HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA
MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,
MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA BARAZA LA EID EL FITRI,
AGOSTI, 2011
Bismillah Rahman Rahim.
Naanza kwa jina la Mwenyezi Mungu ambae ni peke yake anayepaswa kuabudiwa na kushukuriwa na viumbe wote. Yeye pekee ndiye anayestahiki kila sifa njema na kila utukufu. Tunakiri kuwa Yeye ndiye mmiliki wa vyote vilivyomo mbinguni na ardhini na hana mfano wake. Naomba sala na salamu zimshukie Mtume wetu Karim Sayyidna Muhammad (SAW) pamoja na Aali zake, Sahaba zake na wote waliofuata njia yake ya uongofu. Tunamuomba Mola wetu atuzidishie rehema na baraka katika maisha yetu hapa duniani na akhera na awape maghfira na rehema wazee, ndugu, marafiki na wenzetu wengine waliokwishatangulia mbele ya haki. AMIN!
Sheikh Saleh Omar Kabhi,
Naibu Mufti;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad,
Makamu wa Kwanza wa Rais;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi,
Makamu wa Pili wa Rais;
Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume,
Rais Mstaafu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Omar Othman Makungu,
Jaji Mkuu;
Mheshimiwa Pandu Ameif Kificho,
Spika wa Baraza la Wawakilishi;
Sheikh Khamis Haji Khamis,
Naibu Kadhi Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri,
Waheshimiwa Mabalozi,
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Ndugu Wageni Waalikwa,
Ndugu Wananchi,
Mabibi na Mabwana.
Assalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh
Baada ya kumtukuza Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala na kumtakia Rehma Mtume Wetu Muhammad (SAW), natanguliza shukurani zangu kwa Mola wetu mwenye huruma, mwingi wa rehema na kila sifa njema na utukufu kwa kutujaalia neema ya uhai na uzima tukaweza kujumuika hapa hivi leo katika hafla hii adhimu. Hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuimaliza funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa salama na amani. Kuikamilisha nguzo hii ya Uislamu ni miongoni mwa rehema na neema zake Mwenyezi Mungu kwetu, kwani wapo wenzetu wengi tulioanza nao kufunga ambao hawakudiriki kuimaliza funga hio ama kwa ugonjwa au kwa kutangulia mbele ya haki. Mola wetu tunamuomba awape shufaa wagonjwa, wale waliotangulia awape hatma njema na sisi atufanyie wepesi katika kufanya yanayomridhia. AMIN!
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Azza Wajala azikubali funga zetu na atujaaliye tuwe ni wenye kunufaika na fadhila za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kurehemewa, maghfira na kutunusuru na adhabu za Jahhanam. AMIN!
Ndugu Wananchi,
Leo ni Sikukuu ya Eid el Fitri, ni siku ya furaha kwa Waislamu sote baada ya kuikamilisha nguzo ya nne ya Kiislamu (saum). Natoa pongezi kwa Waislamu wote duniani kwa kuweza kuikamilisha faradhi hii na napenda kuitumia nafasi hii kuwashukuru mashekh na waalimu wetu walioendesha darsa, kutoa mawaidha na kuongoza ibada mbali mbali nchini mwetu katika kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Namuomba Mwenyezi Mungu Subhannahu Wataala awape kila la kheri, afya, nguvu na umri mrefu waendelee kutupa mafunzo na mawaidha juu ya dini yetu yanayotokana na kitabu kitukufu cha Qur-an na Hadithi za Bwana Mtume ili tupate kufuzu hapa duniani na huko akhera tuendako.
Naamini kuwa katika kuitekeleza Saum, kuna baadhi yetu tuliifanya ibada hii katika hali ya matatizo yakiwemo ugonjwa, uhaba wa maji, na hata upatikanaji wa futari yenyewe. Lakini bado tunapaswa kumshukuru Mola wetu kwa neema alizoturuzuku kwa sababu wapo Waislamu wenzetu wa baadhi ya nchi duniani hawakupata fursa ya kufunga Ramadhani katika hali ya utulivu kama alivyotujaalia sisi. Sote ni waumini ni wajibu wetu kumshukuru Allah kama tunavyoelekezwa katika Qur- an tukufu aya ya 7 ya Suratul- Ibrahim.
(Nakumbukeni) Alipotangaza Mola wenu (kuwa) “ Kama mkinishukuru, nitakuzidishieni, na kama mtanikufuru (juweni) kuwa adhabu yangu ni kali sana.”
Ndugu Waislamu,
Kwa dhati kabisa nachukuwa nafasi hii kuwashukuru wakulima na wafanyabiashara kwa kutusaidia katika upatikanaji wa chakula katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Vile vile nawashukuru wafanyakazi wa Mamlaka ya Maji (ZAWA) kwa juhudi zao za kuwapatia maji wananchi wanaoishi katika maeneo yenye upungufu wa maji. Aidha, nawashukuru sana wafanyakazi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuimarisha hali ya amani na utulivu, hasa askari wa usalama barabarani kwa kusaidia kudhibiti ajali za barabarani katika Mwezi wote Mtukufu wa Ramadhani.
Natoa shukurani kwa wananchi wasiokuwa Waislamu kwa kuonesha ushirikiano wa dhati katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Ushirikiano wao umetupa fursa ya kuitekeleza ibada ya Saum katika hali ya utulivu. Naamini walifanya hivi kwa makusudi wakiweka pembeni uhuru walionao kulingana na imani za dini zao. Waislamu ni wajibu kuithamini heshima hii tukiamini kuwa kuheshimiana miongoni mwa waumini wa dini na madhehebu tofauti kuna umuhimu wa pekee katika kudumisha amani ya nchi yetu.
Ndugu Wananchi,
Mwezi tuliomaliza haukuwa Mwezi wa ibada tu, bali kwa hakika ni Mwezi wa mafunzo makubwa. Miongoni mwa mafunzo ya mwezi huu ni pamoja na kuzidisha ucha Mungu, kula riziki za halali, kuepuka kusengenya, kutosema uwongo, kufanyiana ihsani, kuhurumiana na kusaidiana, kufanya uadilifu na kuwa na tabia nzuri zenye kumpa pambo jema Muislamu. Ni vyema tuyaendeleze mafunzo haya muhimu katika miezi kumi na moja iliyobakia. Tukimudu kuyatekeleza haya, tutajenga Taifa bora la wacha Mungu na raia wema na bila ya shaka Mwenyezi Mungu atatufanyia wepesi katika kuzitumia neema zake.
Hatuna budi kukumbushana kuwa mafunzo ya Saum yanahusiana na maisha yetu ya kila siku. Kwa mfano, suala la uadilifu siyo tu sifa ya muumini lakini ni ya kila mmoja wetu hasa kwa viongozi na watumishi wote wa umma. Mwenyezi Mungu anatuambia katika Kitabu chake Kitukufu aya ya 29 ya Suratul Al-Aaraf:
“Sema: Mola wangu ameamrisha uadilifu, (ameniamrisha nikuambieni) elekezeni nyuso zenu (kwake) wakati wa kila sala na mwabuduni yeye tu kwa utii halisi……..”
Kutokana na agizo hili kutoka kwa Mola wetu, tunaona jinsi uadilifu ulivyo muhimu kwetu, tukielewa kuwa kutoutekeleza ni kukosa utii wa maamrisho yake. Aidha, kuna ukweli kuwa uadilifu unasaidia sana kujenga imani za wananchi kwa viongozi wao na watumishi wa umma na kuwafanya wananchi wawe tayari kutoa ushirikiano wao wa dhati katika masuala mbali mbali ya maendeleo.
Nasisitiza suala hili la uadilifu kutokana na umuhimu wake katika jamii. Uadilifu ni kipimo cha imani ya mtu na kumfanya awe raia mwema. Mfanyakazi mwadilifu hutekeleza majukumu yake ipasavyo pamoja na kufika kazini kwa wakati na kuondoka kwa wakati, mfanyabiashara mwadilifu haghushi bidhaa na hakwepi kulipa kodi, mtumishi wa umma hatodai rushwa na mzazi mwadilifu hawezi kuitelekeza familia yake. Ni lazima sote turudi katika njia sahihi na tusimghadhibishe Mwenyezi Mungu. Tunamuomba Mola wetu atuongoze katika njia iliyonyooka na atuepushe na makatazo yake.
Ndugu Wananchi,
Mafunzo mengine tuliyoyapata katika mwezi tuliomaliza ni umuhimu wa kula riziki za halali. Bila ya shaka riziki ya halali inatokana na kazi au chochote kilichochumwa kwa halali. Kila mmoja wetu lazima afanye kazi ya halali ili apate heshima na riziki ya halali. Mola wetu anatutaka tutawanyike katika ardhi yake ili tutafute riziki. Aidha, Bwana Mtume (SAW) ametwambia kwenye moja kati ya hadithi zake kuwa:
”Chumo bora ni lile mja analolichuma kwa mikono yake.”
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa mipango ya kuhakikisha inaongeza fursa zaidi za ajira rasmi na zile zisizo rasmi hapa nchini. Katika mwaka huu wa fedha Serikali inatarajia kuajiri watu wapatao 2,476 kulingana na mahitaji na uwezo uliopo. Tunaelewa kuwa mahitaji ya fursa hizo ni makubwa zaidi. Katika kukabiliana na uhaba wa fursa za ajira, Serikali inashajiisha wananchi kujiunga katika vikundi vya Ushirika ili waweze kunufaika na huduma za mafunzo na mikopo iliyotayarishwa. Mkazo umewekwa katika kuvisaidia vikundi vya uzalishaji mali vinavyoanzishwa na vijana na wanawake ili waweze kujiajiri wenyewe, wajiongezee kipato na kupambana na umasikini.
Vile vile juhudi zinaendelea kufanywa kuwasaidia wakulima wetu ili waweze kujiongezea kipato. Sote tunaelewa kuwa kilimo kinatoa nafasi kubwa ya ajira hapa nchini. Kwa kuthamini mchango wa sekta hii, Serikali imeamua kuziimarisha shughuli za kilimo kwa kupunguza bei ya pembejeo za kilimo na huduma za matrekta. Maandalizi yameanza kwa kuwaajiri Mabibi na Mabwana Shamba wapya na kuimarisha miundombinu ikiwemo kuchimba visima vya umwagiliaji maji na kupeleka umeme kwenye mashamba. Azma ya Serikali ni kuongeza uzalishaji na kutoa ajira zaidi kwa wananchi kwenye sekta hii. Maandalizi, pia, yamefanywa katika kuimarisha shughuli za uvuvi na ufugaji ili nazo ziwe na tija na kuongeza ajira.
Ndugu wananchi,
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umetufunza kufanyiana ihsani, kupendana na kusaidiana. Hili ni jambo muhimu ambalo nalo ni vyema tukaliendeleza. Mwenyezi Mungu ametuumba katika hali tofauti. Kuna wenye uwezo na wasio nao, kuna watu wenye ulemavu na wazima wa kiwiliwili na kuna wazima wa afya na wagonjwa. Ni wajibu wetu kuwafikiria wenye matatizo mbali mbali na kuwasaidia. Wazee walituambia, Udugu ni kufaana siyo kufanana. Wenye uwezo wa mali wana wajibu wa kutoa zaka na sadaka, wazima tuwasaidie wagonjwa na wenye mahitaji mbali mbali wakiwemo wasiojiweza na mayatima. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumezishukuru neema alizotupa Mola wetu na tutarajie kupata radhi zake. Mwenyezi Mungu anatuambia katika Qur-an aya ya 83 ya Suratul Al Baqarah:
“Na (kumbukeni habari hii ) tulipochukua ahadi ya kizazi cha Israel (Mayahudi) tukawaambia kuwa “Hamtamuabudu yoyote (sasa) ila Mwenyezi Mungu, na muwafanyie wema wazazi na jamaa na mayatima na maskini na semeni na watu kwa wema na simamisheni sala na toweni zaka” kisha mkageuka isipokuwa wachache tu katika nyinyi (na hivi sasa pia ) nyinyi mnapuuza.
Nawashukuru na kuwapongeza wananchi na Taasisi zinazotoa misaada ya kijamii kwa watu mbali mbali. Nimefarajika sana na taarifa niliopewa ya Wizara ya Afya juu ya kuongezeka kwa mwamko wa watu wanaokwenda kutoa damu kwenye benki ya damu. Kitendo hiki ni cha kizalendo na cha kishujaa chenye lengo la kuokoa maisha ya wagonjwa wetu. Serikali inathamini sana mchango huo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awalipe malipo mema hapa duniani na huko akhera tuendako wale wote wanaojitolea na wafanyakazi wa afya wote wanaoshughulikia huduma hizo na zile zote tunazozihitaji kila siku.
Ndugu Wananchi,
Darsa mbali mbali zilizoendeshwa na Masheikh wetu katika mwezi tulioumaliza zimetusaidia sana kupanua uwezo wetu wa maarifa. Kwa msingi huu, tumeweza kujiongezea uwezo wa kupambanua mabaya na mazuri. Ni vyema kuitumia elimu hiyo kwa kuimarisha mwenendo wetu wa maisha sisi, watoto wetu na wengineo. Tujiepushe na vishawishi vinavyoweza kutuletea matatizo yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya na maambukizo ya virusi vya UKIMWI mambo ambayo yanaathiri sana kundi la vijana.
Tujitahidi kuwahimiza watoto wetu kutilia mkazo masomo yao. Wazazi turudishe utamaduni wetu wa zamani wa kushirikiana katika malezi ya watoto wetu. Tukumbuke maneno ya wahenga “Mwana wa mwenzio nawe ni mwanao pia”. Vile vile “Kidole kimoja hakivunji chawa.” Kwa hivyo lazima tushirikiane ili tupate vijana wazuri wenye nidhamu. Serikali inajitahidi kuandaa mazingira mazuri yatakayowezesha watoto wetu kupata elimu iliyo bora. Ujenzi wa Skuli mpya unaendelea na juhudi zinafanywa kuziimarisha ziliopo kwa kuzipatia samani, walimu, vitabu, na vifaa vya maabara kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu nchini. Wazazi tuna wajibu wa kuwashajihisha watoto wetu kuzitumia vyema fursa za elimu zilizopo.
Ndugu Wananchi,
Sikukuu ya Eid el Fitri ya mara hii inafanyika muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha mkutano wa Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2011/2012. Hivi sasa kila wizara imeshajipangia mipango yake ya kuwaletea maendeleo wananchi na imeshaidhinishiwa fedha. Hivi karibuni nilipata fursa ya kusikiliza vipaumbele vya kila Wizara kuanzia tarehe 10 Agosti hadi tarehe 27 Agosti 2011 ambapo Wizara hizo zilifika Ikulu na kuwasilisha mipango ya utekelezaji ya bajeti ya mwaka 2011/2012. Kama ilivyo kawaida kwa manufaa ya nchi yetu wananchi wote wataendelea kuiunga mkono mipango ya Serikali.
Kwa hakika ni jambo la faraja kuona jitihada zetu zinaungwa mkono na kupongezwa na wenzetu wengi. Kuna mataifa mengi yametuahidi kuendelea kushirikiana nasi kwenye juhudi zetu hizi. Kwa hivyo sisi wenyewe tunapaswa kuwa mbele, hasa kwa yale mambo yaliyo ndani ya uwezo wetu. Turudishe moyo wa kujitolea kwa kufanya shughuli na kazi zetu za kijamii. Ni wajibu kujitolea katika kuijenga nchi yetu, kwani Zanzibar itajengwa na Wazanzibari wenyewe lakini ni dhahir kuwa tutaungwa mkono na marafiki zetu mbali mbali.
Inatia moyo kuona kuwa uchumi wetu unaendelea kukua na kutupa matumaini ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maendeleo. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha hatua hii. Shukurani za kweli kwa Mola wetu ni kujitahidi kuyatumia vizuri mapato yetu hasa kwa yale mambo tuliyoyapa kipaumbele. Ni lazima tuchukue hadhari kwa matumizi ya mapato yetu ili kupunguza athari zinazoweza kutokea kufuatia mwelekeo wa kutokea mtikisiko wa uchumi duniani kama inavyoarifiwa na baadhi ya wachumi. Kidogo tunachopata kinaweza kutumika vizuri kufanya mambo ya msingi. Wahenga walisema, Kupanga ni kuchagua.
Napenda kuitumia nafasi hii kuwashukuru sana wakulima wetu wa karafuu kwa namna wanavyounga mkono juhudi za Serikali za kuinua uchumi wetu. Tunathamini sana kwa kuitiikia wito wa Serikali wa kuziuza karafuu kwenye Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC). Serikali imeshapanga mipango madhubuti ya kuliimarisha zao hili na kuwalipa wakulima bei nzuri kulingana na bei ya soko la dunia. Tunawanasihi sana wakulima waendeleze ushirikiano na Serikali katika kupambana na wafanya magendo ya karafuu kwa nguvu zote. Watu hao wanatudhulumu na hawatoi manufaa yo yote kwa Serikali wala wakulima. Natoa wito kwa wananchi wote kushiriki katika vita dhidi ya magendo ya karafuu kwani zao hili ndiyo muhimili mkuu wa uchumi wetu. Kwahivyo, ni wajibu wetu kuulinda.
Ndugu Wananchi,
Wakati tunasherehekea kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani, baadhi ya waumini wanajitayarisha kuitekeleza nguzo ya tano ya Kiislamu- HIJJA. Wenzetu hawa wameitikia wito wa Mola wetu aliyewataka wale wenye kutimiza masharti ya Hijja kwenda kuizuru nyumba tukufu - Makka Saudi Arabia. Tumuombe Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala awape matayarisho mema, awazidishie afya njema na ustahamilivu ili waweze kuitekeleza ibada hiyo kwa ufanisi. Mola awafikishe huko salama na awarudishe salama na aikubali ibada yao hiyo. Serikali kupitia Ofisi ya Wakfu na Mali ya Amana itashirikiana na Mahujaji wote kwa kila hatua.
Namalizia kwa kuwashukuru viongozi, mashekhe, wananchi na wale wote waliofanikisha hafla hii. Nawatakia Waislamu wote na Wananchi wote Sikukuu njema yenye kheri na Baraka. Matumaini yangu ni kwamba tutaendelea kusherehekea Sikukuu hii kwa amani na utulivu. Tukumbuke kuwa leo ni siku ya furaha, kwa hivyo sote ni haki yetu tufurahi, tutembeleane tujipambe na tule vizuri bila ya kufanya israfu. Tukifanya hivi tutakuwa tumedhihirisha maana halisi ya Sikukuu hii.
Mwisho, nachukua fursa hii kuwaasa waendeshaji wote wa vyombo vya barabarani vya moto na vyengine, wawe waangalifu, wazingatie na wazifate kanuni za usalama barabarani na wawajali watumiaji wengine wa barabara na waepuke kuyahatarisha maisha ya watumiaji hao; wakiwemo wazee, watu wenye ulemavu na watoto katika siku zote za sikukuu yetu. Maafisa wa Polisi wa Usalama barabarani wawe makini katika kuhakikisha usalama kwa watumiaji wote wa barabara ili kuepuka ajali.
Mwenyezi Mungu atupe kila la kheri na kutuzidishia neema. Atulinde na majanga yote ya dunia. Atuwezeshe kudumisha umoja, mshikamano, maelewano na amani ya kudumu nchini mwetu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aturehemu sisi na wenzetu wote waliotangulia mbele ya haki.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
IDD MUBARAK
WA KULLU AAM WAANTUM BIKHEIR
Ndio kwanza, nimeisoma kumbe ni bonge moja la hotuba! na kama itafanyiwa kazi inaweza ikatutowa.Mimi nadhani kuhsu suala la elimu,lisiishie tu kuwasomesha bali pia kuwaandaa vijana kisaikolojia wawe tayari kufanya kazi popote nje ya ZNZ.Muda mfupi ujao serekali haitaweza tena kukabiliana na wimbi la vijana wanao maliza vyuo hapa.Pia wazazi wahamasishwe kusomesha watoto wao nje ya zanzibar,mathalan,Tza bara, kenya,uganda etc.ili wapate exposure.Tukumbuke East Africa inakuja hiyo tutakuja kusema tunaonewa bure!watu ambao huwajui,hujawahi ku interact nao wala kufika kwao sijui utawezaje jujadiliana nao? yasije yakawa yale ya bungeni, ndugu zetu wenyewe(bara) tukisimama mbele yao tunaanza kutetemeka ujasiri wote unakwisha!Tusiishie tuu kupewa nafasi za kisiasa tujiandae,Rwanda wamepeleka vijana 2000 marekani kujiandaa na ajira za Afrika mashariki...mimi wa SUZA si wataninyanyapaa hawa?
ReplyDelete