Habari za Punde

Ahmad Kuwania Tuzo Mwanamichezo Bora

 Dar es Salaam
MSHINDI wa medali ya dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki mwaka jana yaliyofanyika Athens, Ugiriki Ahmad Bakari Khamis, ni miongoni mwa wanamichezo watakaowania tuzo zinazoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) mwaka 2011.

Ahmad (19) ambaye ni mlemavu wa akili, alishika nafasi ya kwanza katika mashindano ya mbio fupi kwenye michezo hiyo, medali ambayo ilikuwa pekee kwa timu ya Tanzania kushinda.

Hafla ya kuwania tuzo ya mwanamichezo bora wa Tanzania mwaka 2011 ambayo inadhaminiwa na kampuni ya TBL kupitia kinywaji chake cha Serengeti, imepangwa kufanyika Juni 14, mwaka huu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Mbali na Ahmad, wanamichezo wengine wa Zanzibar walioteuliwa kushiriki kinyang’anyiro hicho, kupitia mchezo wa judo Mbarouk Suleiman Mbarouk, Mohammed Khamis Juma na Azzan Hussein Khamis katika uzito tafauti.

Wengine ni Farhan Abubakar kutoka timu ya Mafunzo kwa mchezo wa mpira wa wavu upande wa wanaume, na Aggrey Morris, mwakasoka anayekipiga na klabu ya Azam FC.

Aidha kwenye orodha hiyo, yumo mchezaji Faraji Shaibu Khamis ambaye anawania tuzo kupitia mchezo wa mpira wa mikono kwa wachezaji wanaume, akitokea klabu ya Nyuki ya Zanzibar.

Michezo mbalimbali itashindaniwa tuzo, ambayo ni mpira wa kikapu, netiboli, gofu, olimpiki maalumu, riadha (kisahani, tufe, mkuki), paralimpiki, ngumi za ridhaa na kulipwa, kuogelea, judo na mpira wa wavu.

Michezo mingine ni tenisi, baiskeli, wachezaji wa Tanzania wanaocheza nje, wachezaji wa nje wanaocheza Tanzania, soka la wanawake, mpira wa mikono, kriketi.

Taarifa hizi ni kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo Masoud Sanani, na mwanamichezo bora wa jumla atazawadiwa donge la dola elfu nane za Kimarekani (zaidi ya shilingi milioni 12).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.