SERIKALI ya Zanzibar, imesema imelazimika kutumia majengo ya mtu binafsi kwa ajili ya kutoa mafuzo kwa wanafunzi wa Chuo cha Fedha Chwaka, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na Chuo hicho.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi Mipango ya Maendeleo Omar Yussuf Mzee, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, Mohammed Said Mohammed Dimwa, aliyetaka kujua ni kwanini Wizara hiyo inayatumia majengo ya Skuli ya Glorious Academy, kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa chuo hicho na gharama inazotumia.
Akijibu hoja hiyo, Waziri huyo, alisema Zanzibar hivi sasa imekuwa inahitaji kupata wataalamu zaidi jambo ambalo limesababisha kufurika kwa wanafunzi katika chuo hicho, kiasi ambacho wamelazimika kukodi skuli hiyo.
Alisema walilazimika kuitumia skuli hiyo kutokana na kukidhi viwango vinavyotakiwa na Baraza la Mitihani Tanzania NECTA,kwa vile ni moja ya mambo waliyotakiwa kuzingatia na taasisi hiyo.
Alisema kabla ya kutumia majengo ya skuli hiyo Wizara hiyo, ilijaribu kuomba madarasa katika skuli ya Haile Selasie, lakini kwa bahati mbaya hayakuweza kutosha kutokana na kupewa darasa moja wakati mahitaji yao yalikuwa ni madarasa mawili.
Akiendelea kujibu suala hilo, Waziri huyo alisema, sababu nyengine ambayo iliwafanya kukodi madarasa hayo ni pamoja eneo la Chuo kuwa mbali na makaazi ya wanafunzi, jambo ambalo huwalazimu kutumia shilingi 2600 kwa siku, huku mabasi iliyonayo ni machakavu na yenye uwezo mdogo wa kubeba wanafunzi kwa vile huchukua watu 100.
Kutokana na hali hiyo, Waziri huyo alisema, walilazimika kuchukua wanafunzi wa Fani ya Ugavi kutokana na kuwapo mahitaji yao serikalini na isingependa kuwaacha wakati wakiwa tayari wamejitokeza kutaka kupatiwa masomo hayo.
Alisema katika majengo hayo ya mtu binafsi, skuli hiyo hivi sasa imekuwa ikiwapatia masomo wanafunzi 110 na mkataba waliofunga na mmiliki wa skuli hiyo utakuwa ni wa mwaka mmoja.
Alisema gharama ambazo Chuo cha Chwaka inatumia kwa ajili ya ukodishwaji wa madarasa hayo, ni shilingi milioni 26,000 kwa mwaka ikiwa ni sawa na wastani wa shilingi milioni 2,160.00 kwa mwezi .
Alisema Chuo hicho kimekuwa kinapata shilingi milioni 88 ikiwa ni malipo ya ada za wanafunzi na fedha za usajili ni shilingi 60.000 kwa wanafunzi 110 ambazo ni sawa na shilingi milioni 6,600,000 na mapato halisi kwa wanafunzi wanaosoma kwenye Chuo hicho ni shilingi milioni 94,600.
Haya wataalamu wote hao, halafu muwaongezee watu mikataba baada ya muda wao wa kustaafu!..
ReplyDeleteHalafu jamani,hichi chuo kwani kiko chini ya NECTA au NACTE ?