Habari za Punde

CANNAVARO: OFA YANGU EL MEREIKH FAHARI KWA ZANZIBAR

Na Aboud Mahmoud
BEKI mahiri wa timu ya Yanga ya Dar es Salaam Nadir Haroub Ali 'Cannavaro', amesema kuwa, nafasi aliyopata kuchezea timu ya El Mirreikh ya  Sudan, ni fahari kwa Zanzibar kutoa wachezaji wa kulipwa.


Mlinzi huyo tegemeo Jangwani na timu za Taifa Stars na Zanzibar Heroes, alizungumza na gazeti hili jana akiwa kisiwani hapa kwa mapumziko baada ya kuisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa nne wa Kombe la Kagame hivi karibuni.

Alisema kutakiwa na mabingwa hao wa Sudan, ni ushahidi wa hazina kubwa ya wachezaji wenye vipaji walioko kila pembe ya visiwa vya Unguja na Pemba, ambavyo vinahitaji msukumo ili viweze kuonekana katika medani ya kimataifa.

"Hii ni furaha kwangu, pia ni faraja kwa nchi, familia na wapenzi wote wa soka wa Zanzibar, ninaahidi kuitumia vyema fursa hii kupeperusha bendera yetu ili Zanzibar iendelee kuwa chaguo la vipaji kwa timu mbalimbali Afrika na duniani kwa jumla", alifafanua mlinzi huyo mwenye bidii uwanjani.

Alisema kujiunga na klabu hiyo maarufu, kutamsaidia kuinua hali yake ya maisha pamoja na kuimarisha kiwango chake jambo linaloweza kumfungulia milango zaidi ya soka la kulipwa.

Tayari mlinzi huyo aliyeng'ara katika michuano ya Kagame mjini Dar es Salaam, amemalizana na klabu hiyo na kusaini mkataba wa miaka miwli ambao pia umeridhiwa na timu yake ya Yanga.

Cannavaro anatarajia kwenda Khartoum tayari kuanza kuitumikia El Mirreikh katika kibarua chake hicho kipya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.