Habari za Punde

UANZISHWAJI CHUO CHA ANGA, UBAHARIA WAIVA

Na Mwantanga Ame

WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud amesema kuanzishwa Chuo cha Usafiri wa Anga na Ubaharia kunalenga kuleta mageuzi ya kiajira kwa vijana wa Kizanzibari watakasoma fani hizo.


Masoud alisema hayo jana ofisi za Mamlaka ya Viwanja wa Ndege Zanzibar, alipokuwa akizindua kamati mbili za kusimamia uanzishwaji wa vyuo hivyo, ambazo zitatoa mapendekezo serikalini namna ya kufanikisha mpango huo.

Alisema sekta ya mawasiliano inahitaji mabadiliko ambayo yataleta mbinu mpya za kisasa na kitaalamu, hivyo Zanzibar lazima ichangamkie mabadiliko ili isiachwe nyuma kwa kuanzisha vyuo vitakavyoweza kuwafunza fani hizo vijana.

Waziri huyo alisema kuwepo vyuo hivyo kutawafanya vijana wa Zanzibar kuzitumia fursa za ajira za fani hizo bila ya wasiwasi, kwani   wengi wao tayari ni wenye kuishi katika visiwa ambavyo wananchi wake hutegemea usafiri wa bahari pamoja na ndege.

Alifahamisha kuwa hivi sasa Zanzibar imekuwa na mabaharia wengi wanaofanya kazi katika meli mbali mbali za kigeni duniani lakini tatizo kubwa linalowakabili ni elimu ya kutosha juu ya shughuli hizo, jambo ambalo linaweza kuwasababishia kutofahamu haki zao wakiwa kazini.

Waziri huyo alisema kuwepo kwa vyuo hivyo hapa Zanzibar kutasaidia kupatikana kwa faida kadhaa ikiwemo kuokoa fedha nyingi ambazo zimekuwa zikitumika kuwasomeshea vijana nje ya Zanzibar.

Alisema nia ya serikali ni kuhakikisha inaleta mabadiliko katika sekta ya mawasiliano ya anga na bahari, ikiwa pamoja na kufungua milango kwa taasisi za nje kushirikiana na serikali kuwekeza kwa pamoja.

Alisema kamati hizo zitazingatia hadidu rejea tisa ikiwemo ya kuangalia kwa kina taratibu za kuanzisha chuo cha Usafiri wa Anga na Ubaharia hapa Zanzibar, kupendekeza mfumo wa uendeshaji wa Chuo hicho na kuangalia kwa kina soko la Chuo hicho hapa Zanzibar na nje ya nchi.

Maeneo mengine ambayo kamati hizo itazingatia ni kuendeleza taratibu zitazotumika katika kutoa mafunzo katika chuo, kupendekeza mipango ya muda mfupi na muda mrefu ya kitaaluma na uendeshaji wa vyuo hivyo na kupendekeza utaratibu za kutambuliwa Chuo hicho duniani na taratibu za kuingia kwenye ‘White list’ ya I.M.O.

Kamati itakayosimamia uanzishwaji wa vyuo hivyo, Chuo cha Usafiri wa Anga, Mwenyekiti wake ni Abdulla Hussein Kombo, wajumbe ni Kepteni Said Ndumbugani, Abdulhalym M. Sururu, Said Sumry, Seif Said Issa, Kapten Khamis Suleiman na Katibu wake ni Zaid R. Taufik.

Upande wa Chuo cha Mabaharia, kamati hiyo inaundwa na Mwenyekiti Abdulla Hussein Kombo, wajumbe ni Abdulrahman Chande, Injinia  Haji Vuai Ussi, Salma Suleiman Omar, Kepteni Alhaj Sururu, Said Salim Bakhressa na Katibu wake ni Zaid R. Taufik.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Anga, Said Ndumbugani, akitoa shukrani zake alisema dhamira ya mamlaka hiyo ni kuona inainua sekta ya usafiri wa anga ambapo watahakikisha wanafanikisha mpango huo wa serikali kwani utawawezesha Wazanzibari kupata elimu hiyo hapa nchini.

Katika hatua nyengine waziri huyo alisema Zanzibar inajiandaa kuanzisha shirika lake la ndege, huku nchi kadhaa zikiwa tayari kushirikiana katika mpango huo zikiwemo Falme za Kiarabu, Malaysia, na Wazanzibari walioko nchini Oman huku mazungumzo yakiendelea katika kufanikisha mpango wa kuanzishwa shirika hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.