Habari za Punde

ZFA YAPATA 40% UDHAMINI LIGI KUU

Na Salum Vuai, Maelezo

MBIO za Chama cha Soka Zanzibar kutafuta wadhamini wa ligi kuu ya mwaka 2011/12, zimefanikiwa kupata asilimia 40 ya udhamini huo.

Hayo yamethibitishwa na Msaidizi Katibu wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Masoud Attai, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho hoteli ya Bwawani juzi.


Akijibu masuala ya waandishi hao waliotaka kufahanu mwelekeo wa ligi hiyo iliyochelewa kuanza kutokana na Umoja wa Klabu kushikilia msimamo wa kutocheza bila udhamini, Attai alisema kumejtokeza taasisi iliyo tayari kubeba gharama za usafiri wa timu kwenda katika vituo vya michezo yao.

Hata hivyo, hakuwa tayari kuitaja taasisi hiyo, akidai kuwa bado mazungumzo kati yake na chama hicho hayajafikia hatua ya kutiwa saini, na kwamba kuitaja kwa sasa, itakuwa sawa na kuuharibu mchuzi.

"Kimsingi tumepata udhamini wa usafiri kwa timu zitakazocheza ligi kuu, lakini siwezi kuitaja sasa mpaka pale tutakapokuwa tumetiliana saini makubaliano kikamilifu", alisema.

Kuhusu gharama nyengine za ushiriki wa klabu katika ligi hiyo ikiwemo zawadi, Attai alifahamisa kuwa, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan, amewaahidi kuwa analifanyia kazi, na kwamba upo mwelekeo kuwa atafanikiwa.

"Baada ya ZFA kupata udhamni kwa asilimia 40, Waziri Jihad amejitolea kuhangaikia sehemu iliyobaki, ili ligi yetu iweze kuanza, na zipo taarifa kwamba tamaa ya kufanikiwa ni kubwa", alieleza Msaidizi Katibu huyo.

Alipoulizwa iwapo chama chake hakihofii kuachwa nyuma na kalenda ya kimataifa iliyokusudia kuanza kuifuata msimu huu, Attai alijibu kuwa si lazima kwenda sambamba na kalenda hiyo kwa asilimia 100, kwani nchi za ng'ambo na Zanzibar hazilingani kijiografia.

Wakati huohuo, timu ya soka inayoundwa na wachezaji wa zamani kutoka nchini Uswisi, imewasili Zanzibar jana kwa boti ya Kilimanjaro, na kupokelewa bandarini na viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).

Wakongwe hao watakaokuwa nchini kwa ziara ya wiki mbili itakayojumuisha michezo kadhaa, pamoja na kutembelea maeneo ya kihistoria, leo saa 10:00 jioni itakuwa na mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan, katika ukumbi wa VIP hoteli ya Bwawani.

1 comment:

  1. Mimi, nadhani wakati umefika kwa taasisi za kibiashara za z'bar kuchangia shughuli za michezo badala ya kuona hawana wajibu huo. hebu tujiulize Zantel na PBZ wanashindwa nini kudhamini kaligi kadogo kama hako! wakati wao ndio wanao 'dominate' biashara za mawasiliano na fedha! Watu hapa wamekaa kama waliorogwa kimawasiliano, karibia wote Zantel! kila unaemuliza Account, PBZ! na yenyewe ilikua mwisho chumbe siku hizi kidogo wamefika DAR. Mm nadhani tutumie mtindo wa 'nipe nikupe'

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.