Rajab Mkasaba, Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kisiwani Pemba kushirikiana na serikali katika kupambana na wanaofanya magendo ya karafuu kwani hawana nia njema na serikali na nchi kwa jumla.
Amesema kuwa iwapo mwananchi atauza karafuu zake kwa njia ya magendo ajue kwamba kipato kitakachopatikana hakitomsaidia yeye binafsi wala serikali.
Dk. Shein aliyasema hayo katika ziara yake kisiwani Pemba wakati alipokuwa akizungumza na wananchi huko katika banda la karafuu Daya Mtambwe mara baada ya kutembelea kituo cha ununuzi wa karafuu ZSTC, Daya Mtambwe ambapia pia alifuatana na Mama Mwanamwema Shein na viongozi wngine wa seriali na vyama vya siasa.
Katika maelezo yake Dk. Shein aliwasisitiza wananchi wa Daya Mtambwe pamoja na wananchi wote kwa ujumla kutambua kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuuza karafuu serikalini kwani itasaidia matumizi ya kuimarisha huduma za maendeleo pamoja na kuwasaidia wao wenyewe kuendeleza maisha yao.
Aliwataka wananchi wasidanganyike kwani magendo ni kitu kibaya na hakina tija ya aina yoyote katika biashara ya zao hilo la karafuu na kuwasisitiza umuhimu wa kuuza karafuu zao serikalini kwa kupitia katika Shirika lake la ZSTC.
“Tusihadaike na wapiti njia tusiuze karafuu zetu kwa njia ya magendo, tuiuzie serikali na tuisikilize kwani sote tuna malengo ya kuendeleza serikali”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa wananchi kisiwani Pemba wakiwemo wananchi wa Daya Mtambwe na kueleza furaha yake kutokana na jitihada zao walizozianza za kuuza karafuu serikali na kuwataka waendelee na utaratibu wao huo.
Pia, Dk. Shein aliwapongeza wananchi wa Daya Mtambwe kwa kuwakaribisha na kushirikiana nao vizuri wafanya kazi wa Shirika la ZSTC kwa kuuza karafuu zao sanjari na kukifufua kituo hicho ambacho kilikuwa kimefungwa kwa takriban miaka saba kutokana na wananchi kutouza karafuu zao wakati huo kwa ZSTC kupitia kituo hicho.
Dk. Shein pia, aliwapongeza wananchi kwa kupalilia mashamba yao ya mikarafuu kwa wakati, kuvuna na kuwasisitiza haja ya kuendelee kuitunza mikarafuu kutokana na umuhimu wake na kusisitiza kuwa karafuu za Zanzibar ndio pekee zino sifa duniani.
Dk. Shein alisema kuwa hayo maendeleo yanayosisitizwa kila siku ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta zake zikiwemo afya, elimu, maji safai na salama, hicho kilimo chenyewe na sekta nyenginezo huimarishwa kutokana na fedha hizo za karafuu.
Akitoa maelezo yake, Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Daya Mtambwe kuwa nia ya serikali ya kuijenga barabara yao ya kutoka Bahanasa hadi Mtambwe kwa kiwango cha lami chini ya ufadhili kutoka serikali ya Marekani ipo pale pale na kazi za ujenzi huo zitaanza wakati wowote kwani tayari zimeshatengewa fedha zake.
Alieleza kuwa mbali ya barabara hiyo pia, serikali itaangalia uwezekano wa kuziweka vizuri kwa kuzipitishia burdoza zile barabara ndogo ndogo ambazo inasemekana baada ya kufanyiwa marekebisho hayo zitasaidia kupitisha karafuu kuleta vituoni kwa urahisi zaidi.
Katika maelezo yake hayo, Dk. Shein alieleza kuwa ni historia kwa zao hilo la karafuu hapa Zanzibar kuwa na bei kubwa kama hiyo na kueleza kuwa hali hiyo inatokana na dhamira za serikali katika kuleta mabadiliko ya kilimo ikiwemo kuliimarisha zao la karafuu.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Daya Mtambwe kuwa serikali imo katika jitihada za kupambana na bei za vyakula kutokana na kubadilika kwa maisha kueleza kuwa na tayari imeshafanya mazungumzo na wafanyabiashara kwa kuangalia hali hiyo na kueleza nia ya serikali kuimarisha Bandari Huru.
Alieleza kuwa juhudi hizo za kuzungumza na wafanya biasahara wa vyakula zimesaidia kwani ni kipindi sasa bei za sukari, mchele na unga hazijapanda huku akieleza nia ya serikali kupitia Wizara ya husika kuzungumza na wafanyabiasahara wa nguo kutokana na uhali wa bidhaa hiyo uliopo hivi sasa ambapo alikiri kuwa hali hiyo pia inachangiwa na kupata kwa maisha duniani kote.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Daya Mtambwe kuwa serikali ina mpango wa kutoa miche ya mikarafuu laki5 ambayo tayari imeshazalishwa katika kitalu cha Chanjani na kuigawa kwa wananchi bure ndani ya miezi michache ijayo ambapo pia, watapewa wananchi ambao mikarafuu yao imekatwa kutokana na kpitishwa barabara katika eneo hilo.
Nae Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mhe.Nasor Mazrui alimueleza Dk. Shein kuwa kufarajika kwake na hali inayoendelea hivi sasa katika uendelezaji wa uuzaji wa karafuu katika kituo hicho cha Daya Mtambwe.
Nao wafanyakazi wa ZSTC kituoni hapo walimueleza Dk. Shein kuwa wamefurahishwa na mashirikiano mazuri wanayoyapata kituoni hapo hivi sasa na kueleza kuwa ni tofauti na hapo siku za nyuma ambapo mashirikiano hayakuwepo na kupekekea kukifunga kituo hicho.
Wananchi wa Daya Mtambwe nao walitoa shukurani na pongezi kwa Dk. Shein pamoja na serikali yake anayoiongoza kwa kuonesha mwanzo mzuri wa matumaini na mwanga wa maendeleo na uimarishaji wa maisha yao kutokana na kupandisha kwa bei ya zao hilola karafuu na kuahidi kuziuza karafuu zao serikalini.
Baada ya hapo Dk. Shein alitembelea kambi ya karafuu ya Daya Mtambwe ambapo wakulima walieleza kufarahishwa na hatua za serikali na kuahidi kushirikiana nayo ikiwa ni pamoja na kuziuza karafuu zao katika vituo vya ZSTC.
Dk. Shein pia, alitembelea eneo la Bandari ya Wete na kuangalia ghala la karafuu pamoja na kuangalia karafuu zilizokamatwa ambazo zilikuwa zikisafirishwa kimagendo.
No comments:
Post a Comment