Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Zanzibar (TASWA-ZANZIBAR), kimeelezea kusikitishwa kwake na vifo vya wanahabari wakongwe Halima Mchuka na John Ngahyoma vilivyotokea ndani ya siku mbili.
Marehemu Halima Mchuka aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), alifariki juzi baada ya kuugua ghafla ugonjwa wa kiharusi, wakati Ngahyoma ambaye alikuwa mtangazaji wa BBC Tanzania, aliaga dunia jana asubuhi jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa TASWA-ZANZIBAR Mwinyimvua Abdi Nzukwi, alisema chama chake kimeshtushwa na misiba hiyo, huku akimtaja marehemu Mchuka kuwa ameacha rikodi ya kuwa mtangazaji wa kwanza mwanamke kutangaza mpira wa miguu Afrika Mashariki.
"Kwa kuwa tangu wakati huo, bado hatujasikia mtangazaji mwengine wa kike kufuata nyayo za marehemu Halima, tunaweza kusema amekufa huku rikodi aliyoiweka ikiwa haijafikiwa wala kuvunjwa", alifafanua.
"Mbali na kuwa mtangazaji, Halima alidhihirisha kuwa ni mwanamichezo aliyeifahamu vyema kazi yake, na ni vyema wanahabari wanaochipukia sasa waige mfano wa kujituma wa mwanahabari huyo", alishauri Nzukwi.
Aidha alimuelezea Ngahyoma kuwa mmoja wa watangazaji waliowasaidia wanahabari vijana, hasa alipohamishiwa Zanzibar, ambapo alishirikiana vyema na waandishi wa hapa.
Alitoa salamu za pole kwa familia za marehemu hao, pamoja na mashirika waliyokuwa wakiyatumikia, na kuwataka wawe na subira katika kipindi hichi kigumu, huku akimuomba Mwenyezi Mungu awape makaazi mema.
No comments:
Post a Comment