Na Thompson Mpanji, MBEYA
ALIYEKUWA Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi ametawazwa rasmi kuwa Chifu wa Mbeya na kupewa jina la Chifu Mwalembe ikiwa ni shukrani ya machifu na wazee wa Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na jamii kupunguza vitendo vya uhalifu mkoani hapa.
Tukio hilo lilifanyika kwenye hafla fupi ya kumuaga Kamanda Nyombi anayehamishiwa makao makuu ya Jeshi la polisi Tanzania, iliyoandaliwa na Muungano wa jamii Tanzania (MUJATA) kwa kushirikiana na machifu wote wa kutoka wilaya za Mkoa wa Mbeya.
Akimvisha mgololi mweupe na kumkabidhi mkuki Chifu Matunge ambaye naye alitawazwa kuwa chifu wa Mbeya, alisema rangi nyeupe ni ishara ya kumtakia afya njema na kwamba anakokwenda ni salama huku mkuki ukiwa ni silaha ya kuendelea na mapambano dhidi ya uhalifu.
Chifu Matunge alisema kitendo kilichofanywa na machifu wa Mbeya ni cha kipekee na nadra kuwatokea viongozi mbalimbali hivyo Kamanda Nyombi aelewe kuwa aliishi na kushirikiana vizuri na viongozi hao wa kijadi katika kupambana na maovu na kwamba kuna kila dalili ya kuendelea kupata mema aendako.
Alisema MUJATA kama chombo cha jamii kitaendelea kudumisha polisi jamii ili kukomesha maovu yote mkoani Mbeya kwa kushirikiana na kamanda wa polisi anayekuja pamoja na viongozi wa chama na serikali na amethibitisha kuwa muungano huo hauna itikadi za kichama,kabila wala ubaguzi wa rangi.
Naye Kamanda Nyombi, aliwashukuru machifu kwa kumuandalia hafla fupi ya kumuaga ambayo hakutegemea kupata heshima kubwa kama hiyo na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa muungano huo akiwa huko alikopangiwa.
"Ninaondoka kwa majonzi kutokana na kuishi nanyi vizuri kwa miaka mitatu niliyokuwepo hapa, nimeshirikiana nanyi katika kukomesha uhalifu kwa sababu wahalifu ni wake,waume na watoto zetu, ninyi ni mashahidi nondo sasa hakuna risasi mitaani za majambazi kupora, uchunaji wa ngozi na uhalifu mwingine hakuna, ninaondoka kifua mbele", alisema.
Akikabidhi kuku aina ya jogoo mweupe Inspekta Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Elizabeth alisema huyo kuku anapowika alfajiri atakuwa akimkumbusha kuwahi kuamka asubuhi na kuendela na mapambano.
Kamanda Nyombi katika mabadiliko aliyoyatangaza Mkuu wa Jeshi la polisi IG Said Mwema alipangiwa kuwa Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa makosa ya jinai Tanzania ambapo aliyekuwa msaidizi wake mkoani Mbeya ambaye alipandishwa wadhifa na kuwa Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Kamanda Diwani atachukuwa nafasi yake.
No comments:
Post a Comment