WATUHUMIWA waliokamatwa wakiingiza mifuko ya plastiki Zanzibar wameachiwa huru, baada ya Mkurugenzi wa mashitaka kuwabaini hawana makosa yanayoweza kuwabana kutokana na mifuko hiyo kukutwa wakiwa baharini.
Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Alhabib Fereji, aliyasema hayo Barazani jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea.
Mwakilishi Mbarouk Mussa Mtando, alitaka kujua ni hatua zipi walizochukuliwa watu hao baada ya kukamatwa na mifuko hiyo ilipelekwa wapi.
Waziri Fatma, alisema ni kweli askari wa KMKM walifanikiwa kuwakamata mabaharia 19 waliokuwa wakiingiza mifuko katika kisiwa cha Bawe, lakini wameachiwa huru kutokana na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kutowaona na makosa kwa vile walikamatwa bado wakiwa baharini.
Alisema mabaharia hao walikamatwa wakiwa na mapolo 426 ya mifuko iliyopigwa marufuku katika eno hilo na mabaharia wengine walikamatwa wakiwa na mapolo 281 ya mifuko ya plastiki katika eneo la Ras Shangani.
Alisema baada ya watu hao kukamatwa walipelekwa kwa Muendesha Mashitaka lakini walionekana hawana kosa kwa mujibuwa sheria.
Akitoa sababu za kutofunguliwa mashitaka watu hao alisema ni kutokana na kosa hilo kushindwa kuthibitika kutokana na eneo walilokutwa likiwa bado ni sehemu ya baharini na bado walikuwa hawajashusha mifuko hiyo Zanzibar.
Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa Mashitaka alieleza kuwa katika matukio hayo bado kulikuwa hakuna kosa kwa vile mifuko hiyo haijawahi kushushwa Zanzibar.
Alisema ili kosa lingeweza kutokea kwa mujibu wa sheria ilitakiwa kama mabaharia hao wangelikamatwa wakiwa na nyaraka za kuingiza mzigo nchini, ama kuingiza mzigo huo Zanzibar.
No comments:
Post a Comment