na Pemba kwa miaka mingi iliyopita.
Kuna siri kubwa ya mfuniko huo ambao asili ya utengenezwaji wake ni kutoka maeneo haya haya ya Afrika hasa katika sehemu za mwambao.
Wengi wanaolitumia kawa kwa kufunikia chakula hulichukulia sawa na aina nyengine ya mifuniko ya kawaida almuradi funika kitu kisionekane.
Kwa upande wa stara ya kawa husitiri mambo mengi pale linapokuwa limefunika kitu au mara nyengine hufunika hali ya maisha yaliyomo ndani ya nyumba inayohusika na mgeni anapoingia ndani asijue chini ya kawa kumewekwa nini.
Kutokana na muundo wa kawa kukaa kwake ni kufunika kiwepo kitu au kuwe hapana kitu stara hiyo hubaki palepale imefunika na kumuweka mtu katika kitendawili kwa kiliopo mezani au mkekani.
Si mara nyingi kuliona kawa limewwekwa chali kwa kawaida kuwekwa kwake hukaa mkao wa fudifudi kwa tafsiri ya kufunika.
Ususi wa kifaa hicho hauna tafauti na utengenezaji wa mkoba, mkeka kwa kuwa vyote huundwa kwa kutumia ukindu.
Kwa mujibu wa utamaduni wa watu wa Zanzibar, katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kawa hutumika sana kuficha kwa tafsiri ya kuhifadhi futari kabla ya kuwekwa kwa mlo wa pamoja.
Chombo hicho kina uwezo wa kufunika vyakula vingi kwa wakati mmoja kulingana na ukubwa wa kifaa hicho cha asili visiwani humu.
Siri nyengine ya ya kawa ni kutoa mvuto kwa mlaji kuwa na hamu ya kufunua ili ajue kilichomo chini ya hifadhi hiyo.
Rangi za kili zilizo nakishiwa na msusi humshawishi baba anapotaka kula hupenda kufunua mwenyewe ili agundue kilichomo ndani mara nyingi sana hufanyika kwa jamii ya waswahili wa Zanzibar.
Chungu joto (Hot pot) hakiwezi kuipiku sifa ya kawa kwa uhifadhi wa chakula kiafya, ladha na hata ustahamilivu wa kuharibika wakati wa kuwekwa kwake.
Chakula kilicho hifadhiwa na kawa na kile kiliomo ndani ya chungu joto wakati wa kukila ladha huwa tafauti hiyo ni kwa mujibu wa watumiaji wa vitu hivyo viwili walibainisha.
Umoto sawa, lakini uzuri wa chakula hupotea pindipo kikaa muda mrefu kwenye chombo hicho ikilinganishwa na ufunikwaji wa kawa.
Kwa uasilia wake kawa halihitataji kupakwa rangi au kuongeza urembo wa mauwa kwa msukaji mzuri wa zana hiyo hulifanya kujitosheleza kwa muundo wake wa awali.
Wasusi akina mama, bado wana kila sababu ya kuendelea na sanaa ya utengenezaji makawa na zile taasisi kama UWAZI zinastahili kupewa msukumo wa kutafuta masoko ya ndani na nje kwa bidhaa hiyo inayozalishwa na wazalishaji wadogo wadogo.
Vitu asilia vinavyozalishwa na wananchi ni vyema kukawepo msukumo na nguvu za pamoja kuishajiisha jamii kuendelea kuwepo, ili visipotee kama baadhi ya mambo yaliyotoweka kwa sababu za kukosa kutunzwa, kudumishwa na kuendelezwa.
Wafinyazi, wachongaji nao wana mambo mengi ya kuendelezwa na mengine kuyafufua kwa dhamira ya kurejesha uasili wa mambo ya kifundi yaliyopotea kwa sababu ya mapokezi ya tamaduni za kigeni.
Tamaduni hizo huingia nchini kupitia namna mbalimbali ikiwemo mitandao, wageni, yote hayo huchangia kuporomoka kwa ubunifu wa kutumia raslimali ziliopo nchini.
Chungu, mkungu, mtungi, mwiko, upawa, kunuto, chano vyote hivyo vilikuwa na siri kubwa ya matumizi yake kwa jamii ya Kizanzibari.
Vijana wa kileo wamekosa uelewa wa kutumia vitu kama hivyo kijamii, kiuchumi na kiutamaduni ni wazi hali hiyo hairidhishi kuendelea kuwepo Visiwani mwetu itafutiwe njia ya kuiondosha
No comments:
Post a Comment