BAADA ya kuhukumiwa adhabu ya kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi 18 kwa makosa ya kuchoma moto msahafu pamoja na juzuu za dini ya Kiisilamu, hatimae kijana, Ramadhan Handa Tuma atembea kifua mbele mitaani.
Ramadhan ambaye ni mkaazi wa Mombasa wilaya ya Magharibi Unguja, amepata faraja hiyo baada ya kumaliza adhabu iliyotolewa na mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe Fubuari 21 mwaka jana.
Habari za uhakika zilizopatikana kutoka Vyuo vya Mafunzo Kilimani Mjini Unguja, pamoja na kupatikana kwake kwa tarehe aliyomaliza adhabu hiyo, lakini Ramadhan tayari ameshaachiliwa kutoka kizuizini Chuoni humo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Wakati akiwa anatumikia Chuo hicho, Ramadhan aliwasilisha rufaa ya kupinga hukumu na adhabu iliyotolewa na mahakama hiyo ya wilaya iliyokuwa chini ya hakimu Khamis Ali Simai, ambaye hivi sasa ni hakimu wa mahakama ya mkoa Mwera.
Ramadhan alishitakiwa kwa kosa la kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani chini ya kifungu cha 74 (1) (b) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, kwa kuchoma msahafu pamoja na juzuu za dini ya Kiisilamu shitaka ambalo alikuhumiwa kutumikia Chuo cha Mafunzo wa miezi sita baada ya kushindwa kulipa faini ya shilingi 200,000.
Sambamba na adhabu hiyo, pia alihukumiwa kutumikia Chuo hicho kwa muda wa miezi 18 kwa kosa la kuikashifu dini ya Kiisilamu, kwa kuchoma moto vitabu hivyo kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 117 na 27 cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Rufaa hiyo nambari 4/2011 kutoka katika kesi ya jinai nambari 432/2010, ameiwasilisha mahakamani hapo tokea Oktoba 10 mwaka jana, mbele ya hakimu Nassor Ali Salim wa mahakama ya mkoa Vuga, lakini imeshindwa kusikilizwa kwa vipindi viwili tofauti baada ya mkata rufaa huyo kushindwa kufika mahakamani hapo.
Hivyo, rufaa hiyo imeahirishwa kwa mara nyengine tena na inatarajiwa kufikishwa tena mahakamani Mei 21 mwaka huu.
Katika kesi ya msingi Ramadhan alitiwa hatiani na mahakama hiyo ya wilaya chini ya kifungu cha 219 cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar, baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka uliowasilishwa mahakamani hapo.
Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 18, 2010, na kwa muda wote huo hadi kutolewa kwa hukumu hiyo mshitakiwa huyo alikuwa rumande kwa kile kilichoelezwa kwa usalama wa maisha yake.
Siku hiyo ilifahamishwa kuwa, mahala hadharani kwa makusudi Ramadhan alitenda makosa yote hayo katika maeneo ya Mombasa, wilaya ya Magharibi Unguja majira ya saa 2:30 za usiku wa Novemba 16 mwaka jana.
Mtuhumiwa Dawa za Kulevya Rumande kwa Kushindwa Dhamana
Na Husna Sheha.
MTU mmoja (40) Mkaazi wa Bumbwini Mjawiri Kaskazini unguja amefikishwa mahakama ya Mkoa Mfenesini akikabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la kupatikana na dawa za kulevya aina ya heroin na bangi.
Ilidaiwa mahakamani na mwendesha mashitaka Ali Rajab, mwanasheria wa serekali kuwa mshitakiwa huyo, Said Mansuri Said alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) Na 9 /2009 sheria za Zanzibar, Aprili 12, 2012.
Ilidaiwa kuwa majira ya saa 3:30 asubuhi mtuhumiwa huyo alipatikana na kete 89 za unga aina ya hiroin zenye uzito wa gramu 0.10 mbele ya hakimu Makame Mgeni Simshamba.Aidha hati hiyo ilidaiwa kwamba April 12 mwaka huu majira ya saa 3:30 asubuhi huko Fujoni Nyumba ya Ndege wilaya ya Kaskazini B unguja.
Mtuhumiwa huyo inadaiwa pia alipatikana na nyongo 20 za Bangi zanye uzito wa gramu 0.20 gram, katika eneo hilo hilo la Fujoni Nyumba ya Ndege.
Baada ya kusomewa mashitaka yake mbele ya hakimu Makame alikana na kuiomba mahakama impatie dhamana kwa sababu ni mgonjwa wa vidonda vya tumbo, na familia yake inaongozwa na watu wazima ambao anapaswa kuwahudumia.
Upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Hivyo mahakama imempeleka rumande hadi April 30 kesi hiyo itakapotajwa tena kwa kushindwa kutimiz masharti ya dhamana.
Bakari Juma Mzee kizimbani tuhuma wizi baada ya kuaminiwa
Na Rehema Abdulrahman, MCC
BAKARI Juma Mzee (44) mkaazi wa Uzi Mwanakwerekwe Unguja, amefikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe kwa kosa la wizi baada ya kuaminiwa.
Mtuhumiwa anakabiliwa na kosa hilo ambalo ni kinyume na kifungu cha 267 (1) na 274 (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004, ikiwa ni sheria za Zanzibar.
Kesi hiyo ambayo ilisomwa na mwendesha mashitaka Maulid Ame kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka mbele ya hakimu Valentin Andrew Katema wa mahakama hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka ilidaiwa kuwa mtuhumiwa aliaminiwa kwa kupewa vespa na Haji Wazir Haji, kwa madhumuni ya kufanyabiashara yake halafu airejeshe kwa mwenyewe.
Vespa hiyo ambayo ni aina ya Bajaji yenye namba za usajili ZNZ 5654, ikiwa na thamani ya shilingi 650,000, mtuhumiwa huyo haku irejesha tena kwa mmiliki wake.
Mwendesha mashitaka alidai kuwa miaka mitatu iliyopita katika maeneo ya Nyerere mjini Magharibi Unguja, mtuhumiwa alipewa vespa hiyo kwa kufanyiabiashara zake halafu amrejeshee mwenyewe
Kutokana na madai hayo kutoka kwa mwendesha mashitaka mtuhumiwa huyo alipotakiwa kueleza chochote kuhusiana na madai hayo alikataa kosa mbele ya hakimu wa mahakama hiyo.
Hakimu Valentin, aliamuru mtuhumiwa apelekwe rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana.
Wadhamini hao ambao watatakiwa kufika mahakamani hapo siku ya kuendeshwa tena kesi hiyo, ambapo watatakiwa kufika mahakamani na barua za sheha pamoja na kopi ya vitambulisho vya uzanzibari ukaazi.
Baada ya maamuzi hayo, hakimu huyo ameiahirisha kesi hiyo hadi Mei 4, 2012, ili kuupa muda upande wa mashitaka kuendelea na upelelezi wa shauri hilo.
Mtuhumiwa Akiri Kumshambulia Mwenzake
Na Madina Issa
MARYAM Mjaka Haji (24) mkaazi wa Nyerere amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za shambulio la kuumiza mwili.
Ilidaiwa mahakamani na mwendesha mashitaka Ali Talib mbele ya hakim Maisara Abdalla Maisara kuwa mshitakiwa amemshambulia kwa kumuumiza mwili Maryam Mfaume Abdallah mkaazi wa Nyerere kwa kumumiza kichwa.
Hati hiyo, ilidai kuwa Februari 21 saa 12:30 jioni katika maeneo ya Nyerere, Wilaya ya Mjini mshitakiwa Maryam Mjaka Haji alimshambulia kwa makusudi bila ya halali, Maryam Mfaume Abdallah kwa kumsukuma na kuanguka chini na kuumia sehemu ya kichwa na kupata maumivu ya kichwa na maumivu mwilini.
Ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa kesi hiyo kuwa mtuhumiwa amefanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 247 cha kanuni ya adhabu sheria namba 6/04 ya Zanzibar.
Kwa upande wake, mtuhumiwa alikiri kosa mbele ya hakim Maisara na kuiomba mahakama impatie dhamana.
Mtuhumiwa huyo amepatiwa dhamana ya mtu mmoja na kesi yake itatajwa tena April 25 mwaka huu.
Mkaazi wa Shakani Korokoroni kwa Madai ya Wizi
Na Khamisuu Abdallah
MKAAZI wa Shakani Unguja, Juma Mussa Kasumbi (25) amepandishwa mahakamani kwa tuhuma za makosa mawili tofauti.
Ilidaiwa mahakamani na mwendesha mashitaka Muhammed Kassim mbele ya hakimu Muhammed Ali Muhammed kuwa mshitakiwa aalidaiwa kuvunja nyumba na kuiba katika nyumba kuishi ya Aisha Benard Kidala kwa dhamira ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 297 (1) (a) (2) cha sheria Na 6/2004 sheria ya Zanzibar.
Katika shitaka la pili ilidaiwa kuwa mtuhumiwa aliiba kanga pea mbili buibui na vitu vyengine kadha vya ndani vikiwa na thamani ya
150,000 mali ya Aisha Benard Kidala.
Kosa hilo linakwenda kinyume na kifungu 267(1) na 274(1) cha sheria Na 6/2004 sheria ya Zanzibar.
Kwa upande wake, mtuhumiwa apinga tuhuma hizo na kuiomba mahakama impatie dhamana ambapo hakimu Mohammed Ali alimkublia kwa sharti la kuwasilisha wadhamini wawili na kila mmoja awasilishe saini bondi ya shilingi 50,000 barua ya Sheha na kitambulisho cha Mzanzibari.
Shauri hilo limesogezwa mbele hadi Mei 2, 2012.
No comments:
Post a Comment