Na Joseph Ngilisho, Arusha
MWANARIADHA Fabian Joseph (27), amevunja rekodi ya mwaka jana kwa kuibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya riadha ya nusu marathoni ya Ngorongoro.
Katika mfukuzano huo uliofanyika Wilaya ya Karatu, Fabian Joseph aliwaweka nyuma na kuwashinda washiriki 107 waliochuana katika mbio hizo za kilomita 21, zilizodhaminiwa na kampuni ya simu Tigo na kuandaliwa na taasisi ya Zara Charity.
Mkimbiaji huyo alitumia saa moja, dakika tatu na sekunde 47, akivunja rekodi ya mwaka jana ambapo katika mbio hizo alitumia muda wa saa 1:04:35.
Mshindi wa pili alikuwa Martin Sulle (29) aliyetumia saa 1:04:26, ambaye aliwahi kuwa mshindi wa mashindano ya Afrika mwaka 2008, akifuatiwa na Stephano Huche (21), ambaye alikimbia kwa saa 1:04:30.
Kwa upande wa wanawake, mshindi wa kwanza alikuwa ni Jackline Sakilu (25) aliyetumia muda wa saa 1:16:01, akifuatiwa na mkongwe wa mashindano ya riadha nchini, Restituta Joseph (39), aliyekimbia kwa saa 1:18:21, na Siata Romanus, saa 1:20:30.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mashindano hayo, mratibu wa promosheni wa kampuni ya Tigo Edward Shilla, alisema kampuni yake kwa zaidi ya miaka mitatu imekuwa mdhamini mkuu wa mashindano hayo yenye lengo la kupambana na kutokomeza ugonjwa hatari wa malaria nchini.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwarejeshea wananchi faida kidogo inayopatikana pamoja na kuibua vipaji vya vijana kwa ili wamudu kushiriki michuano ya kitaifa na kimataifa ikiwemo Olimpiki nchini Uingereza.
Washindi wa mashindano hayo walizawadiwa medali na fedha taslimu kati ya shilingi laki moja na laki tano.
No comments:
Post a Comment