HOTELI ya Zanzibar Ocean View iliyopo Kilimani mjini hapa, imevunja na kuubomoa mkahawa iliyoujenga kinyume na sheria pembezoni mwa ufukwe wa bahari.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kuvunjwa kwa mkahawa huo kumekuja ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kufuatia kutolewa kwa ripoti ya kamati teule ya Baraza la Wawakilishi, ambayo ilielezea kwa kina ukiukwaji wa sheria unaofanywa na wawekezaji wa miradi ya hoteli za kitalii.
Ripoti hiyo ilizitaja hoteli kadhaa zilizopo katika visiwa vya Unguja na Pemba ambazo ujenzi wake umekiuka sheria kwa kujengwa ufukweni, huku kamati hiyo ikiibuka na mpendekezo kadhaa.
Pamoja na Meneja Mkuu wa hoteli hiyo Gilbert Kazungu kushindwa kuliweka wazi gazeti hili kuwa hatua hiyo ni kufuata maagizo ya kamati teule ya Baraza, lakini alisema hoteli imeamua kuvunja mkahawa huo uliokuwa ukijulikana kwa jina la Vero kutokana na kuwepo malalamiko kutoka kwa vyombo husika.
Maneja huyo alisema kutokana na malalamiko hayo, mmiliki wa hoteli hiyo Amani Ibrahim Makungu, amekubali uvunje, ikiwa ni kuitikia wito wa serikali juu ya kufuatwa kwa sheria zinazokwenda kinyume na ujenzi ufukweni.
"Mmiliki wa hoteli ameamua tuuvunje kwa kuelewa kuwa hakuna aliye juu ya sheria, alisema tumevunja sheria ya mazingira hakuna budi kuuvunja mkahawa huu bila ya kujali hasara tutakayopata kwa hatua tunayoichukua", alisema Meneja huyo.
Alifahamisha kuwa mkahawa wa Vero, ulijengwa mwaka mmoja na nusu uliopita kwa gharanma za shilingi milioni 7.5 kwa lengo la kuongeza eneo la kupata huduma ya chakula kwa wateja pamoja na wateja wa hoteli hiyo kupata mandhari nzuri ya bahari.
Hata hivyo meneja huyo alijitetea kuwa kujengwa kwenye ufukwe haikuwa na lengo la kuvunja makusudi sheria, ila walilenga kupanua wigo wa biashara hasa ikizingatiwa kuwa hoteli nyingi zilizopo Zanzibar tayari zimeshafanya ujenzi kama huo.
Kazungu alilamika kuwa lazima hoteli zote zilizovunja sheria ya ujenzi ufukweni ziwajibike kama ilivyowajibika hoteli yake na isiwe miradi ya wazawa tu ndiyo inayopewa shindikizo huku miradi ya wageni ikiachwa iendelee kuvunja sheria.
Katika ripoti ya kamati teule, hoteli ya Zanzibar Ocean View ilitajwa kama miongoni mwa zile zilizokiuka ujenzi kwa kujengwa ufukweni mwa bahari.
“Kuna uvamizi mkubwa wa maeneo ya fukwe na uharibifu wa mazingira na kamati imejiridhisha kwamba, ujenzi wa miradi ya mahoteli Zanzibar hauzingatii matakwa ya sheria zinazoelekeza juu ya masuala ya ardhi na mazingira”, ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.
Miongoni mwa mapendekezo ya kamati hiyo ni kutaka hatua za kisheria zichukuliwe kwa dhidi ya wawekezaji waliojenga kwa kukiuka sheria ya mazingira.
Afadhali serikali onaonesha kidogo msimamo madhbut...ila isiishie hapo tu, kuna wala rushwa aidha ya pesa au ngono...kwa hili heko serikali
ReplyDelete