STATE HOUSE ZANZIBAR OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 22.5.2012
OFISI ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo imeeleza vipaumbele ilivyojiwekea kwa mwaka ujao wa fedha ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kufikia kiwango cha asilimia 20ya pato la Taifa, kwa kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato na kuendeleza elimu kwa walipa kodi.
Uongozi wa Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo ulieleza hayo leo katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa kuangalia robo tatu ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2011-2012 na kulinganisha na robo ya kwanza na ya pili pamoja na vipaumbele na malengo kwa mwaka wa fedha 2012-2013.
Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo Mwenyekiti wake ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein pia, ulihudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Abdulhamid Yahya Mzee pamoja na Mshaurui wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa na Uwekezaji Balozi Mohammed Ramia.
Uongozi huo, chini ya Waziri wake Mhe. Omar Yussuf Mzee, ulieleza kuwa kipaumbele chengine ni pamoja na kuendelea kulipa kwa wakati mishahara na mafao ya wastaafu pamoja na kuendeleza uhakiki wa mali za serikali na kuhakikisha mali yote imewekwa thamani kama sheria inavyotaka.
Waziri huyo alieleza kuwa pamoja na mambo mengineyo Wizara hiyo itaendelea kushajiisha sekta binafsi katika kushiriki zaidi katika kuendeleza uchumi wa Zanzibar na kudhibiti mfumko wa bei.
Aidha, Wizara hiyo ilieleza kipaumbele chake katika kusimamia uratibu wa mipango ya kimataifa, sera na kuimarisha utendaji wa Tume ya Mipango sanjari na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa MKUZA na kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
Pia, uongozi huo ulieleza hatua inazoziendeleza katika kusimami na kutoa taarifa ya mwenendo wa uchumi nchini ikiwemo maendeleo na ukuaji wake, mfumko wa bei, mwenendo wa biashara ya ndani na nje, hali ya uwekezaji na ukuzaji rasilimali nchini.
Kwa upande wa Shirika la Bima Zanzibar, uongozi huo ulieleza lengo lake la kuanzisha huduma za Bima Kanda ya Kusini huko Tanzania Bara sanjari na kutafuta mtaalamu wa kuanzisha Bima ya Kiislamu baada ya kupitishwa Sheria.
Uongozi huo pia, ulieleza lengo lake la kuendeleza maeneo huru ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kujenga jengo la kitega uchumi huko kisiwani Pemba, kujenga maghala, kuhifadhi eneo huru la uchumi la uwanja wa ndege , kuendeleza ujenzi wa afisi iliopo Tibirinzi na mengineyo.
Pia, ulieleza lengo lake la kushajiisha zaidi wawekezaji ili kuongeza uwekezaji wa utalii wa daraja la juu pamoja na kutangaza fursa zilizopo kwenye uvuvi, viwanda na huduma za afya, mawasiliano, kilimo na elimu
Aidha, kwa upande wa Ofisi ya Mtwakimu Mkuu wa Serikali, Wizara hiyo ina lengo la kuanzisha kitengo cha Elimu, Mawasiliano na Habari ili kuweza kuwasilisha takwimu zinazozalishwa kwa wadau wote mpaka katika ngazi ya nchi.
Wizara hiyo pia, ilieleza lengo la chuo chake cha Usimamizi wa Fedha Zanzibar la kuongeza uwezo wake wa kufundisha katika zama za utandawazi ikiwa ni pamoja na kutengeneza Mitaala ya Shahada ya Kwanza ya Teknohama na Shahada ya Ununuzi na Ugavi.
Nae Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa na Uwekezaji Balozi Mohammed Ramia, alieleza kuwa ipo haja kwa Mamlaka ya Kuendeleza Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), kuandaa kongamano hapa nchini ili watu waliowengi nchini na hata nchi za nje waweze kushiriki.
Pamoja na hayo, Balozi Ramia alieleza kuwa umefika wakati wa kuangalia uwekezaji katika maeneo mengine likiwemo eneo la bahari kwani linaweza kutumika vizuri.
Kwa upande wake Rais Dk. Shein ametoa pongezi kwa Wizara hiyo kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja kwa Wizara hiyo kuishirikisha sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wa nchi ikiwa ni pamoja na kuishauri ama hata kuiwezesha iwapo hali itaweza kuruhusu.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwashajiisha wawekezaji wazalendo na kusisitiza kuridhishwa kwake na mipango, sera na mikakati ya Wizara hiyo katika kuelekea Dira ya 2020.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment