Habari za Punde

Wanasheria Wasiowaaminifu Kikwazo Upatikanaji Haki

Na Mwanajuma Mmanga
KUKOSEKANA uadilifu miongoni mwa watendaji wa vyombo mbali mbali vinavyosimamia masuali ya sheria hapa nchini, ni baadhi ya sababu zinazoifanya jamii kukosa imani ya kuwasilisha taarifa za matukio ya uhalifu katika vyombo hivyo.

Wasaidizi wa Sheria (PARALEGALS), wanaoshiriki katika mafunzo ya siku mbili yenye lengo la kutafuta njia za upatikanaji wa misaada ya kisheria, walielezaa hayo huko katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni mjini hapa.

Mafunzo hayo yaliowashirikisha wasaidizi wa Sheria kutoka majimbo yote ya Unguja na Pemba, yameandaliwa kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Kituo cha Huduma za sheria Zanzibar ( ZLSC) na Mfuko wa wa kutoa fedha wa mashirika yanayotoa misaada ya kisheria (LSF).

Walisema pamoja na kuwa Mahakama ni moja kati ya mihimili mikuu ya dola yenye kazi ya kutafsiri sheria, kusimamia haki, bado baadhi ya watendaji wa chombo hicho wamekuwa hawawajibiki ipasavyo katika utekelezaji wa kazi zao, na badala yake wameegemea zaidi katika kujipatia maslahi yao binafsi.

Walisema baadhi ya Mahakimu na Makarani wa Mahakama nchini si waaminifu, wakihusishwa kuhusika na vitendo vya kupindisha sheria pamoja na upotevu wa makusudi wa vielelezo kwa lengo la kuharibu kesi zinazowasilishwa kwao.

Aidha walisema baadhi ya watendaji katika jeshi la polisi, hususan wapelelezi wa kesi wamekuwa na tabia ya kuchelewesha upelelezi na hatimae kusababisha kesi kufutwa mahakamani.

Aidha watendaji hao wanadaiwa kujenga mashirikiano na mahakimu kwa kuaandaa mianya inayopelekea kesi hizo kukosa ushahidi wa kutosha, hatua inayotoa fursa kwa washitakiwa kutopatikana na hatia.

Katika hatua nyengine washiriki hao waliomba kupatiwa ofisi katika majimbo yao pamoja na vifaa vyote vinavyohitajika ikiwemo vile vya mawasiliano ili iwe rahisi kwao kuwasiliana na jumuiya mbali mbali zinazosimamia utetezi wa haki katika jamii.

Wamekiomba Kituo cha Huduma za sheria Zanzibar na wafadhili mbalimbali kuwawezesha kimaslahi ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

“Tunaomba kuwepo mazingira mazuri na mahusiano mazuri baina yetu na vyombo vyengine vinavyosimamia sheria vikiwemo masheha, Polisi, wanasheria, Wakuu wa wilaya pamoja na Wakuu wa mikoa”, alisema Abdalla Juma kutoka jimbo la Mkwajuni.

Mapema Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC), Harusi Miraji Mpatani, alisema kuwepo kwa wasaidizi wa sheria katika majimbo mbali mbali nchini, kutawezesha wananchi kuwa na uelewa juu ya sheria mbali mbali zinazowatawala na kumudu kutatua matatizo wanayoyapata.






No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.