Habari za Punde

UJENZI WA UDOM KIKWETE ATAKUMBUKWA - MAALIM SEIF

Na Abdi Shamnah

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ni miongoni mwa mambo yatakayomfanya Rais Jakaya Mrisho Kikwete akumbukwe kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania.


Amesema chuo hicho kinacholenga kuchukua wanafunzi 40,000 kwa mwaka katika fani tofauti pale kitakapokamilika, kitakuwa ndio kikubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo kumudu ushindani na nchi jirani, pamoja na kufikia dhana ya mafanikio ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Maalim Seif amesema hayo leo katika ukumbi wa Chuo hicho mjini Dodoma alipofika kukitembelea pamoja na kupokea  taarifa juu ya shughuli za chuo hicho.

Alisema ametiwa moyo sana na maendeleo makubwa yaliofikiwa na chuo hicho chenye muundo wa kitaifa, kwa kuwahusisha wanafunzi na wafanyakazi kutoka sehemu zote za Tanzania, na kutaka hatua hiyo iendelee ili kuwavunja moyo maadui wasioutakia mema Muungano.

Alipongeza juhudi za uongozi wa chuo hicho kwa kuwa na mikakati madhubuti ya kupata walimu wenye sifa na uwezo, watakaofanikisha kuifikia azma ya Serikali katika kuimarisha kiwango cha elimu nchini.

Aliwataka wananchi kutolalamikia hatua inayochukuliwa na uongozi wa chuo hicho ya kuajiri walimu kutoka nje ya nchi (ikiwemo India), kwa misingi kuwa kuna mfumo mzuri katika kuchuja waliomu walio bora.

Aidha aliwataka wasomi kujiuliza sababu za kushuka kwa kiwango cha elimu nchini na kushauri juhudi zichukuliwe kuwawezesha wahitimu wanaomaliza chuo hicho kuweza kufahamika na kutoa ushindani dhidi wahitimu wengine duniani kote, kwa kuzingatia kuwa chuo kina walimu na vifaa vilivyo bora.

Pia alipongeza mfumo wa kuchuja wanafunzi wanaoingia chuoni hapo kwa kuzingatia sifa zinazohitajika, hatua aliyosema itadumisha sifa ya chuo hicho.
Maalim Seif alivipongeza vitivo (College) vya chuo hicho kwa kujitegemea wenyewe na kuisifia mipango bora ya college ya Afya kwa kuwa na mipango bora ya ujenzi wa hospitali kubwa itakayoendesha uchunguzi za kina kuhusu magonjwa mbali mbali (ikiwemo cancer) pamoja na kutoa tiba, hatua aliyosema itaokoa fedha nyingi za kusafirisha wagonjwa nje ya nchi.
Alisema pale malengo hayo yatakapokamilika, Watanzania watakuwa na hakika ya kupata matibabu bora ya magonjwa hayo pamoja na kuvutia wageni kuja kutibiwa.

Katika hatua nyingine, Maalim Seif alitoa changamoto kwa uongozi wa chuo hicho kuangalia kwa kina mitaala inayofundishwa katika kitivo cha Sayansi ya jamii, ili kuwawezesha wahitimu kuweza kujiajiri wenyewe bila kusubiri ajira toka serikalini.

Alisema uwepo wa vijana wengi waliohitimu na kukosa kazi, kunaiweka nchi katika hatari ya kuibuka kwa machafuko na ghasia.

Katika ziara hiyo Maalim Seif alipata fursa ya kutembelea Colleges mbali mbali za chuo hicho na kupata maelezo juu ya mafanikio na changamoto zinazokabili pamoja na malengo yaliopo.

Nae Msaidizi Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Pro. Kinabo akitoa neno la shukrani alimhakikishia Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar kuwa Chuo kimo katika mchakato wa kuboresha mitaala yake ili kuhakikisha elimu inayotolewa inazingatia  mahitaji yaliopo.

Aidha alisema Chuo kinaendelea na juhudi za kukabiliana na changamoto kubwa ya upungufu wa walimu , ili kuona maendeleo ya kweli yanafikiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.