Habari za Punde

MAKUNDUCHI WAZIPOKEA SHEREHE ZA MARIDHIANO KWA SHANGWE



Na Aboud Mahmoud

NGOMA ya Mpe Chungu kutoka katika kijiji cha Mzuri Makunduchi,ambayo kwa takriban miaka saba sasa imetoweka katika macho wa wanakijiji hao,imeonekana kuvuta mashabiki wengi katika mradi wa 100% Zanzibari maarufu kwa jina la 'Shangiria Maridhiano'.

Katika mradi huo ambao limeandaliwa na Taasisi ya Swahili Perfomance Art Centre na kudhaminiwa na Ubalozi wa Norway na Kampuni ya simu ya Zantel lilifanyika katika uwanja wa Jamhuri Makunduchi.


Ngoma hiyo ya Mpe chungu ilionekana kuvutia wengi hasa wananchi wa kijiji hicho kutokana na uchezaji wa ngoma hiyo huku wakitumia lahaja ya ambayo ndio inayozungumza kijiji hapo.

Mashabiki na wapenda burudani ya muziki wa kijiji cha Makunduchi walionekana kuvutiwa sana huku wengine wakishindwa kustahamili na kuanza kuserebuka uwanjani hapo.

Aidha kikundi cha taarab cha Maendeleo Music Taarab kuotaka Pemba, ambao ndiyo walikuwa wageni katika onesho hilo la Makunduchi, nacho kiliamshia hisia za hadhira waliofika katika eneo hilo hasa pale walipoanza kuimba nyimbo zao maarufu ikiwemo Zao la karafuu.

Pia nyimbo ya Lulu, Mgomba na Kitandawali zilizoneka kuvutia hadhira hiyo kutokana na umaarufu wa nyimbo hizo katika masikio na midomo ya wananchi wengi wanaopenda taarab.

Katika fani ya maigizo nayo haikuwa nyuma ambapo kambi ya wasanii hao kutoka kisiwani Pemba wakiongozwa na msanii maarufu, Khamis Nyange Makame 'Profesa Gogo' na wa kijiji cha Makunduchi ilifanikiwa kuteka nyoyo za mashabiki hao hasa pale wasanii hao walipoonyesha onesho lenye kuelezea kero zinazowakabili wananchi

Akizungumza na wananchi waliohudhuria katika muendelezo wa tamasha hilo,Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Mzee Haji Makungu Mgongo,amewataka wananchi wa kijiji hicho kuendelea kuyadumisha maridhiano hasa katika upande wa ngoma za utamaduni.

Amesema kuwa kuyaendeleza maridhiano yaliofikiwa na viongozi wa nchi ni kupata maendeleo mbali mbali ikiwemo kuitangaza sanaa na utamaduni wa nchi.

Mradi wa 100% Zanzibar 'Shangiria Maridhiano' wiki hii linatarajiwa kuhamia katika kijiji cha Kangagani kisiwani pemba ambapo wasanii mchanganyiko wa Taarab kutoka Pemba na Unguja watafanya kamb ya kisanii kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 25 hadi 29 Oktoba. Onesho la wiki hii litafanyika katika Uwanja wa skuli ya Kangagani siku ya Jumamosi tarehe 29 Oktoba.

1 comment:

  1. Inabidi tu, ndugu zangu tusome alama za nyakati.
    Inaeleweka kua 'haya mambo' kae hatuyataki lkn.tutafanyaje? na wenzetu wameshayakubali.si tutakuja kutengwa bure!..au jee?

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.