Habari za Punde

Mama Asha Atembelea Soba House Pemba

 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mama Asha Suleiman  Iddi akizungumza na Vijana wanaobadilishwa tabia katika Nyumba ya Kubadilisha Tabia iliyopo Mkorosoni Chake Chake Pemba.
 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akikabidhi magodoro  kwa Vijana wa Soba House  katika Nyumba yaoi liyopo Mkoroshoni chake chake Kisiwani Pemba.                                                                                                                                                                           Mama Asha amefanya ziara  ya kuwatembelea Vijana hao akiambatana na Ujumbe wa Umoja wa Wake wa Wawakilishi na Wabunge  wa CCM ulio chini ya  Uenyekiti wa  Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwena Shein.    
 

Mama Asha Suleiman Iddi akiwakabidhi Viongozi wa Soba House Chakula na Vifaa vya Michezo Vikiwemo Viti  baada ya kuwatembelea Vijana hao kwenye nyumba yao ya kubadilisha tabia iliyopo Mkoroshoni Chake chake Pemba.   



Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi amewanasihi Vijana wanaoishi katika Nyumba za kubadilisha tabia { Soba House } kuwa walimu kwa Vijana wenzao wakati wanaporejea katika maisha yao ya kawaida ili kusaidia Jamii hasa Vijana kuepuka kujiingiza katika vitendo viovu.      
                                                                                                                                   
Mama Asha alieleza hayo wakati akizungumza na Vijana hao waliopo katika nyumba ya kubadilisha tabia iliyopo Mtaa wa Mkoroshoni Chake Chake Kisiwani Pemba. 
                                                                                                                                                        
Ziara ya Mama Asha iliyojumuisha pia Wake wa Wawakilishi na Wabunge wa CCM unaounda Umoja wa Wake wa Viongozi unaoongozwa na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Sheni ilienda sambamba na kukabidhi   zawadi za  Magodoro, Vyakula, Mafuta ya kupikia pamoja na Viti kwa Vijana hao hapo Soba House Mkoroshoni Chake Chake Pemba.    
                                                                          


Mama Asha alisema  matatizo ya Dawa za kulevya yanayopelekea maambukizi ya Virusi vya Ukimwi yanauma na kuleta uchungu mkubwa ndani ya Jamii.                                            

Alisema mapenzi kwa Familia hupungua au kutoweka kabisa inapotokea Kijana wao amejiingiza katika janga la dawa za kulevya.                                                                           

“ Mzazi anapata furaha na faraja pale anapotoa  mafunzo na malezi kwa Mtoto wake na  yakatekelezwa vizuri katika misingi ya maadili”. Alisisitiza Mama Asha Suleiman Iddi.                                                                                                                                        

Alifahamisha kwamba Serikali kupitia Taasisi zake pamoja na Jumuiya za 
Kiraia bado zinathamini Vijana hao kwa vile wao ni sehemu ya Jamii.                                                     

Mama Asha aliwataka Vijana wote Nchini hasa wale wanaotumia dawa za kulevya kuachana na anasa hiyo mbaya kwa kuwasusia wauzaji wa Biashara hiyo.                                                                                                                                                             

“Mkifanya mgomo baridi kwa kutotumia dawa za kulevya wauzaji wa bidhaa hiyo watashindwa kuendeleza biashara hiyo. Na hiyo ndio kampeni pekee ya kupambana na mchezo huo mchafu katika Nchi yetu”. Alifafanua Mama Asha.                                                      

Katika risala yao Vijana hao wa Nyumba ya kubadilisha Tabia Chake Chake Pemba wameelezea faraja yao kutokana na Vituo vyao kumtabulika Kitaifa na Kimataifa.                                                                                                                                               

Walisema yapo mabadiliko makubwa kwa Vijana wanaopitia Nyumba za kubadilisha Tabia.                                                                                                                                       

Hata hivyo bado wamekuwa wakikabiliwa na Changamoto nyingi ikiwemo fedha kwa ajili ya huduma pamoja na maeneo ya Michezo.                                                   

Wameiomba Serikali kuandaa Mipango madhubuti ya kuwajengea mazingira bora ya mafunzo ya Amali kwa ajili ya kujiajiri wenyewe jambo ambalo litawanyima muda wa kujiingiza tena katika janga la Matumizi ya Dawa za kulevya.                                                                                                                                                         

Akipokea msaada wa vyakula na Vifaa hivyo msimamizi wa Nyumba za kurekebisha Tabia Pemba Bwana Abdull Wahid alisema msaada huo ni chachu ya kupunguza  matatizo yanayozikabili nyumba hizo.                                                                          

Bwana Abdull Wahid alimshukuru Mama Asha  pamoja na Wanachama wa Umoja wao kwa msaada huo ambao utatumika kwa lengo lililokusudiwa.                            

Msaada huo wenye thamani ya Shilingi Milioni mbili {2,000,000/- } umejumuisha Mchele, Mafuta ya Kupikia, Sabuni, Magodoro pamoja na Viti kwa ajili ya matumizi ya Ofisi.


Othman Khamis Ame                                                                                                                         Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar                                                                                    

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.