Habari za Punde

Mabingwa wa NSSF, Timu za Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zalakiwa kwa Shangwe

Na Faki Mjaka-Maelezo 

Timu za Wizara ya Habari,Utamaduni,Utalii na Michezo, Habari Sports na Habari Queen, ambazo zilishinda michuano ya Kombe la NSSF jijini Dar es Salaam zimewasili leo Zanzibar na kupata mapokezi ya aina yake ambayo yaliongozwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Bi Hindi Hamad Khamisi.

Mara baada ya kuwasili bandarini Zanzibar vikosi hivyo vililakiwa kwa ngoma aina ya Boso ambapo wachezaji wa timu hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa Wizara hiyo walishiriki kusakata burudani hiyo ya ushindi.

Katika mchezo wa fainali kwa upande wa soka timu ya Habari Spots ilifanikiwa kuwatandika wenyeji wa michuano hiyo timu ya NSSF kwa jumla ya mabao 4-0 katika uwanja wa Sigara-Chang’ombe ambapo kwa upande wa netiboli Habari Queen waliwabanjua kinadada wa TBC kwa magoli 30-10

Akielezea siri ya mafanikio ya ushindi huo Kocha wa Habari Queen Amina Kapenta amesema ushindi wao ulitokana na juhudi na matayarisho ya muda mrefu ambayo waliyafanya kabla na wakati wa mashindano hayo.

Kwa upande wa Soka, Mwenyekiti wa timu hiyo Issa Ahmada amesema nidhamu ya wachezaji na moyo wa kujituma ndiyo iliyokuwa silaha pekee ya kuweza kupata ushindi huo wa kishindo

NSSF ilianzisha mashindano hayo tokea mwaka 2004 ikiwa ni mwaka wa tisa hivi sasa na imepanga kuyaboresha zaidi mashindano hayo kwa kuyafanyia katika mikoa mbali mbali ambapo kuna wanachama wake.

Huu ni mwaka wa pili mfululizo kwa timu ya Habari Queen kunyakua kombe la NSSF ambapo kaka zao Habari Sports ni mara yao ya kwanza kuchukua Kombe hilo tokea kuanza kushiriki.

Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar 2/04/2012



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.