Na Rose Chapewa, MOROGORO
MAMLAKA ya Usafirishaji wa Majini na Nchi kavu (SUMATRA) Mkoa wa Morogoro, kwa kushirikiana na jeshi la Polisi kitengo cha Usalama barabarani imesema itafanya msako maalumu kubaini madereva wasio na mikataba ya ajira.
Hayo yalibainishwa na Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka hiyo Mkoani hapa, Walukani Luhamba wakati akizungumza na gazeti hili, nakwamba msako huo utaanza Mei 28 mwaka huu.
Alisema madereva watakaobainika kutokuwa na mikataba ya ajira iliyopitishwa na idara ya kazi kisheria magari yao yatakamtwa, bila kuangalia ikiwa ni gari la abiria ama mizigo.
“Kama dereva hana mkataba wa ajira, inamaana hata gari analoendesha halina leseni ya usafirishaji, tutafuatilia kwa mmiliki kwa nini dereva wake hana mkataba huo”, alisema.
Luhamba alifafanua kuwa uchunguzi ukifanyika na kubaini kuwa mmiliki aliidanya Mamlaka hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni ya usafirishsji.
Aidha Ofisa huyo pia alizungumzia magari madogo yanayofanya safari zake ndani na nje ya Manispaa ya Morogoro ambapo aliwataka madereva wa magari hayo kuhakikisha wanatoa tiketi kwa abiria.
Alisema magari hayo yamekuwa yakipuuza agizo hilo na kwamba msako huo pia utawalenga ili kubaini wote wanaopuuza agizo hilo, ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutozwa faini.
No comments:
Post a Comment