Na Abdi Shamnah
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeshauriwa kuelekeza nguvu zake katika uimarishaji wa michezo midogo midogo ilioanza kupata mafanikio ili kuliletea sifa Taifa.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha NLD Ahmeid Rashid ‘Joe’ na Katibu Mwenenzi wa Chama hicho, Nassor Mbarouk, wakati walipokuwa na mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdillah Jihad Hassan, ofisini kwake Kikwajuni.
Viongozi hao wamesema kuwa wakati umefika kwa Serikali kuelekeza nguvu zake na kutoa msukumo wa dhati, ikiwemo wataalamu na v
Walisema matokeo ya hivi karibuni ya kijana Ahmad Bakar, mlemavu wa akili alieiletea Tanzania Medali ya Dhahabu katika michuano iliofanyika Athern Ugiriki, ushindi wa timu ya Wanyanyua vitu vizito nchini Uganda pamoja na ule wa Judo katika michuano ya Afrika Mashariki iliofanyika jiji Dar es Salaam, ni kielelezo tosha kuwa iwapo michezo hiyo itapewa msukumo, mafanikio makubwa yaweza kupatikana katika kipindi kifupi kijacho.
Wakizungumzia uhai wa mchezo wa kunyanyua vitu vizito, wanasiasa hao walimuomba Waziri Jihad kutembelea eneo lao la mazoezi na kufanya jitihada za dhati kuliimarisha jengo lao pamoja na kupatiwa vifaa vinavyohitajika.
Aidha walimuomba Waziri huyo kupitia Wizara yake kufanya kila linalowezekana kuona vijana hao wanapata mtaalamu wa kuendeleza kituo hicho, ambapo pia hutumiwa na watu mbali mbali kwa mazoezi, wakiwemo wagonjwa wa maradhi ya baridi.
Katika hatua nyingine wakongwe hao wa siasa waliiomba Serikali kufanya juhudi ili Wajasiarimali wa Zanzibar waweze kupata fursa kikamilifu ya kuyatumia maeneo ya Mji Mkongwe na Bandarini kwa ajili ya kuendesha biashara zao zinazoendana na utamaduni wa Kizanzibari.
Walisema hali ilivyo hivi sasa, ni ya kusikitisha kwani bidhaa zinazouzwa kwa watalii katika maeneo hayo ni zile zenye asili na tamaduni kutoka nje, ikiwemo vinyago.
Walisema Serikali inasisistiza uanzishaji wa vikundi vya ushirika kwa wajasiriamali wazalendo, ili waweze kujiendesha kupitia biashara zao, hivyo hatua ya kuwanyima maeneo hayo ni kuwafanya washindwe kufikia lengo la kujitegemea
Aidha waliiomba Wizara hiyo yenye dhamana na Utamaduni kusimamia kikamilifu maadili katika nyanja mbali mbali ikiwemo katika sanaa, kwa kigezo kuwa yamekuwa yakiporomoka kadri siku zinavyosonga.
Nae Waziri Jihad alieleza azma ya kuendeleza mashirikiano yaliopo na uongozi wa Chama cha Wanyanyua vitu vizito kupitia BTMZ kwa dhamira ya kuendeleza mchezo huo.
Akizungumzia suala la wajasiariamali wa Zanzibar kupata fursa ya kuendesha biashara zenye asili na utamaduni wa Zanzibar, alisema tayari Wizara yake imeanza kuchukua hatua, huku akiahidi mikakati kabambe kuandaliwa kukabiliana na mporomoko wa maadili.
No comments:
Post a Comment